Saturday, June 1, 2013

Kiingereza cha dunia kinavyotutesa Waswahili

Hili linafahamika na hata viongozi wetu wamekuwa wakisema kuwa Kiswahili ndiyo lugha yetu yaTaifa.
Binafsi siamini kama kauli hii ina ukweli ndani yake kwa sababu Watanzania tumeshindwa kukienzi Kiswahili, licha ya kuwa lugha hiyo ni ya 10  duniani kwa idadi ya wazungumzaji, inazungumzwa na watu takriban 100 milioni.
Hivi karibuni Serikali ilieleza mkakati wake wa kuhakikisha Kiswahili kinazungumzwa katika  makongamano ya kitaifa na kufundishia, lakini binafsi siamini kama juhudi hizo zitaweza kuifanya lugha hiyo ilingane na hadhi yake ya kuwa moja ya lugha 10 duniani.
Serikali imetufumbua macho baada ya kueleza wazi kuwa Kiswahili ni kati ya lugha 10 zinazozungumzwa zaidi duniani, lakini wakati huohuo  wanaofundisha Kiswahili katika vyuo vikuu nje ya nchi siyo Watanzania, lakini kama hilo halitoshi hata viongozi wetu wakiwa katika makongamano nao wanakikacha Kiswahili na kuzungumza Kiingereza hivyo kuwaacha kwenye mataa Waswahili.
Zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanazungumza Kiswahili, lakini hakuna juhudi za makusudi za kuimarisha lugha hii.
Huwa najiuliza maswali mengi ninapowasikia viongozi wetu wakisema kuwa Kiswahili ndiyo lugha ya taifa.
Kama jibu ni ndiyo, inakuwaje  sekta nyeti za nchi hii kama Mahakama, Serikali na taasisi nyingi wanatumia lugha ya Kiingereza. Sijui matumizi haya ya Lugha ya Kiingereza yana lengo gani katika nchi hii ya Waswahili inayoaminika kuwa ndiyo chimbuko la Kiswahili duniani.
Sikatai, wapo wanaokitetea Kiingereza kwamba ni lugha ya kibiashara duniani hivyo Watanzania ni lazima wajifunze na kukijua kwa ufasaha.
Sasa kama ukweli ndiyo huo kuna ulazima gani kwa Kiingereza kutumika mahakamani wakati idadi kubwa ya wanaokwenda mahakamani ni Waswahili wasiokijua kwa ufasaha Kiingereza.

 Hivi sasa taifa letu halijui lisimame wapi, na nathubutu kusema kwamba kuendekeza Kiingereza ndiyo chanzo cha idadi kubwa ya wanafunzi kushindwa kufanya vyema katika masomo yao, Wengi wao hivi sasa wanakariri tu maswali na majibu,  ukiligeuza swali wanashindwa kulifanya kwa sababu ya kutojua Kiingereza. Mwanafunzi anaanza darasa la kwanza hadi la saba akifundishwa kwa kutumia lugha ya Kiswahili, anapoanza kidato cha kwanza anakutana na lugha ya Kiingereza.
Kwa mantiki hiyo  ni wazi kuwa hatafanya vyema katika masomo yake, hasa kama hatakuwa na msingi mzuri katika lugha ya Kiingereza.
Kiswahili kikipewa kipaumbele taifa litapiga hatua kubwa kimaendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu.
Nasema hivyo kwa sababu maarifa na lugha ni vitu viwili tofauti. Hivyo mtu anapofundishwa somo la Jiografia, Historia, Fizikia  kwa Kiswahili ataelewa zaidi na atapata  maarifa yatakayomwezesha kunufaika yeye na jamii inayomzunguka.

Source Mwananchi

No comments:

Post a Comment