Friday, October 25, 2013

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA BODA BODA ADAI ALIPEWA MASHARTI NA SANGOMA WAKE.

 PICHA ZA MATUKIO SIKU AMBAYO MAUAJI YA BODA BODA
 KISU KINACHODAIWA KILITUMIKA KUMUUA BODA BODA
MAITI IKIWASILI HOSPITALI YA WILAYA SERENGETI


Oktoba 25,2013
MTU mmoja anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa boda boda mjini Mugumu Wilayani Serengeti Gwitembe Yagera(60)amekamatwa na kudai kuwa aliambiwa na Sangoma wake aue mtu yeyote ili apate utajiri.
 
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara Fernandi Mtui alithibitisha kukamatwa kwa Mtuhumiwa huyo anayeshikiliwa na polisi wilayani Serengeti Elias Jonathan(23)mkazi wa kijiji cha Burunga kata ya Uwanja wa Ndege wilayani hapa,amekamatwa hivi karibuni eneo la Sirari na kuwa uchunguzi zaidi unaendelea .
 
Habari kutoka ndani ya jeshi la polisi zinadai kuwa mtuhumiwa huyo alisema kuwa alitekeleza mauaji hayo kutokana na masharti ya mganga wake ambaye anasakwa na jeshi la polisi,kuwa afanye mauaji pekee yake na kwa mtu yeyote ndipo na atapata  utajiri.
 
“Alisema aliamua kumkodi huyo boda boda kwa kuangalia umri wake kwa madai kuwa anakwenda Mosongo…kufika eneo la Nyisense Nyichoka akamchoma kisu na kusababisha mauaji yake na kukimbia akitelekeza kisu hapo na hakuchukua kitu chochote”kilisema chanzo cha uhakika kutoka ndani ya jeshi la polisi.
 
Kuhusu kukamatwa kwake  chanzo hicho kilisema baada ya kutenda unyama huo alitoroka hadi Sirari na ambako alihusika katika mauaji ya baiskeli na kukamatwa ,na baba yake alitoa ushirikiano baada ya kujua kuwa anatafutwa kwa mauaji na kunaswa na kuletwa Mugumu kuhusiana na tuhuma hizo.
 
Oktoba 4,mwaka huu majira ya saa 8 arasili mtuhumiwa huyo anadaiwa alimkodi Yagera kwa sharti kuwa wakifika kijijini Mosongo angemlipa fedha yake,lakini kabla ya kufika inadaiwa alimchoma kisu eneo la kushoto chini ya ubavu na kusababisha kifo chake.
 
Na baada ya kutenda unyama huo hakuchukua kitu na kutokea na maiti yake iligunduliwa na wapiti njia ambao walitumia simu ya marehemu kuwataarifu viongozi wa chama cha waendesha pikipiki wilayani hapo,na askari polisi. 
 
Habari tulizozipata wakati tunaandaa taarifa hizi zinadai kuwa mtuhumiwa huyo amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi wilaya ya Serengeti kuhusiana na tuhuma hizo,hata hivyo hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.

No comments:

Post a Comment