Monday, April 7, 2014

MH Mkono awalilia wanawake wanaouawa Butiama


Na George Marato,Musoma
 
MBUNGE wa Musoma vijijini Nimrod Mkono,ameishutumu Serikali kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya mauaji ya kinyama na kikatili  wanafanyiwa wanawake katika baadhi ya vijiji vya tarafa ya Nyanja jimboni humo huku akisema Serikali imekuwa ikitumia nguvu kubwa kulinda wanyama pori kuliko binadamu.
 
Mkono ambaye kitalum ni mwanasheria,alitoa kauli hiyo juzi katika kijiji cha Mugango katika halmashauri ya Musoma wilayani Butiama baada ya watu wasijulikana kumnyonga hadi kufa kwa kutumia kanga yake mwanamke mmoja mkazi hicho Anastazia Mang’ombe (42) kabla ya kumbaka wakati akiwa shambani kwake.
 
Mauaji ya mwanamke huyo ni mwendelezo wa mauaji ya kinyama na kikatili yanayotokea katika vijiji vya mwambao wa ziwa Victoria vya Nyakatende,Etaro,Nyegina,Mkirira katika tarafa hiyo yakihusisha wanawake yakiwa ni ya pili kutokea katika kipindi cha wiki mbili tu baada ya mwanamke mwingine mkazi wa kijiji Kamguruki kata ya Nyakatende wilayani humo kuuawa pia kwa kunyongwa.
 
Alisema tangu kuibuka kwa wimbi la mauaji hayo ya kinyama ambayo hadi sasa yanahusishwa na imani ya kishirikina hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa na Serikali licha ya viongozi wake kutoa kauli za kisiasa ambazo zimeshindwa kumaliza mauaji hayo na hivyo kuongeza hofu kubwa kwa jamii hasa wanawake.
 
“Jamani mauaji haya ya wanawake mwisho wake utakuwa lini,hivi Serikali iko wapi,mbona tembo mmoja tu akiuawa tunasikia filimbi na ndege zinaruka huku na huku kuwasaka wauaji iweje leo binadamu hasa hawa wanawake wanauawa bila hatia hatujasikia serikali wala haijachukua hatua?
 
“Wakina mama zangu wanauawa,wanachinjwa kama kuku sijaiona Serikali ikichukua hatua,sasa ni wakati wa Waziri mkuu na Rais wetu waje hapo ili kutusaidia kukomesha mauaji hayo ya kikatili…hivi niwaweke wapi wakinama hao sasa wanaishi kwa hofu kubwa”alisema Mkono kwa uchungu huku akibubujikwa machozi.
 
Kwa sababu hiyo mbunge huyo alisema serikali inaonekana kuwapuuza wananchi hao wanauawa kinyama kwani ina vyombo vya kuwabaini wauaji wote na kuchukuliwa hatua za kisheria.
 
“Nakwenda bungeni kupigania hili kwani ni janga la kitaifa ikiwezikana serikali itangaze oparesheni maalum kama ilivyofanya katika kupambana na ujangili ndani ya hifadhi zetu,hatuwezi kuacha mama zetu wanauawa kiasi hiki cha kutisha,kwa kweli sitakubali tena wala kukaa kimya kwa jambo hili”alisema.
 
Kwa upande wake mwenyekiti mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Butiama  Angelina Mabula,pamoja na kulaani vikali mauaji hayo amewaka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuhakikisha wauaji hao wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
 
“Kwa kweli hali ni mbaya kweli,nawaomba muwe watulivu kwani matukio haya yametuchanganya,wiki iliyopita wanawake wawili wameuawa hivi hivi,ukiangalia matukio yote yanafanana na yanafanyika wazi sasa lazima tujiulize wote hapa kuna nini?
 
“Hata tufanyeje polisi hawawezi tosha kulinda wote lazima tuweka mikakati ya pamoja katika kushughulikia mauaji haya,kwa muda mfupi tu kwa eneo hili la kata nne wanawake wanane wameuawa kikatili na mauaji yote yanafanana”alisema DC Angelina.
 
Kwa sababu hiyo aliwaomba wananchi kutoa taarifa za kina kwa vyombo vya dola zikiwemo ofisi za viongozi katika kuhakikisha mauaji hayo yanakomeshwa.
 
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya alitoa agizo kwa wanaume kuwasindikiza wake zao mashambani na katika shughuli nyingene za kutafuta kipato wakati vyombo vya dola vikipambana na vitendo hivyo vya mauaji hayo.
 
Alisema viongozi wa Serikali sasa wameshindwa kuhamasisha shughuli za maendeleo kwani muda wote wamekuwa wakishughulikia matukio ya mauaji kila kukicha.
 
Kwa mujibu mujibu wa mkuu huyo wa wilaya hadi sasa watu watano wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji kama hayo huku wanne wakishikiliwa polisi kwa uchunguzi.
 
Naye katibu wa CCM wilaya ya Butiama Mercy Mollol,aliomba Serikali kutangaza eneo hilo kuwa kanda maalum ya kipolisi ili kuongeza idadi ya askari kwaajili ya kukabiliana na mauaji hayo.
 
“Kama chama tumesikitishwa sana na mauaji haya yanayoendelea katika eneo hili,sasa tunaitaka Serikali chini ya Mh Jakaya Kikwete na IGP Mango kutangaza oparesheni ya watu wanaua wanawake kabla hatujatangaza maandamano makubwa ya kupinga ukatili huu”alisema kiongozi huyo wa CCM.
 
Kamanda wa polisi mkoa wa Mara,kamishina msaidizi mwandamizi Ferdinand Mtui,akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba hadi sasa watu watatu wanashikiliwa kwa mahojiano.

No comments:

Post a Comment