Sunday, December 1, 2013

Watu wawili wauawa kwa kupigwa Risasi Serengeti

Serengeti
WAFANYABIASHARA wawili wilayani Serengeti  wameuawa katika mazingira na maeneo tofauti  mmoja kwa kupigwa risasi tatu  na watuhumiwa hawakuchukua kitu mwingine kwa kuporwa pikipiki,simu na maiti yake kutelekezwa   eneo la shule ya msingi Matare.

Polisi wilayani hapa wamethibitisha kutokea kwa mauaji hayo kwa tarehe na maeneo tofauti na kumtaja aliyeuawa kwa kupigwa risasi tatu ni Mugaya Marwa Mnata(37)aliyekuwa na duka la dawa baridi kijiji cha Rung’abure na Thomas Marwa Nyahure mkazi wa Matare na aliyekuwa na duka mjini Mugumu.

Kwa mjibu wa taarifa za kipolisi matukio hayo yametokea Novemba 26 na 28 ambapo maiti ya Nyahure ilikutwa imelazwa kifudifudi  eneo la shule ya Msingi Matare huku kichwani kukiwa na jeraha la kupigwa na kitu cha ncha kali,na Mnata aliuawa Novemba 28 kwa kupigwa risasi tatu ubavuni majira ya saa 3:30 usiku na kufa hapo hapo,ambapo maganda yalionekana ni silaha ni Smg.

Akizungumzia tukio la Mnata Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Rung’abure Charles Kibure alisema alikutwa na mauti muda mfupi baada ya kufunga duka lake akielekea nyumbani.

“Aliuawa eneo la stoo ya kijiji kitongoji cha Kwanina…watu wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa wamejificha walimpiga risasi tatu ubavuni na moja kuchana masikio kisha wakakimbia…haijajulikana nia yao maana inaonekana hapakufanyika uporaji”alisema.

Alisema wananchi walijitokeza muda mfupi baada ya kusikia mlio lakini watuhumiwa hawakupatikana na kumkuta ameishakata roho,”haya mauaji yanaacha maswali sana …maana marehemu alihamia hapa kibiashara miaka mitano iliyopita akitokea kijiji cha Kebweye wilayani Tarime….alikuwa mfamasia mzuri na alikuwa na wateja wengi sana “alisema Mwenyekiti.

Ofisa mtendaji wa kijiji hicho alisema kutokana na matukio ya mauaji kama hayo kujitokeza mara kwa mara ,waliitisha mkutano wa hadhara na wananchi wameahidi kufuatilia na kutoa taarifa za siri ili wahusika waweze kukamatwa kwa kuwa wanakijiji wanajawa na hofu.

Naye msemaji wa familia ya Nyahure Samweli Marwa alisema mdogo wake alitoka novemba 25 asubuhi mwaka huu kuwa anaenda dukani na hakurejea mpaka maiti yake ilipookotwa novemba 26 asubuhi kijijini hapo.

“Hatujajua chanzo cha mauaji hayo…maana hakuna mtu anahisiwa ama amekamatwa…sisi tulikuta maiti imelazwa kifudi udi kichwani kaumizwa na kitu cha ncha kali…pikipiki,simu aliporwa,fedha hatujui kama alikuwa nazo ama la…lakini kila mara tunapewa taarifa kuwa pikipiki imeonekana maeneo Fulani tukienda hakuna mafanikio”alisema Marwa ambaye ni kaka wa marehemu.

Michael Mwita jilani wa marehemu alisema kuwa kutokana na matukio kama hayo kujiridia rudia mara kwa mara,ameomba polisi wafanya uchunguzi wa kina ili kukomesha mauaji kama hayo.

Polisi wanaendelea na uchunguzi na hakuna mtu anashikiliwa kwa matukio yote mawili.
 

No comments:

Post a Comment