Sunday, December 1, 2013

Asomewa mashitaka ya kubaka na kulawiti akiwa wodini

SERENGETI.
 
 
MAHAKAMA ya Hakimu wa Wilaya ya Serengeti imelazimika kuhamia hospitali ya wilaya ya Nyerere na kumsomea mashitaka  Marwa Ibrahimu(30)mkazi wa Kijiji cha Matare wilayani hapo,anayekabiliwa na mashitaka mawili  ya kubaka na kulawiti mtoto wa miaka 12.
 
Hakimu wa Mahakama hiyo Franco Kiswaga alilazimika kuhamia hospitalini hapo kutokana na mtuhumiwa kushindwa kufikishwa mahakamani kufuatia kupigwa na kuumizwa na wananchi walipomkuta anafanya unyama huo .
 
Mwendesha mashitaka wa polisi Jakobo Sanga akisoma maelezo ya shitaka hospitalini hapo alisema mnamo novemba 19 mwaka huu majira ya saa 2 usiku katika kitongoji cha Bukore kijiji cha Nyichoka kata ya Kyambahi mtuhumiwa anadaiwa kumbaka na kumlawiti mtoto wa miaka 12.
 
Akisoma hati ya mashitaka alisema kuwa mshitakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili ikiwemo la ubakaji na kulawiti mtoto kinyume cha maumbile ikiwa ni kinyume cha sheria.
 
Na kuwa mtuhumiwa akijua kuwa ni kosa alimkamata mtoto huyo na kumwingilia kwa nguvu na kumsababishia majeraha sehemu za siri na haja kubwa mtoto huyo. 
 
Mwendesha mashitaka alisema kuwa upelelezi umekamilika,hata hivyo mshitakiwa alikana mashitaka  na hakimu kuamru apelekwe mahabusu atakapopona  hadi desemba 5 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

No comments:

Post a Comment