Friday, May 3, 2013

WAANDISHI WA HABARI MARA WAASWA



 Augustine Mgendi-Mwanahabari Mara
 Belensi Alkaid-Mwanahabari Mara
 George Marato-Mwanahabari Mara
 Florence Focus -Mwanahabari Mara
 Shomar Binda-Mwanahabari Mara

 Mwenyekiti wa MRPC Emanuel Bwimbo kushoto na Kaimu katibu wa MRPC Raphael Okello Kulia


Waandishi wa habari  nchini wameaswa kupendana ikiwa ni mikakati ya kuendeleza taaluma hiyo pamoja na kuthamini Kazi ya Uandishi wa habari hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari Mkoani Mara (MRPC) Emanuel Bwimbo katika Bwalo la Polisi mjini Musoma mkoani Mara Ikiwa ni Maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari  duniani ambayo hufanyika kila Mwaka Mei 3.

Alisema taaluma ya habari ni taaluma nyeti hapa nchini ambayo inategemewa na Jamii kubwa hasa iliyopo Vijijini lakini baadhi ya Waandishi wa habari wamekuwa hawaithamini taaluma hiyo na hivyo kupelekea Jamii kuiona ni taaluma ya Kawaida wakati ina unyeti wake.

“Mimi nashangaa sana maana hii taaluma ni nyeti sana hapa nchini na inategemewa na asilimia kubwa hasa Vijijini lakini sisi waandishi wa habari hatuitahamini taaluma hii kwanini?” alisema Bwimbo 

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amelaani tabia ya Mkuu wa Mkoa wa Mara John Gabriel Tuppa kwa tabia yake ya kuchagua vyombo vya habari wakati akijua kuwa kufanya hivyo kunaleta matabaka kwa Waandishi wa habari.

Biwimbo alisema kuwa tabia ya Mkuu wa Mkoa kuchagua vyombo vya habari mbali na kuleta Matabaka lakini pia husababisha Mahusiano kati ya Waandishi wa habari na Ofisi ya Mkoa kuwa Mabaya na hivyo kulaani kitendo hicho.

“Tunamshangaa sana Mkuu wa Mkoa maana siku hizi amekuwa na tabia ya kuchagua vyombo vya habari lakini hiyo haitoshi ameanzisha tabia nyingine akialikwa sehemu anawaeleza wahusika hao vyombo vya habari vya kuita katika hili hatukubaliani nalo kama Waandishi” alisema Bwimbo.

Wakichangia katika Kongamano hilo baadhi ya Waandishi wa habari kutoka Mkoani Mara wamesema tabia aliyoianzisha katika kubagua Vyombo vya habari si nzuri na hivyo kusema hatua hiyo haitaleta Mauhusiano mema katika Mkoa wa Mara.
Waliongeza kuwa haitakuwa rahisi Mwandishi wa habari kuandika habari ambazo Mkuu wa Mkoa anazitaka huku wakiongeza kuwa wao watasiamam Misingi ya habari.

“Haiwezekani Mkuu wa mkoa atake waandishi wa habari wafanye kile ambacho anakitaka yeye kwani kufanyaa hivyo ni kukiuka Misingi ya uandishi wa habari”

Katika Kongamano hilo Waandishi wa habari wamependekeza kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Mara kujadili hilo na baada ya hapo Chama cha Waandishi wa habari Mkoani Mara watatoa tamko.

Kwa upande wake Kaimu katibu Mkuu wa Chama hicho kutoka Wilaya ya Bunda Mkoani Mara  Raphael Okello alisema suala la Maadili linapaswa kuzingatiwa katika taaluma ya habari ikiwa ni njia ya kuipa heshima taaluma hiyo.

Alisema kumekuwepo na baadhi ya Waandishi ambao wamekuwa wakikiuka Misingi ya taaluma ya habari na hivyo kuendelea kuipaka Matope taaluma hiyo,aidha kuhusu baadhi ya wanahabari wanaotumia nafasi hiyo kutisha jamii Kaimu katibu mkuu huyo alisema kuwa hiyo ni tabia mbaya ambayo haipaswi kufumbiwa Macho.

“Baadhi ya Waandishi wamekuwa wakiipaka Matope taaluma hii kwa kukiuka Maadili hivyo basi ni vyema kila Mwandishi wa habari akafuata misingi ya taaluma hii ya habari” alisema Okello

No comments:

Post a Comment