Tuesday, April 30, 2013

Rais masikini zaidi duniani

NCHI ya Uruguay yenye raia takribani milioni 4, inatajwa kuwa na bahati ya kuwa na Rais asiye na chembe ya tamaa. Hana makuu, kiasi kwamba anatajwa kuwa ndiye Rais masikini zaidi kuwahi kutokea duniani.

Huyu si mwingine, bali ni Jose Mujica, Rais wa sasa wa Uruguay ambaye pia ni Rais wa 40 wa nchi hiyo. Tangu aingie madarakani Machi mosi mwaka 2010, amekuwa akionekana kuwa kiongozi wa tofauti kabisa, tofauti na waliomtangulia.

Mathalan, baada ya kufanikiwa kuishika nchini, hakuwa na tamaa ya kukimbilia Ikulu, yeye alichokifanya ni kuamua kuishi katika makazi yake yaleyale, katika nyumba ya mkewe iliyoko shambani, nje ya Jiji la Montevideo.

Kwa ujumla, anapenda maisha ya kawaida, maisha ya kuwahurumia wengine na kujitahidi kuonesha kwa vitendo.

Ni vigumu kuamini, licha ya kuwa ni Rais wa nchi, amejishusha mno kiasi cha mara kadhaa kuonekana akijichanganya na raia wake katika shughuli za ujenzi wa taifa, ikiwamo ujenzi wa barabara, kulima mashamba ya mfano.

Na wakati mwingine, anapougua huwahi kupanga mstari ili kuonana na daktari, akichelewa anapanga mstari kusubiri zamu yake.

Ni Rais pekee ambaye ameamua kutoa mshahara wake kwa zaidi ya asilima 90 kugawana na watu masikini wa nchi yake, kwamba fedha hizo huingizwa katika vikundi mbalimbali vya maendeleo.

Akiwa amepangiwa na Bunge kupokea dola za Kimarekani 11,000 (sh milioni 17.6 kwa fedha za Tanzania) kwa mwezi, hajawahi kupokea fedha hizo na ameiamuru Hazina kuzipeleka fedha hizo kwa wananchi masikini.

Yeye hupokea shilingi milioni 3 tu, tena hizi akizitumia kwa ajili ya mafuta ya gari lake alilonunua na mkewe aina ya Volkswagon Beetle maarufu kama `Mgongo wa Chura’. Gari hilo lenye umri wa miaka 23, ndio utajiri pekee anaojivunia.

Hana kingine anachokimiliki. Hana akaunti benki, hana nyumba yake binafsi, wala mali nyingine ya aina yoyote aliyojilimbikizia. Kuhusiana na gari lake lenye thamani ya dola za Kimarekani 1,900 (Sh milioni 3), ambalo analiendesha mwenyewe, anasema:

“Niko mimi na mke wangu, wawili tu, gari kubwa la nini, sina haja nalo, sitaki kuwaibia wananchi, kunichagua tu kuwaongoza ni sifa pekee, tena kubwa inayokaribia utukufu wa kawaida, sasa zaidi ya hapo nini…

“Nahitaji sana kuwatumikia wananchi wa Uruguay, sio kuwanyonya wala kuwaibia au kuwa mwanya wa kuchuma na kujifurahisha mimi, mke wangu, watoto wangu na ndugu zangu, sioni haja hiyo na sitaki kuwa mnyonyaji kamwe,” anasema Rais Mujica. Anasisitiza anayafurahia maisha ya kawaida, hivyo haoni shida kuishi na watu wa kawaida mtaani kwake, kupiga nao porojo na hata kushirikiana katika shughuli za kijamii pale inapolazimu.

“Nikiwa na akaunti benki, nikiwa na magari makubwa, nitakuwa nakaribisha ushawishi wa kuwa mwizi, kuwaibia wananchi wangu, sitaki chochote,” anaongeza Rais huyo ambaye hata anapoamua kunyoa nywele zake, hahitaji kinyozi maalumu, bali yeyote anayejua kunyoa anamwita nyumbani kwake aweze kumnyoa.

Staili ya maisha ya Rais huyo inaonekana pia kumwingia mkewe ambaye pia tofauti na wake wengine wa marais, yeye hajipambi kwa dhahabu, almasi wala aina nyingine ya vito vya thamani.

Anashirikiana na mumewe katika shamba lao la maua katika makazi yao, huku Rais Mujica wakati mwingine akifanya usafi wa nyumba na hata kumwagilia maua. Hayo ndiyo maisha ya Jose Mujica, Rais wa 40 wa Uruguay ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 77, lakini licha ya kupigania mno kuingia Ikulu, ameonesha kutokuwa na kiu ya utajiri, hataki kujikweza na wala kuonekana ni tofauti na watu wengine.

Ndiyo maana ameonekana kuwa Rais wa ajabu, akitajwa pengine kuwa ndiye asiye na makuu na masikini kuliko wote duniani. Hata vaa yake ni ya kawaida, mara nyingi akiingia ofisini na mavazi ya kawaida, lakini mara moja moja tu, akivalia suti na tai hasa anapokuwa na ugeni mzito.

Angalau Makamu wake, Danilo Astori anaonekana na `ufisadi’ kidogo, kwani ana nyumba yenye thamani ya dola 250,000 (Sh milioni 400) na gari kama la milioni 30 hivi. Je, kuna wengine wenye staili ya maisha ya Rais Mujica? Yawezekana, lakini kwa sasa imeonekana hakuna kama Mujica.

No comments:

Post a Comment