Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
Sekunde, dakika, saa zazidi kukatika
kuelekea mpambano mkali wa ligi kuu soka Tanzania bara baina ya mabingwa
watetezi wa ligi hiyo wekundu wa msimbazi Simba dhidi ya mabingwa mara
mbili wa kombe la mapinduzi na wawakilishi pekee wa Tanzania katika
michuano ya kimataifa, Azam fc kwenye uwanja wa kisasa wa taifa jijini
Dar es salaam.
Azam fc na Simba kwasasa zina upinzani mkubwa sana na kila zinapokutana hakika kipute kinakuwa kikali zaidi ya kawaida.
Simba wanaingiwa uwanjani wakiwa tayari
wameshapoteza ubingwa na sasa wanahitaji hata nafasi ya pili ili kupata
nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa mwakani wakati lambalamba wao
wapo nafasi ya pili na pointi 46 wakihitaji kushinda ili kwasogelea
vinara wa ligi hiyo Dar Young Africans.
Kikosi cha Azam kinaonekana kuwa imara
zaidi msimu huu kutokana na matokeo wanayopata katika mechi za ligi kuu
na michuano ya kombe la shirikisho, wakati Mnyama pori anahaha kweli
kutengeneza kikosi kipya baada ya wachezaji wengi `Mafaza` kutemwa na
kocha wake Patrick Liewig kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Mechi tatu zilizopita Simba ilicheza
bila wakongwe wake, Mwinyi Kazimoto Mwitula, Amir Maftah, Ramadhan
Chombo `Redondo`, Haruna Moshi Shaban `Boban`, Ferlix Mumba Sunzu,
Komanbil Keita, Juma Said Nyoso na Abdallah Juma baada ya kocha Liewig
kuwapiga chini.
Wachezaji Juma Kaseja, Mrisho Khalfan
Ngasa `Anko`, Amri Athman Kiemba, Shomary Kapombe Jr, Masoud Nassor
Cholo, walibakishwa kwenye kikosi hicho na kucheza michezo yote mitatu
dhidi ya Coastal union, Kagera Sugar na Toto Africa.
Kwa sasa Kazimoto na Sunzu wamerejeshwa
katika kikosi cha Simba na wanaweza kucheza katika mchezo wa leo endapo
mwalimu utapiga hesabu zake vizuri.
Kwa upande wa Azam fc , wao wako kamili
kado baada ya nyota wake Said Morad, Erasto Nyoni, Aggrey Morris,
Deogratius Munish `Dida` kurejeshwa kikosini baada ya TAKUKURU kushindwa
kuwakuta na hatia ya kula mlungula kama walivyoshitakiwa na klabu yao.
Mbali na nyota hao kuwepo, klabu hiyo
ina wachezaji hatari katika kufumania nyavu, John Rafael Bocco, Brian
Umony, Hamphrey Mieno na Kipre Herman Tchetche.
Lakini wapo wengine machachari kama
Abubakar Salum `Sure Boy`, Michael Bolou, Himid Mao, David Mwantika,
Khamis Mcha `Vialli` na wengineo.
Hakika mpambano huu ni mkali sana na
timu zote zitahitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya msimamo
wa ligi kuu soka Tanzaniania bara inayoelekea ukingoni.
CHELSEA V MAN CITY WEMBLEY HOMA YAPANDA KWA KASI KUBWA!!
Na Supersport.com
Mabingwa watetezi wa kombe la FA
nchini England watakuwa kibaruani leo hii majira ya saa 12 jioni katika
uwanja wa taifa wa Wembley kupepetana na mabingwa watetezi wa taji la
ligi kuu soka nchini England, klabu ya Manchester city mchezo wa nusu
fainali ya pili ya FA.
Miamba hiyo imeshindwa kupambana
na mashetani wekundu kuwania taji la ligi kuu msimu huu ingawa Chelsea
wamefika hatua ya nusu fainali ya ligi ya UROPA, lakini mchezo huu
utakuwa muhimu kwao wote ili kumaliza msimu angalau na kikombe kimoja.
Mshindi wa mchezo wa leo
utakumbana naWigan Athletic katika mtanange wa fainali baada ya klabu
hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya daraja la
Championship, Millwall na kutinga hatua ya fainali.
Kocha wa muda wa Chelsea Rafael
Benitez na wa City Roberto Mancini wote kwa pamoja wanawania kutwaa
kombe kwa mara ya pili wakifanya kazi nchini Uingereza.
Mwishoni mwa mwezi februari mwaka
huu timu hizo zilikutana katika dimba la Etihad katika mchezo wa ligi
kuu na kushuhudia City wakiwabamiza wapinzani wao mabao 2-0, lakini
Benetez amesema amejifunza kwa kiasi kikubwa.
“Tunajua itakuwa mechi ngumu,
lakini ni nusu fainali yenye ushindani mkubwa”. Alisema Mhispania huyo
aliyetwaa ubingwa wa kombe hilo mwaka 2006 akiwa na wekundu wa Anfield,
klabu ya Liverpool.
Benetez aliongeza kuwa City ni
timu nzuri, ina kikosi bora na kocha mzuri mwenye uzoefu mkubwa, lakini
watajituma zaidi endapo wanataka kuibuka kidedea katika kipute hicho.
City wanaingia uwanjani wakiwa na
kumbukumbu nzuri ya kuwafumua watani zao wa jadi Manchester United mabao
2-1 katika uwanja wa Old Traford jumatatu ya wiki hii mchezo wa ligi
kuu soka Uingereza.
Mancini amekuwa na presha kubwa
baada ya kuweka rehani ubingwa wake mbele ya united, lakini bado ana
nafasi ya kujikusanyia kombe la tatu ndani ya miaka mitatu.
Kocha huyo aliondoa ukame wa City
kutotwaa ubingwa wa kombe la FA kwa miaka 35 baada ya kuiongoza klabu
yake kunyakua ubingwa mwaka 2011 akiwafunga Stoke city mchezo wa
fainali.
Mancini alisema, “nadhani kucheza
Wembley ni bonge la mechi kwa mashabiki wote wa soka hivyo ni nafasi
muhimu kushuhudia mechi hiyo ya nusu fainali”.
Kocha huyo aliongeza kuwa kila
kombe ni muhimu kwa timu zote, lakini kwa upande wao ni muhimu zaidi
kwani wana nafasi ya kutinga fainali na kubeba kombe hilo kwa mara ya
pili ndani ya miaka mitatu.
SHEHATA AULA MUNICH 1860, SASA MSHAURI WA BENCHI LA UFUNDI!!
Na mtandao
Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya
Misri “Mafarao” Hassan Shehata ameteuliwa kuwa mshauri wa benchi la
ufundi la klabu ya Munich 1860 inayoshiriki ligi daraja la pili nchini
humo
Klabu hiyo imempata Shehata shavu la
kuwa mshauri mkuu wa timu zote klabuni hapo yaani timu ya kwanza, ya
pili na kikosi cha vijana.
Kocha huyo alisafiri kwenda ujerumani
ijumaa ya wiki hii na alianza kazi kwa kuangalia mchezo wa klabu hiyo na
kuandika ripoti yake anayotaraji kuiwasilisha kwa viongozi wake.
“Niko hapa kuisaidia timu irejee
Bundesliga, Munich 1860 ni timu kubwa sana na nitafanya kila
linalowezekana kurudisha heshima ya klabu hii”. Shehata ameuambia
mtandao wa Supersport.com
Kocha huyo ameongeza kuwa “nitawasoma
wachezaji wote na nitahudhuria mechi zote za klabu hii na baada ya hapo
nitakaa chini kupanga mipango thabiti ya kuisaidia timu yangu”.
Munich 1860 inayojulikana kwa jina la TSV Munchen iliundwa miaka 152 iliyopita na makao makuu yake ni jijini Munich Ujerumani.
Timu hiyo inacheza ligi ya daraja la pili ya Bundesliga tangu msimu wa mwaka 2003-2004.
No comments:
Post a Comment