Kocha wa Manchester United Sir
Alex Fergusson amekanusha taarifa zilizosambaa kwenye vyombo Vya habari
barani ulaya za klabu yake kuwa mbioni kumsajili mshambuliaji wa
kimataifa wa Colombia na klabu ya Atletico Madrid Radamel Falcao.
Fergusson amekanusha taarifa
hizo kwenye mkutano na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa yeye
mwenyewe ameshangazwa na taarifa hizo ambazo amethibitisha kuwa hazina
ukweli wowote kwani hadhani kama United ina nafasi ya mshambuliaji
mwingine .
Wiki iliyopita gazeti la
michezo la Hispania Marca liliandika taarifa kuwa Manchester United
inafanya mpango wa kumsajili Falcao ambapo ilikuwa tayari kulipa paundi
milioni 27 pamoja na mshambuliaji wa Mexico Javier Hernandez Chicharito .
Gazeti hilo (Marca) lilisema
kuwa United tayari imeanza kufanya mazungumzo na Atletico Madrid ambapo
mwandishi wa habari na mchambuzi maarufu wa soka nchini Hispania
Guillaume Balague alithibitisha uwepo wa taarifa hizo kupitia ukurasa
wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter ambapo aliongeza kuwa United
wameanza kulipa fedha za awali kwa ajili ya mshambuliaji huyo.
Man U tayari ina washambuliaji
wanne ambao ni Robin Van Persie,Wayne Rooney, Javier Hernandez
Chicharito na Danny Welbeck huku mshambuliaji mwingine Angelo Henriquez
akiwa kwenye timu ya Wigan Athletic kwa mkopo .
United imehusishwa na usajili
wa mshambuliaji wa Borrusia Dortmund raia wa Poland Robert Lewandowski
taarifa ambazo zinaendana na tetesi nyingine zinazomhusisha mshambuliaji
Wayne Rooney na usajili wa kwenda kwenye klabu ya PSG.
No comments:
Post a Comment