Wednesday, March 6, 2013

MAKAMU WA RAIS AMALIZA ZIARA YA SIKU TATU MKOANI MARAMAKAMU wa Rais Dk.Mohamed Gharib Bilal amezindua rasmi Kivuko cha MV Musoma na kutoa wito kwa Wananchi kukitunza kivuko hicho kwa kuwa kina umuhimu mkubwa katika kurahisisha huduma za kijamii kwa kukitumia katika kusafirisha mahitaji mbalimbali ya kibinadamu.

Katika ufunguzi wa kivuko hicho uliofanyika Wilayani Rorya,Dk Bilal alisema kivuko hicho ni ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alipokuwa kwenye kampeni na kusema ahadi zote zilizoahidiwa na Rais zitatekelezwa na kuutaka uongozi wa mkoa wa Mara kuzipitia ahadi zote zilizoahidiwa.

Alisema kivuko hicho kimenunuliwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 na kutokana na umuhimu wake kwa Wananchi kutambua kuwa Serikali imetumia fedha nyingi kwa ajili ya kukikamilisha hivyo kuwataka kukitunza na kukitumia kikamilifu kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii.

Alisema kwa kutumia kivuko hicho huduma za Wananchi zitaimalika katika kuunganisha Wilaya za Rorya na Musoma pamoja na mkoa mzima wa Mara na hivyo kuondoa hadha ya usafiri ambayo walikuwa wakiipata Wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu na hivyo shughuli mbambali kukwama na kuzoletesha Uchumi.

Bilal alisema Serikali imedhamilia kuhakikisha vivuko vyote Nchini vinakuwa vya uhakika na salama kwa matumizi ya Wananchi na itatimiza lengo hilo kwa kukarabati na kununua vivuko vipya kila inapohitajika ili shughuli za kiuchumi na kijamii ziweze kufanyika kwa wakati pasipo vikwazo.

Alisema katika kutekeleza hayo,Serikali ilikarabati vivuko viwili vya MV.Kigamboni mkoani Dar es salaam na MV.Sengerema mkoani Mwanza ambao katika ukarabati huo viliboleshwa na tayari vinafanya kazi katika maeneo husika na kuwanufahisha Wananchi kwa kufanya shughuli mbalimbali kwa kutumia vivuko hivyo.

Makamo wa Rais alisema katika kuelewa umuhimu wa vivuko katika maeneo yenye mahitaji,Serikali imenunua vivuko vipya vya MV.Kilombero cha tani 50,MV.Misungwi (35),MV. Ujenzi (85),MV.Kilambo tani 50 pamoja na MV.Musoma ambacho kimezinduliwa.

"Napenda niwahakikishieni kuwa kazi hii bado inasonga mbele,Serikali inaendelea na ujenzi wa vivuko vipya vya Msangamkuu (Mtwara) na Ilagala katika mto Malagarasi mkoani Kigoma na Serikali inanunua kivuko cha tani 85 kati ya Kihunda na na Maisome mkoani Geita,kivuko cha tani 35 kitakachotumika maeneo ya Itungi Port Wilayani Kyela mkoani Mbeya,"alisema Dk.Bilal.

Aidha akiwa katika siku yake ya pili ya ziara mkoani Mara,Makamo wa Rais amezindua nyumba tatu za Watumishi wa Umma zinazojengwa na Wakala wa Nyumba Tanzania (TBA) ziatagharimu kiasi cha shilingi milioni 135 ikiwa ni kati ya nyumba elfu kumi ambazo zitajengwa Nchi nzima maalum kwa Watumishi wa Umma wa kada mbalimbali.

No comments:

Post a Comment