Monday, February 4, 2013

MWANAMKE AUAWA KISHA KUCHOMWA MOTO AKITUHUMIWA KUHUSIKA NA KIFO CHA JILANI YAKE
.
“Baada ya kufa jilani yake maiti ikapelekwa kwa
mtuhumiwa,wakachoma nyumba kisha wakampiga na kumteketeza kwa moto”
-Serengeti.
Februari 4,2013.
 
MWANAMKE mmoja mkazi wa kitongoji cha Stooni kijiji cha Nyiberekera kata ya Issenye wilayani Serengeti ameuawa kisha mwili na nyumba yake kuteketezwa kwa moto na wananchi kwa tuhuma za kujihusisha na ushirikina.
Tukio hilo limetokea februari 2 ,majira ya saa 9:00  arasili  nyumbani kwake mwaka huu baada ya kufariki mkazi mmoja kijijini hapo na maiti kutelekezwa kwa mama huyo wakimtuhumu kuhusika na kifo hicho limethibitishwa na uongozi wa kata na polisi wilayani hapa.
Kwa mjibu wa habari zilizolifikia Mwananchi na kuthibitishwa na diwani wa kata hiyo Ally Nyarobi zinadai aliyeuawa na mwili wake kuteketezwa kwa moto na kundi la wananchi ni Nyabuke Mese (50).
Diwani alisema kuwa kabla ya wananchi kufanya unyama huo kulitokea kifo cha mkazi mmoja kwenye kitongoji hicho Kikene Kasinge(40)ambacho mama huyo alihusishwa na maiti kupelekwa nyumbani kwake .
“Mama huyo alihusishwa na kifo cha Kasinge kwa kile kinachodaiwa kuwa alimroga na maiti ikapelekwa kwake wakati hayupo…wakaweka maiti hapo kisha wakachoma moto nyumba yake …alipoona hali hiyo akajitokeza na katika mahojiano akajibu kuwa pamoja na kuchoma nyumba atajenga na hawamfanyi kitu … wakampiga kisha wakamchoma moto na kuteketea ”alisema diwani.
Mashuhuda wanena.
Baadhi ya mashuhuda walioongea na Mwananchi kwa kutokutajwa majina yao gazetini  walisema mapema wiki hii mama huyo alimkuta Kasinge nyumbani kwa Greta Chibagi akinywa pombe ya kienyeji aliyonunua kwa tsh,300  na kumlazimisha  wakae naye na ampe pombe.
“Kasinge alikataa kwa madai kuwa mama huyo ametengwa na jamii kutokana na vitendo vyake vya ushirikina ,watu hawaendi kwake…alimjibu kuwa kama wamenitenga ndani ya siku tatu wewe utakuja kwangu na wengine watafuata”alisema shuhuda .
Alibainisha kuwa kauli hiyo ilimfanya Kasinge atoke eneo hilo,hata hivyo mama huyo alimfuata njiani na kumtaka aende naye kwake nay eye akakataa,lakini akazidi kumwambia kwa njia yoyote lazima atakwenda na kumpa siku 3 tena.
“Januari 30 akaugua ghafla homa kali akapelekwa zzahanati kupimwa akaonekana hana ugonjwa huku hali ikizidi kuwambaya…ajabu akawa bubu …januari 31 akapelekwa kwa mganga wa kienyeji kijijini hapo ambaye ni mgeni akawaambia hana uwezo wa kutibu ugonjwa huo..februari 2,majira ya saa 6:00 mchana akakata roho”alisema shuhuda.
Matukio mengine aliyowahi kuhusishwa nayo.
Vyanzo hivyo vilisema kuwa mama huyo amewahi kukiri mbele ya mkutano wa kitongoji hicho ulioitishwa chini ya Mwenyekiti wake Makuru Siboti kuwa ameishaua watu wanane wa familia moja.
Na kuwa alifikishwa polisi Issenye kisha Mugumu lakini alichiwa kutokana na udhaifu wa sheria ya Uchawi ya mwaka 1928 ambayo hata watendaji wa serikali hawaijui na namna ya kushughulikia masuala yanayohusishwa na vitendo vya kishirikina.
Mbali na hilo pia aliwahi kubanwa kwa tukio la kumtishia Greta Sarota mkazi wa kijijini hapo kuwa mwanae aliyekuwa kidato cha pili Nagusi Sekondari kuwa ana akili atamkomesha.
“Haikuchukua muda mtoto huyo akapotea katika mazingira ya kutatanisha na alipobanwa huyo mama mtoto akarudi lakini akiwa hataki shule mpaka sasa”mwananchi iliambiwa.
Alihusika mgogoro wa kugombea Fisi wa uchawi.
“Mwishoni mwa mwaka jana na Mwanzoni mwa mwaka huu huyo mama alihusika katika mgogoro wa kugombea fisi uliomhusisha Mirengali Kitoshi na kijana mmoja wa kijaluo”alisema mkazi wa kitongoji hicho jina limehifadhiwa.
Katika mgogoro huo Mirengali alimfikisha ofisi ya serikali ya kijiji kijana huyo akidai ni jambazi na ndipo akatoboa siri kuwa ugomvi wao unahusu fisi wa uchawi aliyepewa kwenda naye kijijini kwao Rorya na kufika huko akaokoka na fisi akawa amekufa kufuatia chumba alimokuwa amemweka walipuliza dawa ya ukoka.
Kijana huyo ambaye alikuwa kijijini hapo kwa shughuli za kibarua cha kuchunga mifugo alimtaja mama aliyechomwa moto kuwa ndio walikuwa washirika,ambao walimtaka amtoe mama yake kafara baada ya kupoteza fisi wao wa kazi,hata hivyo alifukuzwa kijijini hapo.
Maiti iliyotelekezwa yachukuliwa na polisi.
Polisi wilayani hapa walilazimika kuchukua maiti ya Kasinge ambayo ilitelekezwa nyumbani kwa mama huyo aliyechomwa na imehifadhiwa chumba cha Maiti hospitali teule ya Nyerere ddh .
Hospitali wathibitisha kupokea maiti ya Kasinge
Mganga mkuu wa hospitali teule ya Nyerere ddh Dk,Kelvin Mwasha amekiri kupokea mwili wa Kasinge ambao ulipelekwa na polisi,ingawa hawajaambiwa nini kinatakiwa kwa kuwa hata polisi hadi tunakwenda mitamboni walikuwa hawajafika hospitali kueleza kinachotakiwa kufanyika.
Ndugu na familia walazimika kuzika mama aliyechomwa.
Katika hali inayoonyesha wananchi kuchukizwa na matendo ya mama huyo hata kwenye mazishi yake hawakuhudhuria bali  ndugu na wanae ndio waliohusika.
Hakuna mtu anayeshikiliwa kuhisiana na tukio hilo na polisi wanadai wanaendelea na uchunguzi huku ndugu wa marehemu Kasinge wakisubiriwa ili kuchukua mwili wa ndugu yao walioutelekeza nyumbani kwa Nyaboke ambaye aliuawa.

No comments:

Post a Comment