Na. Christina Mponji-Jeshi la Polisi, Dodoma.
………………………………………………………
Wito umetolewa kwa Majimbo,
Tarafa na Kata zote nchini kuimarisha dhana ya Polisi jamii na ulinzi
shirikishi katika maeneo yao, ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu
kuanzia ngazi ya familia ambako ndiko hasa chimbiko la uhalifu.
Hayo yamesemwa jana na Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini IJP Said Mwema, wakati akitoa tunuku ya hati ya
utendaji bora kwa Kata/Shehia, Tarafa, na Jimbo zilizofanya vizuri
katika mapambano dhidi ya uhalifu nchini kwa mwaka 2012.
Tuzo hizo zimetolewa katika
Mkutano Mkuu wa Maofisa wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi unaoendelea
mjini Dodoma katika ukumbi wa Pius Msekwa, ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa mpango wa maboresho ndani ya jeshi hilo.
Kata zilizofanya vizuri ni
pamoja na kata ya Bukwe Mkoa wa kipolisi Tarime Rorya, Kizwite ya
mkoani Rukwa, Isansa ya mkoani Mbeya, pamoja na shehia ya Ng’omeni
kutoka mkoa wa Kaskazini Pemba.
Tarafa zilizofanya vizuri ni
tarafa ya Girango ya mkoa wa kipolisi Tarime Rorya, Lwiche ya mkoani
Rukwa, Igamba ya mkoani Mbeya pamoja na Jimbo la Mji Mkongwe la Mkoa wa
Mjini Magharibi visiwani Zanzibar ambapo tuzo hizo zimepokelewa na
makamanda wa mikoa hiyo kwa niaba ya kata/shehia na tarafa/majimbo yao.
IJP Mwema amesema, endapo kata
na tarafa zote nchini zitaimarisha dhana ya ulinzi shirikishi na polisi
jamii, ni wazi kuwa matukio ya uhalifu yatapungua kwa kiasi kikubwa na
hatimaye kuwa historia.
Akiongea katika hafla hiyo Mkuu
wa Huduma za Polisi Jamii, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Lazaro Mambosasa
alisema kuwa kata na tarafa zilizofanya vizuri, zilikuwa na kiwango
kikubwa cha matukio ya kihalifu lakini kupitia dhana ya ulinzi
shirikishi na polisi jamii wamefanikiwa kudhibiti vitendo hivyo huku
akitolea mfano kata ya Bukwe ambako kulikuwa na migogoro ya kikabila, na
hivi sasa migogoro hiyo imekoma kabisa.
Akiongea kwa niaba ya wenzake,
kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kamishna Msaidizi Diwani Athumani,
amesema jamii sasa imeanza kuelewa umuhimu wa kushirikiana na jeshi la
polisi katika mapambano dhidi ya uhalifu na kwamba wamekuwa mstari wa
mbele katika kuhamasishana juu ya uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi
shirikishi.
Jeshi la polisi limekuwa
likifanya jitihada mbalimbali za kuimarisha hali ya ulinzi na usalama
kuanzia ngazi ya kata/shehia, ambapo hivi karibuni wametoa pikipiki kwa
wakaguzi tarafa ili kuwarahisishia utendaji katika tarafa zao.
No comments:
Post a Comment