Wednesday, November 7, 2012

VIONGOZI WA UAMSHO WAPEWA DHAMANA YENYE MASHARTI MAGUMU

.Warudishwa tena Rumande
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar
ZANZIBAR JUMATANO NOVEMBA 7, 2012. Mahakama ya Wilaya ya MwanakwerekwE ya mjini Zanzibar, leo imetoa fursa ya dhamana kwa Viongozi wa makundi mawili ya kidini Zanzibar wanaotuhumiwa kwa makosa ya kufanya fujo na kupelekea ghasia na vitendo vya uvunjifu wa amani na uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Watuhumiwa hao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar Sheikhe, Faridi Hadi Ahmedi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uamsho Sheikhe, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman, Azan Khalid Hamdan, Khamis Ali Suleiman na Hassan Bakar Suleiman.
 
Akisoma uwamuzi huo huku kukiwa na ulinzi mkali eneo lote la Mahakama, Hakimu wa Makahama hiyo Mh. Msaraka Pinja, amesema kuwa ingawa upande wa Mashtaka ulikuwa haukutoa pingamizi ya dhamana kwa watuhumiwa, lakini Mahakama ililazimika kusitisha utoaji dhamana baada ya kupitia mambo kadhaa ya msingi.
Amesema kuwa pamoja na uzito wa tuhuma zinazowakabili watuhumiwa, Mahakama ililazimika kusita kutoa dhamana kwanza kwa usalama wa watuhumiwa wenyewe na kwa kuangalia mazingira yaliyokuwepo wakati huo na uwezekano wa kuingilia upelelezi wa kesi inayowakabili.
Hakimu huyo alisema wasiwasi wa Mahakama ilikuwa kwamba watuhumiwa hao wakiwa nje ya dhamana kuna uwezekano wa kutenda kosa lingine, Kutohudhuria Mahakamani kwa wakati wanapotakiwa na kuangalia kwa mapata uzito wa kosa wanaloshitakiwa nalo.
Baada ya kuridhika na Mahakama hiyo ilitoa dhamana kwa watuhumiwa wote saba kwa mashariti ya kuwasilisha mahakamani fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni tatu kwa kila mmoja pamoja na kuwa wadhamini watatu ambao ni watumishi wa Serikali kwa kila mmoja akitoa kiasi kama hicho cha fedha mahakamani.
Watuhumiwa hao pamoja na Wadhamini wao, kwa pamoja wametakiwa kuwasilisha barua kutoka kwa Sheha wa Shehiya anayoishi pamoja na kivuli cha vitambulisho vya Zanzibar Mkazi na kwa wale wenye Hati za Kusafiria pia wawasilishe vivuli vya hati hizo Mahakamani.
Pamoja na masharti hayo ya jumla, lakini pia wadhamini wometakiwa wawe watumishi wa serikali na wawakilishe barua kutoka katika ofisi wanazozifanyia kazi na vivuli vya vitambulisho vyao vya kazi ili view kama kumbukumbu mahakamani.
Hata hivyo watuhumiwa wote wamerejeshwa rumande baada ya kushindwa kutekeleza masharti ya dhamana pamoja na kukabiliwa na kesi nyingine Mahakama Kuu ya Vuga, kesi ambayo dhamana yake imewekewa pingamizi kwa hati maalum ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar kwa sababu za kiusalama.
Kesi hiyo imeahirishwa tena hadi Novemba 21, mwaka huu itakapotajwa tena.
Akizungumza mara baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo mmoja ya Mawakili wa Watuhumiwa hao Bw. Abdallah Juma, amesema yeye pamoja na wakili mwenzake Bw. Salum Toufik, wataendelea kuwatetea watuhumiwa hao hata baada ya kutishia kujitoa katika kesi hiyo mwezi uliopita.

No comments:

Post a Comment