Friday, November 16, 2012

TUME YA MABADILIKO YA KATIBA YAINGIA MKOANI MARA.

 Shomary Binda wa gazeti la Mtanzania,Emanuel Amas wa TBC na Lazaro Kaaji wa Tanzania Daima wakiwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa
 Waandishi wa habari wakiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kupata taarifa ya kuwasili kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
 Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw John Tuppa akisoma taarifa kwa Waandishi wa Habari ofisini kwake
               Mchakato unaendelea


TUME  ya Mabadiliko ya Katiba inaanza kukusanya maoni ya kuundwa kwa Katiba mpya Mkoani Mara Novemba 19  ikianzia wilayani Tarime katika kata ya Bumera na Tarime Mjini.

Akiongea na Waandishi wa Habari ofisini kwake Leo Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw John Gabriel Tuppa alisema kuwa kufika kwa tume hiyo mkoani Mara ni fursa nzuri kwa wananchi wa mkoa wa Mara kutoa Maoni yao.

Alisema vyema wananchi wakahudhuria kwa wingi katika Maeneo itayokuwepo Tume hiyo na kutoa Maoni ili kuondoa dhana ya kutoshirikishwa katika kuundwa kwa Katiba Mpya.

“Hii ni nafasi nzuri kwa wakazi wa Mkoa wa Mara kutoa Maoni yao ili baadaye wasije wakasema hawajahusishwa katika kuundwa kwa Katiba Mpya” alisema mkuu huyo wa Mkoa.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwaomba wananchi wa mkoa wa Mara kushirikiana vyema na Tume hiyo ili ifanye kazi zake kwa Amani na kuondoa dhana ya kwamba Mkoa wa Mara una watu Wakorofi.

Alisema tayari ameishawasiliana na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani hapa ili kuhakikisha wananchi wanatoa Maoni yao kwa Amani na kuongeza kuwa wananchi wanapaswa kuvumiliana katika utoaji Maoni kwani kila Mtu hutoa kile anachoona kinafaa.

“Mimi naomba Wananchi wa Mkoa wa Mara wawe watulivu na Wavumiliane katika kutoa Maoni maana kila mmoja ana mtazamo wake katika kutoa Maoni” alisema Bw John Tuppa

Tume hiyo ya Mabadiliko ya Katiba ina jumla ya watu 14 ambapo inatazamiwa kumaliza kazi ya ukusanyaji Maoni  Desemba 19 katika kata ya  Kibara wilayani Bunda.

Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa wa Mara alisema kuwa kumekuwepo na watu kutoelewana katika eneo la Ng’ereng’ere wilaya ya Tarime na kupelekea mtu mmoja kufariki dunia.

Aidha mkuu huyo wa Mkoa wa Mara amekanusha kuwepo kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwani tukio hilo limetokana na watu kutofautiana.

“Nimesikia taarifa eti Mapigano ya Koo Tarime yarejea jamani hii si kweli ile ni hali ya kawaida kabisa na inaweza kutokea sehemu yoyote nchi mtu na mtu kutofautiana” alisema Mkuu wa Mkoa Tuppa

Aliongeza kuwa kwasasa Mkoa wa Mara kumekuwepo na Amani tofauti na kipindi kingine chochote na hivyo kuondoa hofu inayojaribu kujengwa na baadhi ya watu

No comments:

Post a Comment