Thursday, November 22, 2012

Tamasha la Jinsia Ngazi ya Wilaya Mkambarani-Morogoro Lafana


 Baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali wakifuatilia mada anuai katika tamasha hilo.
 Baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali wakifuatilia mada anuai katika tamasha hilo.


Na Mwandishi wa Thehabari.com, Mkambarani-Morogoro

TAMASHA la Jinsia Ngazi ya Wilaya linalofanyika Kijiji cha Mkambarani-Morogoro limeanza rasmi kwa kufunguliwa kwa mjadala wa wazi uliotoa nafasi kwa washiriki kushirikishana maswala anuai ya kijamii.

Mada Kuu ya tamasha hilo inasema; 'Haki ya Uchumi, Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake Walioko Pembezoni. Tamasha hilo linaendelea kwa siku tatu mfululizo nje kidogo ya Mji wa Morogoro, eneo la Moseka-Mkambarani, ambapo wananchi mbalimbali pamoja na wanaharakati ngazi ya jamii wanahudhuria kuchangia mada mbalimbali zinazotolewa eneo hilo.


Masuala yaliyoibuka kwa mkutano wa jana ni pamoja na migogoro ya ardhi kati ya wananchi na wanakijiji wa eneo la Mkambarani dhidi ya wawekezaji wanaoingia kutaka kuwekeza hasa kwenye mashamba.


Baadhi ya wananchi wameomba viongozi wa juu kuingilia mgogoro wa ardhi uliopo kati ya wananchi na taasisi ya Islamic Foundation, ambapo inadaiwa wananchi kuyaachia mashamba yao waliyokuwa wakilima awali ili yachukuliwe na taasisi hiyo.

Wananchi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti wameomba zifuatwe taratibu kama kuna wawekezaji wanataka kuingia kwenye ardhi ya wanakijiji ili mazungumzo yafanywe na Serikali ya kijiji na si vinginevyo.


Mkutano huo unaendelea tena leo na unatarajia kufikia kikomo Ijumaa ya wiki hii.
*Chanzo: www.thehabari.com

No comments:

Post a Comment