Geita
KATIKA hali ya kustaajabisha,baadhi ya
wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Ntono iliyopo katika kijiji cha
Ntono Kata ya Kamena Wilayani Geita mwishoni mwa wiki iliyopita waliandamana
hadi kwa viongozi wa chama cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA) ili kufikisha
kilio chao cha kutofundishwa kutokana na baadhi ya walimu wa shule hiyo
kukimbilia machimboni.
Tukio hilo ambalo liliacha maswali mengi
miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho lilitokea majira ya saa 4 asubuhi muda
mfupi baada ya msafara wa viongozi hao wa chadema wakiongozwa na aliyekuwa
diwani wa kata ya Sombetini jijini Arusha kabla ya kutimkia chadema, Alfonce
Mawazo kuwasili kwenye uwanja wa soko la kijiji hicho kwa ajili ya kufanya
mkutano wa hadhara wa oporesheni sangara kupitia kauli mbiu yao ya M4C.
Hata hivyo wakati msafara huo ukiwasili
kijijini hapo baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo walionekana kuzagaa kila kona na
wengine wakicheza mpira ambapo ghafla waliandamana hadi lilipokuwa limesimama gari
la viongozi hao wa chadema kisha kulizunguka na kitendo bila kuchelewa walianza
kutoa kilio chao kwa viongozi hao wa chadema wakitaka kilio hicho kifikishwe
kwa Rais Kikwete.
“Shikamoo..Mmekuja kufanya mkutano
hapa…kamwambieni Rais Kikwete hatufundishwi…tunakuja kufanya kazi za walimu na
kucheza tukisubili wakati wa kutawanyika na kurudi nyumbani kwetu…walimu wetu
wameishia machimboni huko nyangarata”alisikika mmoja wa wanafunzi hao Getruda
Shija anayesoma darasa la sita kwenye shule hiyo akilalama huku wenzake
wakimshangilia.
Wananafunzi hao,walidai kuwa kwa muda mrefu
sasa baadhi ya walimu wa shule hiyo wametimkia machimboni tangu ulipotokea
mulipuko wa dhahabu(Gold Rush) katika kijiji cha Nyangarata kilichopo kata ya
Butobela Wilayani Geita hali ambayo walidai inawanyima haki yao ya msingi ya
kupata elimu bora.
Petro Faida na Emanuel Yohana wanaosoma
darasa la tatu katika shule hiyo waliwaeleza viongozi hao wa chadema kuwa,kutokana
na walimu wao kutimkia kwenye machimbo hayo kwa ajili ya kuchimba mawe yanayozaniwa
kuwa na dhahabu,kwa sasa wamekuwa vibarua wa kufanya kazi majumbani mwa walimu.
“Hapa mnavyotuona tumetoka kufanya shughuli
kwa walimu wetu…na tunapumzika kidogo tu tena tunaenda kulima mashamba ya
walimu…kamwambieni Rahisi Kikwete tunateseka…hatufundishwi kabisa”alisema
Yohana kwa rafudhi ya kisukuma huku akishangiliwa.
Kufuatia hali hiyo,mmoja wa viongozi hao wa
Chadema James John na mwandishi wa habari hizi pamoja na baadhi ya wanafunzi
hao waliongozana hadi ilipo shule hiyo kwa lengo la kuonana na mkuu wa shule
hiyo ili kuthibitisha madai ya wanafunzi hao,ambapo walishangaa kukuta
wanafunzi wakiwa wanacheza nje ya madarasa na wengine wamelala vichakani huku
mwalimu mmoja akiwa amekaa ofisini.
Mwalimu huyo aligoma kutaja majina yake na
hata kuzungumzia madai ya wanafunzi hao kwa madai kuwa si msemaji na badala
yake alitoa namba za mkuu wake na kumtaka mwandishi awasiliane naye aliyedai
yuko jirani.
Aidha Mkuu wa Shule hiyo John Katabazi mara
baada ya kupigiwa simu kisha kukutana na mwandishi wa habari hizi alikiri
walimu wake kwenda kwenye machimbo hayo huku akiwatetea kuwa hawafanyi hivyo
mara kwa mara.
“Ni kweli hili tatizo lipo…walimu wangu
wamekuwa wanakwenda kunusa…wanarudi… kwenye machimbo hayo baada ya kutokea
mulipuko wa dhahabu(Gold Rush)..lakini siyo mara kwa mara”alisema Katabazi.
Mbali na hilo,Katabazi alizitaja changamoto
nyingine zinazoikabili shule hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa walimu,madawati
pamoja na vyumba vya madarasa.
Alifafanua kuwa shule hiyo yenye jumla ya
wanafunzi 1192,ikiwa na mikondo 31 inao walimu 12 badala ya 29,na kwamba inayo madawati
188 pekee pamoja na vyumba vya madarasa 7 badala ya 31 jambo alilodai nalo ni
kikwazo cha wanafunzi kupata elimu inayowastahili.
Kwa upande wake Mawazo akiwahutubia mamia
ya wakazi wa kijiji hicho ambacho ni ngome ya chama cha mapinduzi(CCM)mbali na
kuahidi kufikisha kilio cha wanafunzi hao ngazi husika,aliwataka wananchi hao
kubadilika kwa kuikataa CCM kwa madai kuwa kuendelea kuchagua
pombe,furana,kanga,chumvi na kofia wanazopatiwa na chama hicho hususani wakati
wa uchaguzi ndiyo sababu zilizopelekea kijiji chao kukosa huduma muhimu za
kijamii.
“Ndugu zangu wana Ntono…maeneo yote
waliyochagua Chadema na kuikataa CCM kuna huduma zote za kijamii..ninyi hapa
hamna maji..huduma za afya wala miundombinu ya barabara na bado mnachagua CCM
hii ni laana… mnakubali kuchagua pombe…furana za kijani…kanga..chumvi na
kofia…hivi hamjui wamewafanya kama kuku wa kienyeji…ikataeni CCM mchague
mabadiliko”alisema Mawazo.
No comments:
Post a Comment