Wednesday, October 3, 2012

ASKARI POLISI ATAKAYEFUKUZWA KAZI AMA KUACHISHWA KULIPWA STAHILI ZAKE

Na Mohammed Mhina wa Jeshi la Polisi- zanzibar
ZANZIBAR JUMATANO OKTOBA 3, 2012. Imeelezwa kuwa, kuanzia sasa Askari Polisi yeyote atakayefukuzwa kazi ama kuachishwa kutokana na makosa ya kiutendaji atalipwa stahili zake zote tofauti na zamani ambapo askari aliyekuwa akifukuzwa alikuwa akitoka mikono mitupu.
Ufafanuzi huo umetolewa na Mkuu wa Utawala na Rasilimali watu wa Jeshi la Polisi Kanda ya Zanzibar Kamishna Msaidizi Mwandamizi Kenneth Kasseke, wakati akizungumza kwenye mkutano wa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Perera Juma Silima anayeitembelea Zanzibar.
Kamanda Kasseke ametoa ufafanuzi huo alipotakiwa kujibu hoja mbalimbali zilizoulizwa na askari wakati wa mkutano wa Mh. Silima uliowashirikisha Askari na Maafisa wanadhimu wakiwemo Makamanda wa Polisi wa Mkoa mitatu ya Zanzibar.
Kamanda Kasseke amesema Jeshi la Polisi limefikia hatua hiyo baada ya kuona kumekuwapo na malalamiko ya msingi kutoka kwa baadhi ya askari kuwa wamekuwa wakifukuzwa kazi bila ya kulipwa haki zao hata baada ya kukatwa fedha kuchangia kwenye mifuko mbalimbali ya hifadhi za jamii.
Kutokana na hali hiyo Kamanda Kasseke amesema imeonekana kuwa sio busara wala haki kwa askari huyo kunyimwa fedha hizo ambazo zinatokana na makato kwenye sehemu ya mishahara yao ambayo kama isingekatwa angekuwa amepewa ama kujiwekea mwenyewe akiba benki.
“Fedha hizo ni sawa na mtumishi aliyejiwekea akiba na kwamba zingeweza kumsaidia wakati wowote akiwa kazini ama hata baada ya kumaliza muda wake wa utumishi Jeshini”. Alisema Kamanda Kasseke huku akishangiliwa na Askari waliohudhuria katika mkutano huo.
Kamanda Kasseke alitakiwa na Mh. Silima kujibu hoja mbalimbali zilizoulizwa na askari ikiwemo la kutokulipwa fedha zao baada ya kufukuzwa kazi na hata kufikishwa mahakamani kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo ya bahati mbaya hata baada ya kulitumikia Taifa kwa muda mrefu.
Na kwa upande wake Waziri Silima akizungumza kwenye mkutano huo, amesema kuwa pamoja na juhudi zinazochukuliwa na serikali za kuboresha makazi ya askari ikiwa ni pamoja na  nyumba mpya za Askari katika maeneo mbalimbali hapa nchini, lakini bado hali ya majengo mengi wanayoishi askari Polisi makambini yana hali mbaya.
Amesema amelazimika kufanya ziara ili kujionea mwenyewe hali hiyo badala ya kusikia kutoka kwa baadhi ya Maafisa na askari.
Katika mkutano huo ambao uliendeshwa kwa kuanza kupokea hoja, maoni, kero na maswali mbalimbali kutoka kwa Askari Polisi wa Vikosi mbalimbali, Waziri Silima pia alifurahishwa na hoja za msingi zilizotolewa na askari hao na kusema kuwa zikipatiwa ufumbuzi malalamiko kama hayo yatapungua.
Lakini pia Waziri Silima alipongeza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi hapa nchini akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali saidi Mwema katika kutekeleza baadhi ya mambo wenye lengo la kuboresha ustawi wa kila askari Polisi.
Pamoja na kukemea vitendo vya kudai na kupokea rushwa vinavyofanywa na baadhi ya askari wakiwemo wa Kikosi cha Usalama barabarani, lakini Waziri Silima pia amewahakikishia askari Polisi kote nchini kuwa Serikali itafanya kila liwezekanalo ili kuona kila askari Polisi ananufaika na kazi anayoifanya.
Ametoa wito pia kwa wananchi kuendelea kushiirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za siri zitakazowezesha kukamatwa kwa wahalifu mbalimbali na kuwafanya waishi kwa usalama na amani.
Amesema Serikali haifurahii kuona kila kukicha kuna mwananchi aliyefanyiwa vitendo vya kihalifu kama vile mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha ama kusambaziwa dawa za kulevya na watu wanaofahamika na bila ya kuchukuliwa hatua.
“Tunaendelea kuwaomba sana wananchi washirikiane na sisi kwa kutupatia taarifa ili tuzishughulikie”. Ndivyo alivyomaliza Waziri Silima.
Mwisho

No comments:

Post a Comment