Saturday, September 15, 2012

MBUNGE WA MWIBARA AITAKA HALMASHAURI YA BUNDA KUSIMAMIA FEDHA ZA SERIKALI

BUNGE wa jimbo la Mwibara wilayani Bunda mkoani Mara Bw. Kangi Lugola ameigeukia halmashauri ya wilaya hiyo kwa kuitaka isimamie vizuri fedha za serikali na kurejesha haraka zaidi  ya sh.121milioni zikiwa ni fedha za ruzuku ya maendeleo (LCGD) zilizotumika katika miradi ambayo haikupangiwa.

Fedha hizo zilihamishwa kama mkopo kutoka mfuko wa LCGD zilizoidhinishwa kwa wakati tofauti  na kamati ya fedha, uongozi na mipango ya halmashauri tangu mwaka 2004/2005 na kuzipeleka kukamilisha miradi ambayo haikupangiwa kwa kusudi za kuzirudisha jambo ambalo halijafanyika.

miradi inayodaiwa kutekelezwa kwa fedha hizo pia zimekuwa zikilalamikiwa kufanyika chini ya kiwango huku taarifa ya ukaguzi wa ofisi ya mkaguzi mkuu wa serikaliCAG) hivi karibuni zikidai matumizi mabaya ya fedha.

Alisema kitendo cha kutorudisha fedha hizo na matumizi mengine mabaya yaliyofanyika imechangia baadhi ya miradi lengwa kuathirika na kutaka fedha hizo zirejeshwe kukamilisha miradi iliyokwama.

Pia alisikitishwa na baadhi ya vocha na vilelezo vilivyoidhinisha malipo ya wakandarasi waliohusika katika ujenzi wa miradi hiyo kukosa saini ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo jambo lililodhihirisha kuwa  kuwepo mwanya wa ufisadi.

“Kule bungeni tunaambiwa na serikali kuwa fedha nyingi zinatumika vibaya katika halmashauri huku,ukija huku wananchi wanalalamika kuwa wapo baadhi ya watendaji ambao siku chache tu baada ya kuanza kazi wanaanza kumiliki magari ya fahari, kumbe sisi madiwani ndio tunabariki mianya hiyo” alisema Bw. Lugola.

Katika kikao hicho maalum jana iliyoitishwa kwa lengo la kujadili taarifa ya fedha za ruzuku za program ya maendeleo ya serikali za mitaa(LCGD) baada ya madiwani kuhisi matumizi mabaya ya fedha hizo kwa mwaka wa fedha 2004/2005 Ofisa mipango wa halmashauri ya wilaya ya Bunda Bw. Donatus Wegina alieleza kuwa fedha hizo zilikopwa na halmashauri yenyewe kwa kuhamishia miradi mingine.

Bw. Wegina alijitetea kuwa Kamati ya fedha , uongozi na mipango iliidhinisha matumizi ya fedha hizo kwenda katika miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa upasuaji , wodi ya wanawake na watoto katika kituo cha afya cha Manyamanyama, ukarabati wa jengo la utawala wa makao makuu ya halmashauri hiyo, ujenzi wa uzio wa mnada wa Mugeta .

Miradi iliyolengwa na fedha hizo za LCGD zilizoathirika hadi sasa ni pamoja na ukamilishaji wa mfumo wa umwagiliaji  katika Kijiji cha Kasuguti sh.37miln, ukarabati wa nyumba ya mkurugenzi sh. 21miln.

Alitaja miradi mingine iliyokwama ni pamoja na uchimbaji wa visima viwili sh.40miln, chumba cha darasa kwa watoto wenye ulemavu shule ya msingi Kabalimu sh.20milion,ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji Nyatwari sh.18miln na sh.9milion kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Tamao.

Hata hivyo Bw. Wegina aliwataka madiwani hao kutokubali kukopa fedha kutoka mfuko wa LCGD kufanyia miradi mingine na kutorudisha fedha hizo.

Hata hivyo Bw.Kangi na baadhi ya madiwani ambao hawakushiriki kikao cha kuidhinisha matumizi hayo walipigwa butwaa baada ya kubaini kuwa baadhi ya vilelezo zikiwemo vocha za malipo za wakandarasi waliohusika hazikuwa na saini ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo jambo iliyowatia wasiwasi wajumbe kuwa uko mwanya wa matumizi mabaya ya fedha .

Baraza hilo lilimtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Cyprian Oyier na mhandisi wa ujenzi Bw. Mwita Muhochi  kutoa ufafanuzi juu ya hoja hiyo  ambapo hata hivyo maelezo yao hayakupokelewa na wajumbe hao.

Alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bunda  Bw. Joseph Malimbe alikiri kuwa fedha hizo kutoka mfuko wa LCGD zilikopwa kwenda kwenye miradi mingine na kwamba sheria inaruhusu kufanya hivyo.

Bw. Marimbe alisema tatizo ni kutorejesha fedha hizo kwa wakati  na kwamba  halmashauri yake iko kwenye mchakato wa kutumia makusanyo ya ndani kurejesha fedha hizo.

No comments:

Post a Comment