Sunday, July 8, 2012

    VIONGOZI KUMI AFRIKA AMBAO NI VING'ANG'ANIZI MADARAKANI

 Teodoro Obiang

Teodoro Obiang ndiye anayeshikilia madaraka kwa muda mrefu zaidi. Kiongozi huyo mwenye miaka 69 aliipindua serikali ya nchi yake ya Guinea ya Ikweta mwaka 1979. Miaka 10 baadaye alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo katika uchaguzi wa kwanza huru. Obiang alichaguliwa tena katika chaguzi za mwaka 1996, 2002 na 2009. Kipindi chake cha urais kitakwisha mwaka 2016.
 Paul Biya

Kiongozi huyu mwenye umri wa miaka 79 amekuwa akiiongoza nchi ya Cameroon iliyoko Afrika ya Magharibi kwa karibu miaka 30 sasa. Licha ya kuwapo kwa tuhuma ubatilishaji wa kura, alichaguliwa tena katika chaguzi za urais za mwaka 1997 na 2004. Biya aliibadili katiba ya nchi yake mwaka 2007 ili kupata kutawala tena. Mwaka 2011 alichaguliwa tena ingawa upinzani ulimshutumu kwamba alibatilisha kura.
 José Eduardo Dos Santos

Yeye ana umri wa miaka 69 na amekuwa akiitawala Angola tangu mwaka 1979 bila ya kuchaguliwa na wananchi. Kulingana na katiba mpya ya Angola iliyotungwa mwaka 2010, rais hapaswi tena kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi. Mwenyekiti wa chama kinachopata kura nyingi katika uchaguzi ndiye anayekuwa rais. Hivyo Dos Santos ataweza kuendelea kubaki madarakani kihalali kwa miaka mingi zaidi. 

 Mswati III

Anatambulika kama mtawala pekee wa Afrika: Mswati III. Alikirithi kiti cha kifalme kutoka kwa baba yake Sobhuza II. mnamo mwaka 1986. Tangu wakati huo amekuwa akitawala nchi yake kwa kutoa amri huku akikataa aina yoyote ya demokrasia. Swaziland ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani. Takriban asili mia 26 ya raia wake wameathirika na ugonjwa wa Ukimwi.
 Yoweri Museveni 

Yeye aliingia madarakani mwaka 1986 kwa kutumia nguvu baada ya kuuangusha utawala wa kidikteta Uganda na baada ya hapo kuanzisha utawala mwingine wa aina hiyo hiyo. Kwa sababu ya kubadilishwa mara kwa mara kwa katiba ya Uganda, Museveni sasa amekuwa akiitawala nchi hiyo kwa miaka 26. Museveni amefuta mpaka wa muhula wa rais na hivyo aliweza kuchaguliwa tena mwaka 2011.
 Robert Mugabe

Watu wengi walikuwa na matumaini makubwa na Mugabe pale alipochaguliwa kuwa waziri mkuu mwaka 1980 na miaka saba baadaye kuchaguliwa kuwa rais. Lakini alianzisha utawala wa kidikteta na kuitumbukiza nchi yake katika mzozo wa chakula na wa kifedha. Tangu mwaka 2008, imebidi Mugambe aiongoze nchi pamoja na mpinzani wake Morgan Tsvangirai. Hadi leo Zimbabwe inasubiri mabadiliko yaliyoahidiwa.

 Blaise Compaoré

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 61 amekuwa akiingoza nchi ya Burkina Faso kwa robo karne sasa. Alichaguliwa kuwa rais mwaka 1987 licha ya upinzani kususia uchaguzi. Mabadiliko ya katiba ya nchi yake yalimwezesha kuchaguliwa tena kuwa rais mwaka 2005. Muhula wake wa mwisho utaanza mwaka 2010. Hata hivyo wahakiki wanahofia kwamba Compaoré atagombania tena urais ifikapo mwaka 2014
 Idriss Déby

Awali, Idriss Déby Itno aliyezaliwa mwaka 1952, alikuwa mfuasi wa kundi la waasi. Mwaka 1990, Déby alimwangusha kutoka madarakani Hissène Habré na kuteuliwa kuwa rais wa Chad mwaka 1991. Mwaka 2004, Déby aliibadilisha katiba ya Chad ili kubakia madarakani. Waasi walijaribu kumwondoa madarakani mwaka 2006 na 2008 lakini bila mafanikio. Mwaka 2011 alichaguliwa kuitawala nchi yake kwa muhula wa nne.
 
 Denis Sassou Nguesso

Nguesso aliingia madarakani mwaka 1979 lakini alishindwa katika uchaguzi huru wa kwanza kufanyika Congo Brazaville mwaka 1992. Miaka mitano baadaye alitoka uhamishoni na kujitwalia madaraka kwa nguvu. Katiba ya mwaka 2002 inaeleza kwamba mgombea wa urais haruhusiwi kuwa na umri unaozidi miaka 70. Hivyo Nguesso, mwenye umri wa miaka 69, hataweza kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2016.

Abdoulaye Wade

Abdoulaye Wade amelazimika kuachia madaraka. Katika duru ya pili ya uchaguzi iliyofanyika Senagal tarehe 25.03.2012, mpinzani wake Macky Sall alipata kura nyingi zaidi. Hata hivyo Wade, aliyetarajia kuiongoza nchi yake kwa muhula mwingine, amekubali kushindwa na amempongeza Sall kwa ushindi wake.

No comments:

Post a Comment