Monday, July 2, 2012


MKANDARASI ADAIWA KUCHELEWESHA MRADI WA MAJI WA SHILINGI BILIONI 30 BUNDA

Bunda

BAADHI ya wakazi wa mji wa Bunda na Vijiji vitatu katika halmashauri ya wilaya hiyo mkoani Mara wameiomba serikali kusitisha mkataba na kampuni ya ujenzi ya Nyakirang’ani Construction Ltd iliyopewa kazi ya kuchimba mtaro wa kutoa maji katika ziwa Vctoria kupitia  vijiji hivyo hadi mjini Bunda.

Mradi huo mkubwa wa Maji unaotekelezwa na benki ya dunia kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania unakusudia kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 30 huku kampuni hiyo ikipewa kazi ya kuchimba mtaro na kuweka mabomba kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 6.7.

                      Mji wa Bunda

Wakizungumza na waandishi wa habari,baadhi ya wakazi hao wa vijiji hivyo vya Guta,Tairo na Nyantare pamoja na Mamlaka ya mji mdogo wa Bunda walisema kasi ndogo ya uchimbaji mtaro huo inachangia kutokamilika kwa wakati kwa mardi huo unaotegemewa na wakazi zaidi ya laki moja katika maeneo hayo

 “Wakati mheshimiwa Wassira amekuja kukagua zoezi la uchimbaji wa Mtaro mkandarasi alionekana kwenda kasi lakini alipoondoka tu alihamisha vifaa mradi huu hauwezi kukamilika kwa wakati” alisema Bi Nyanjura Magafu mkazi wa kijiji cha Tairo

Mmoja wa Afisa katika idara ya Maji mjini Bunda ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake alisema wakati Stephen Wassira ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Bunda akikagua mradi huo,Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya Ujenzi Mahuza Mmangi alimweleza  Mtaro huo ungekamilika ndani ya wiki nne na kuweka mabomba lakini hadi sasa hakuna dalili za kukamilika kwa Mtaro huo.

“ Ndugu yangu sisi wengine hapa ni wadogo hatuwezi kulizungumzia hili suala kwa undani, nadhani huyu jamaa ana watu wanamlinda huko juu ndiyo maana anachelewesha kazi hii au la sivyo huu umekuwa mtaji wa CCM kwa kuombea kura kwa kila uchaguzi” alisema Afisa huyo

Alipoulizwa kuhusu kusuasua kwa mradi huo ambao ni tegemeo kubwa kwa wananchi wa mji wa Bunda na Vitongoji vyake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bunda Cyprian Oyier alikiri mradi huo kutekelezwa kwa kasi ndogo huku akisema huenda Mkandarasi ameelemewa na kazi katika Maeneo mengine

 “ Hata mimi nashangaa kasi ndogo ya utekelezaji wa Mradi huu kwani sasa hata mitambo imeondolewa eneo la Mradi sijui huyu bwana amezidiwa na kazi sehemu nyingine?” alisema Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Bunda

Alipotafutwa kuzungumzia malalamiko hayo Mkurugenzi wa Kampuni ya Nyakirang’ani Bw Mmangi kupitia simu yake ya mkononi kwa siku tatu mfululizo simu hiyo iliita bila Majibu hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi ili aweze kufafanua kuhusu malalamiko hayo hakuweza kujibu.

              Mh Wassira akiwa katika eneo la Mradi huo

Mradi huo wa Maji katika wilaya ya Bunda unatekelezwa na Serikali kupitia Benki ya dunia ikiwa ni sehemu ya ahadi aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete wakati akiomba kura kwa Wananchi mwaka 2005 kwa ajili ya kutatua tatizo la Maji kwa mji wa Bunda na Vitongoji Vyake.

Hadi sasa ni wakazi zaidi ya 20,000 tu kati ya 83,000 wa mji wa Bunda  wanaopata huduma ya majisafi na salama na hali hiyo inachangiwa na uchakavu wa miundombinu ya maji iliyojengwa miaka 40 iliyopita.

No comments:

Post a Comment