Monday, February 6, 2012

Mji wa Homs watikisika kwa mashambulio

Homs
Picha iliyopigwa na mkazi wa Homs ikionesha mtu aliyejeruhiwa katika mapigano
Mji wa Homs nchini Syria imekuwa ukitikiswa na mashambulio mazito ya silaha, wakati majeshi ya Syria yakiongeza nguvu za kushambulia mji huo. 

Mwandishi wa BBC aliyeko huko anasema kuna milio inayofuatana, katika shambulio kali zaidi katika kipindi cha miezi 11 ya maandamano.
Rais wa Marekani Barack Obama amesema ni muhimu kumaliza mzozo huo bila kuingilia kijeshi. Wakati huohuo, Urusi na Uchina zimetetea kura yao ya veto katika muswada wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, hatua ambayo imewakasirisha mahasimu wa Rais Bashar al-Assad.

Mji wa Homs, moja ya ngome kubwa zinazopinga utawala wa Bw Assad, umekuwa ukishambuliwa na majeshi ya serikali kwa siku kadhaa.

Mwandishi wa BBC Paul Wood ambaye ameweza kuingia katika mji huo amesema mashambulio yalianza alfajiri ya Jumatatu. Baadhi ya waasi wamekuwa wakijibu mashambulizi hayo ingawa mwandishi wetu anasema hatua hiyo haina mafanikio makubwa.

Waasi wanadai kuwa mashambulizi ya majeshi ya serikali yameteketeza hospitali katika wilaya ya Baba Amr na kusababisha vifo. Hata hivyo mwandishi wetu anasema taarifa hizo ni vigumu kuzithibitisha.
Hospitali hiyo inatibu watu wengi waliojeruhiwa katika mashambulio ya awali katika mji wa Homs.
Mwanaharakati mmoja anayepiga serikali ameiambia BBC kuwa serikali inatumia helikopta na vifaru katika mashambulio yao.

Wanaharakati wanasema watu wasiopungua 15 wameuwawa siku ya Jumatatu.
Kituo cha TV cha Syria kimesema "magenge ya kigaidi" yamelipua majengo mjini Homs.
Shirika la habari la serikali Sana limeripoti kuwa bomba la mafuta karibu na jiji hilo limelipuliwa siku ya Jumatatu. Limelaumu "magaidi" kwa tukio hilo.

Vyombo vya habari vya Syria pamoja na wanaharakati wanaripoti kuwepo kwa mapigano katika mji wa kaskazini wa Idlib na mji wa Zabadani kaskazini magharibi mwa Damascus.

Serikali imesema inapambana na wapiganaji kutoka nje ya nchi wanaoungwa mkono na makundi yenye silaha. Maelfu ya wanajeshi wa serikali wameasi na kuingia upande wa waasi na kuunda jeshi lijulikanalo kama Free Syrian Army.

No comments:

Post a Comment