Sunday, June 19, 2011

UNYANYASAJI WA WATOTO CHANZO CHA KUKIMBILIA MITAANI


MUSOMA

 
JAMII imetakiwa kuheshimu haki za watoto na kuzithamini ikiwa pamoja na kuwasikiliza watoto kama ishara ya kuonyesha upendo na kuthamini mchango wa waototo

 
Hayo yamesemwa mjini hapa na wadau mbalimbali wanaotetea haki za watoto mbalimbali katika warsha ya siku tano iliyoandaliwa na shirika la  kusaidia wajane na watoto (Center for widows and Children Assistance) tawi la Musoma  ambayo imefanyika katika ukumbi wa angilikana  mjini hapa.

 
Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya warsha hiyo mjini hapa Wakili na mwanasheria Mwanadamizi  wa shirika hilo Ostack Mligo tawi la Musoma alisema kuwa mradi huo  wa haki za watoto ni muhimu kuieleza jamii hasa katika kipindi hiki ambacho kumeonekana jamii kukiuka haki za watoto.
Alisema warsha hiyo iliyodhaminiwa na wafadhili kutoka nchini Uholanzi ni mahususi katika jamii kutambua haki za watoto ambapo kwa mkoa wa Mara watoto wanatendewa visivyo.

 
“Mradi huu ni kutaka kuifahamisha jamii juu ya haki za watoto ambazo zimekuwa zikikiukwa hapa mkoani Mara”
Mwansheria huyo alisema kuwa kumekuwepo na vitendo vya kinyanyasaji kwa watoto na hasa kuwatumikisha katika migodi ya dhahabu na sehemu za uvuvi hivyo semina hiyo ni ishara nzuri kwa jamii katika kupunguza vitendo vya kinyanyasaji.

 
Wakili Mligo aliongeza kuwa ugomvi katika familia pia unasababisha ukosefu wa haki za watoto huku akisema kuwa jamii imetakiwa kushikamana ili  kukomesha vitendo  hivyo ikiwa pamoja na kutoa elimu
 “Jamii lazima ishikamane katika hili na kutoa elimu ya kutosha  juu ya haki za watoto hasa katika kipindi hiki tunachoadhimisha siku ya mtoto wa Afrika” aliongea wakili huyo.
Naye mwezeshaji wa warsha hiyo kutoka jijini Dar es Salaama mwanasheria Projestus  Rwehumbiza alisema jamii inatakiwa kuthamini haki za watoto ikiwa pamoja na kufahamu sheria  ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009

 
Alisema sheria hiyo ni mpya hivyo jamii inatakiwa kuisoma na kuelewa ili baadaye wasije wakajiingiza katika matatizo baada ya kukiuka sheria hiyo.

 
  “ Sheria hii ni mpya na kama ni mpya jamii inatakiwa kuifahamu ili isije ikajikuta inapata matatizo kwa kigezo cha kutojua sheria hiyo” alisema mwezeshaji huyo

 
Aidha Mkaguzi msaidizi wa jeshi la Polisi mkoani Mara Fatuma Mbwana  alisemakuwa vituo vingi mkoani Mara havina mahabusu za watoto  kitu ambacho kinakiuka haki za watoto.

 
Warsha hiyo ya siku tano ilikuwa mahususi katika kuangalia juu ya ongezeko la watoto wa mitaani ikiwa ni njia ya kukumbuka siku ya mtoto wa Afrika
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,

No comments:

Post a Comment