Wednesday, June 15, 2011

RAIS KIKWETE KUHUTUBIA MKUTANO WA ILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ni miongoni mwa viongozi saba duniani ambao watakuwa wageni maalum kwenye Mkutano wa kihistoria wa 100 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ulioanza Juni Mosi mwaka huu mjini Geneva, Uswisi.
Rais Kikwete ambaye ameondoka nchini asubuhi ya leo, Jumanne, Juni 14, 2011, kwa ziara ya siku tatu nchini Uswisi, amepangiwa kuhutubia mkutano huo mchana wa kesho, Jumatano, Juni 15, 2011, akiwa mgeni maalum wa mwisho kuhutubia mkutano huo unaomalizika Ijumaa ya wiki hii.
Viongozi wengine maalum walioalikwa kuhutubia mkutano huo ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mheshimiwa Susilo Bambang Yudhoyono na Kansela wa Ujerumani, Mheshimiwa Angela Merkel ambao wanahutubia mkutano huo leo.



Viongozi wengine watakaohutubia mkutano huo unaojumuisha washiriki kutoka nchi zote 183 wanachama wa ILO ni Waziri Mkuu wa Russia, Mheshimiwa Vladimir Putin; Rais wa Jamhuri ya Uswisi, Mheshimiwa Micheline Calmy-Rey; Rais wa Finland, Mheshimiwa Tarja Kaarina Halonen, na Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Palestine, Mheshimiwa Salam Fayyad.
Shughuli za mkutano huo wa 100 tokea kuanzishwa kwa ILO mwaka 1919, unaodhuhuriwa kiasi cha watu 7,000 unashirikisha viongozi wa nchi na serikali wa zamani, mawaziri wa nchi mbali mbali, taasisi za kimataifa, na taasisi za kiraia.
Mada za jumla zinazozungumzwa katika mkutano huo ni pamoja na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira duniani, zahama ya kimataifa ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, jinsi ya kuongeza kiwango cha kulinda watu zaidi duniani kupitia mifuko ya hifadhi za kijamii, na haki za wafanyakazi na watumishi kazini na hasa zile za watumishi wa ndani.
Mada mahsusi zitakazozunguzwa kwenye mkutano huo ni Ajira na Haki za Kijamii katika Dunia ya Utandawazi; Nafasi ya Ajira ya Heshima katika Utandawazi wa Haki Zaidi, Kijani Zaidi na Endelevu Zaidi; Mafunzo Kutokana na Zahama ya Karibuni Katika Kujenga Jamii Eendelevu na Zenye Kushirikiana; na Umuhimu wa Nyakati Mpya za Haki za Kijamii.
Katika barua yake ya mwaliko, Mkurugenzi Mkuu wa ILO Dkt. Juan Somavia amempongeza Rais Kikwete kwa mpango mzuri wa ajira katika Tanzania ujulikanao kama Tanzania Decent Work Country Programme na pia akakumbusha uhusiano wake na shughuli za ILO na jitihada zake za kutafuta na kuboresha ajira duniani hasa kwa vijana.
“Ulitupa heshima wakati ulipohutubia Mkutano wa 11 wa Mwaka wa Afrika Aprili mwaka 2007. Tunakushuru kwa uamuzi wako huo. Pia tunakupongeza kwa kazi uliyoifanya ukiwa mjumbe wa Tume ya Afrika – Danish Africa Commission – kuhusu namna ya kutafuta na kuongeza ajira kwa vijana,” amesema Dkt. Juan Somavia.

1 comment: