Tuesday, February 15, 2011

CHAKULA CHAPELEKWA KENYA KINYEMELA

TARIME
WAKATI baadhi ya maeneo mengi nchini yakikabilia na upungufu mkubwa wa chakula,imebainika kuwa zaidi ya tani 200 za Mahindi makavu zimekuwa vikivushwa kwa njia za magendo kila siku na kuuzwa nchi jirani ya Kenya.
Uchunguzi ambao umefanywa  kwa siku tatu mfululizo wilayani Tarime,umebaini kuwa mahindi hayo yamekuwa yakivushwa kwa kutumia baiskeli na magari madogo madogo kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya Sirari na njia za panya katika eneo la mpaka huo.
Baadhi ya wakulima na watu binafsi ambao wamekuwa wakijihusisha na ulanguzi wa mahindi kutoka kwa wakulima kutoka wilayani Tarime, wamesema hatua ya kuuza chakula hicho nje ya nchi inatokanana na bei nzuri inayotolewa nchini Kenya tofauti na hapa nchini.
Hata hivyo baadhi wananchi wamesema kuwa endapo serikali itashindwa kuchukua hatua za haraka za kudhibiti na kuanza mpango maalum wa ununuzi wa chakula hicho kutoka kwa wakulima kwa kutoa bei nzuri kuna hatari kubwa chakula chote kilichovunwa msimu huu kikashia nchini Kenya jambo ambalo linaweza kusababisha njaa kubwa.
Akizungumza kwa njia ya simu afisa kilimo na mifugo wa wilaya ya Tarime Bw Slvanus Gwiboha,amesema tayari uongozi wa wilaya umepiga marufuku uuzwaji wa chakula nje ya nchi huku akikiri kuwa kumekuwa na tatizo kwa baadhi ya watu kufanya biashara hiyo kwa njia zisizo rasmi ambapo ameahidi kushirikiana na vyombo vya dola kudhibiti hali hiyo.
SERIKALI YAOMBWA KUTATUA MIGOGORO TARIME

SERIKALI imeombwa kuchukua hatua za haraka za kuweka mipaka kati ya vijiji na kata za Mwema na Sirari wilayani Tarime ambayo imekuwa chanzo kikuu cha mapigano ya mara kwa mara ya koo za Wanchari na Wakira.
Ombi hilo limetolewa na wazee wa mila wa koo ya Wanchari,viongozi wa dini na taasisisi mbalimbali katika kata ya Mwema wakati wakizungumza na maafisa kutoka taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Corridor of Peace inayojihusisha na mambo ya amani ambao wanatembelea vijiji ambavyo vimekuwa vikikumbwa na mapigano hayo ya koo.
Mmoja wazee hao Bw Thobias Magere,akizungumza na ujumbe wa maafisa kutoka taasisi hiyo,amesema kumekuwa na mgogoro wa ardhi kwa zaidi ya miaka 30 sasa kwa kuhusisha koo ya Wakira kutoka kata ya Sirari na Wanchari katoka kata ya Mwema jambo ambalo limekuwa likisababisha mapigano na uhalibifu mkubwa wa mazao mashambani.
Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Koratambe katika kata ya Mwema Bw Chacha Kirutu,amesema tangu kuibuka kwa mapigano ya koo kijiji chake kimepoteza zaidi ya watu 45 waliuawa kwa kukatwa mapanga na kuchomwa mishale na mikuki huku zaidi ya nyumba 180 na maghala ya vyakula 300 yakichomwa moto huku zaidi ya kaya 700 zikikosa makazi hadi sasa.
Naye mkurugenzi wa mradi huo wa kujenga Amani kutoka taasisi ya Corridor of Peace Bw Nyasigo Emenuel,amesema lengo la kuwakutanisha wananchi wa koo hizo ni kuona njia sahihi za kuwajengea uwezo wa kutatua migogoro hiyo ya ardhi wenyewe pasipokutumia mapigano ambayo yamekuwa yakisababisha madhara makubwa kwa jamii.

No comments:

Post a Comment