Monday, January 31, 2011

WAFANYAKAZI NCHINI WATAKIWA KUJITATHIMINI KWANZA


SERIKALI nchini imewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa kuwajali wateja ikiwa pamoja na kujiwekea malengo na kutumia mfumo wa kujitathimini mwenyewe (OPRAS) katika utendaji wa kazi.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa na waziri wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma Hawa Ghasia kwenye ufunguzi mafunzo kuhusu mabadiliko katika utumishi wa umma kupitia mikataba ya huduma kwa mteja na OPRAS wilaya ya Musoma mkoani Mara.

Waziri huyo aliwataka watumishi kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wafanye kazi kwa malengo huku wakitizama wanapotoka,walipo na wanapokwenda ili kuimarisha uchumi wa nchi na wao kwa ujumla.

Mbali na hivyo Ghasia aliwataka  watumishi wa umma kufahamu kuwa kipimo hicho  OPRAS kwa mtumishi wa umma ni kipimo ambacho hutoa majibu sahihi ya utendaji kazi kwa mtumishi yeyoyote hivyo wasiogope wala kuogopeshwa na baadhi ya watumishin ambao hawana mapenzi mema na serikali yao.

 “Kipimo hicho kinatoa matokeo sahihi kama kweli ulifanya vizuri au la hivyo msiogope wala kudanganywa na mtu kuhusu kipimo hicho”alisema Waziri huyo

Aidha waziri huyo alisema serikali itachukua hatua ya kuwajengea wananchi uwezo wa kutambua mikataba ya huduma kwa mteja ili kuelewa huduma zinazotolewa na kila taasisi  husika namna ya kuzipata huduma hizo wajibu wa kuzipata na namna ya kulalamika pale ambapo hawapatiwi huduma.

Pamoja na hivyo pia Waziri huyo alisemakuwa serikali itawachukulia hatua kali za kisheria kwa wakuu wote wa serikali ambao hutumia majina hewa kujinufaisha,aliongeza kuwa kuna baadhi ya watumishi ambao tayari wamefariki lakini bado inaonyesha wanapokea mshahara na wengine wakiwa wameachishwa kazi.

‘Hatutavumilia wale wote ambao wanatumia majina hewa kujinufaisha,hakuna taarifa yoyote lakini bado mtu huyo anaonekana yupo kazini wakati aliishafariki hivyo serikali haitavumilia” aliongeza Ghasia

 Naye mkuu wa mkoa wa  Mara Kanali mstaafu Enos Mfuru alisema kuwa ni jukumu la kila mtumishi wa umma kujua majukumu yake sanjari na kuwajibika kiutendaji zaidi badala ya kufanya kazi kimazoea.

Mfuru alisema kuwa mfumo huo uliobuniwa na serikali ni mfumo ambao utamsaidia mtumishi kuboresha maslahi yake kufuatia utendaji kazi ambao utamlazimu mtumishi kujitathimini.

Alisema kuwa mfumo huo wa OPRAS ndio mfumo utakaokuwa unatumika katika kuwapata wafanyakazi bora katika kutoa tuzo na kuwapandisha madaraja.

Mafunzo hayo yalikuwa ya siku moja ambapo yalifanyika katika ukumbi wa uwekazji mjini hapa na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa siasa

No comments:

Post a Comment