Wednesday, January 19, 2011

KANISA LA ANGLIKANA LATOA MSAADA

KANISA la Anglikana dayosisi ya Mara limekabidhi mradi wa mashine mbili za kusaga nafaka zenye jumla ya thamani ya milioni 6,580,000 kwa wilaya ya Musoma vijijini na Serengeti kwa nyakati tofauti.

Mratibu wa mpango wa utume na maendeleo katika dayosisi hiyo Rhobi Samweli akisoma risala katika makabidhiano ya mradi huo jana katika kijiji cha Kirumi kitongoji cha Mang’ore wilaya ya Musoma vijijini alisema kuwa mradi huo umetekelezwa katika wilaya mbili tofauti ambapo kwa kuanza kukabidhi miradi hiyo walianza katika wilaya hiyo.

Alisema kuwa malengo ya kuweka mradi huo katika kijiji hicho ni kuwapunguzia wakina mama kazi nzito za kusaga unga au nafaka ya aina yoyote kwa kutumia vinu au kuponda kwa kutumia mawe kwenye miamba.

Aidha alisema kuwa wakina mama wa kitongoji hicho hushindwa kufanya shughuli zingine za kujitafutia kipato kutokana na kutumia mda mrefu na siku nyingi katika kuandaa unga wa chakula kwa kuwa katika kitongoji hicho hakuna mashine za kusaga.

Nae mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Musoma Kepteni mstaafu Geofrey  Ngatuni akihutubia wakazi alisema kuwa msaada uliotolewa na kanisa hilo ni mchongo mkubwa sana kwa kuwa wananchi wa eneo hilo walitaabika kwa mda mrefu bila serikali kuwa na taarifa za hitaji hilo kwao.

Aidha alisema kuwa michango inayotolewa na makanisa inatakiwa kuheshimiwa kwakuwa serikali haiwezi kutekelezwa kila hitaji la wananchi kutokana na mahitaji kuwa mengi kupita kiasi.

Ngatuni aliwataka wananchi wa kitongoji hicho kuulinda mradi huo pasipo kutokea dosari za wizi kwa kuwa wahalifu hutokea katika maeneo wanayoishi hivyo aliwataka kila mmoja kuwa mlinzi wa mradi huo.

Katika hatua nyingine ya kukabidhi mradi wa mashine katika kijiji cha maji moto kitongoji cha Nymorongoro wilaya ya Serengeti mratibu huyo alisema kuwa mradi huo utawasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na yatima katika swala zima la elimu.

Alisema kuwa mradi huo umefadhiliwa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali,Britain-Tanzania Society na Tanzania Development Trust kutoka Uingereza ambapo alimkaribisha mwakilishi na kutoa nasaha zake kwa wananchi.

Kwa upande wake mwakalilishi huyo ambaye ni mwenyekiti wa mashirika hayo Uingereza  Jlian  Marcus alisema kuwa mashirika hayo yalianzishwa miaka 50 iliyopita ambapo alisema kuwa hayati baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mwasisi wa mashirika hayo.

Marcus alisema kuwa wao hutoa misaada midogo midogo kwa jamii ikiwepo na misaada ya kiroho lakini uwezo wa kutoa misaada mikubwa kama kujenga shule hawana.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Johaness Masirori alisema kuwa msaada huo ni changamoto kubwa katika kusaidia maendeleo ya kijiji hicho kwa kuwa kijiji hicho kipo nyuma katika swala zima la maendeleo.

No comments:

Post a Comment