Tuesday, January 18, 2011

BAADHI YA VIONGOZI SERIKALINI WASALITI


Mbunge wa viti maalum kupitia vijana mkoa wa Mara amesema baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali wamekuwa wakitumia kila mbinu ili kuhakikisha chama cha mapinduzi CCM kinaondoka madarakani. 

Mbunge huyo kijana Esther Bulaya ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji taifa na mkuu wa idara ya uhamasishaji na chipukizi taifa lisema hayo katika ukumbi wa ccm mkoa wa Mara mjini Musoma wakati akizungumza na wajumbe wa baraza kuu la UV-CCM mkoa wa Mara katika kuwashukuru kwa kumchagua kupitia kuwawakilisha kundi hilo na hatimaye kushinda nafasi hiyo ya ubunge. 

Alisema kwa sasa kuna mambo ya msingi ambayo yanapaswa kusimamiwa na serikali ili kuondoa kero kwa wananchi hasa katika sekta ya elimu ya juu lakini viongozi hao kwa mbinu chafu walionayo kwa chama cha mapinduzi wamekuwa wakishindwa kutimiza wajibu wao katika kuichonganisha serikali ya ccm na wananchi. 

Mheshimwa Bulaya alisema kuwa suala la migomo kwa vyuo vikuu nchini nalo limeingizwa kisiasa wakati ukweli unafahamika na hivyo baadhi ya viongozi kutumia nafasi hiyo katika kukihujumu chama.

“Kwa mfano suala la mgomo wa wanachuo pale chuo kikuu cha Dodoma wanasema Chadema ama siasa pale hakuna siasa hata kidogo wewe unawezaje mwanafunzi wa sayansi akafanya mafunzo kwa vitendo bila fedha kama hii si hujuma ya baadhi ya viongozi serikalini hapa hakuna uwajibikaji sisi wenyewe tunatengeneza misingi ya kukataliwa badae tunalalamika eti ni siasa”alisema mbunge huyo kijana. 

Katika mkutano huo Mheshimiwa Bulaya aliwaomba vijana wa CCM kutokubali kamwe Chama hicho kufia katika mikono yao bali washikamane kwa pamoja katika kuhakikisha wanakuwa wawazi kusema wote wenye njama chafu ya kusababisha chama hicho kueonekana hakifai mbele ya jamii. 

Alisema hakuna sababu ya serikali kutafuta mchawi kuhusu migomo inayoendelea katika vyuo vikuu nchini bali inapaswa kujipanga kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wanachuo na wahadhiri katika vyuo hivyo na kuchukua hatua kwa watendaji wote wanaonekana kuwa kikwazo kwa serikali katika kutimiza majukumu yake. 

Aidha katika kipindi cha miaka mitano mbunge huyo alisema atahakikisha anatetea kwa nguvu zote kundi la vijana hasa katika suala la ajira pasipokujali itikadi za kisiasa ili kujenga taifa moja lenye mshikamono wa dhati na moyo wa uzalendo.
Bulaya waliwahimiza vijana hao kutumia nafasi za ajira zinazopatikana katika halmashauri badala ya kukaa vijiweni ikiwa ni pamoja na kubuni mbinu mbalimbali za kujiari kwa kutumia vikundi vya vijana ambavyo vitawawezesha kupata mikopo kutoka katika mifuko mbalimbali ya halmashauri na vyombo vya fedha. 

Alisema kwa sasa uchaguzi umekwisha hivyo ni vyema wananchi wote wakaungana katika kulijenga taifa lao kwani itikadi za kisiasa zitachelewesha maendelo kwa ujumla
Katika hitimisho kwenye kikao hicho mbunge huyo alisema baada ya kumaliza kikao cha bunge lijalo la februari atafanya ziara kila wilaya ya mkoa wa Mara kwaajili ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero zinazohusu kundi la vijanao na kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo kwa  haraka.

Mwisho

No comments:

Post a Comment