Makamu
wa Rais wa Jmhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mohammed Gharib Bilal
ameiwakilisha Tanzania katika mkutano wa mashirikiano baina ya nchi za Afrika
na zile za Kiarabu, mkutano wa siku mbili unaofanyika katika nchini Kuwait.
Mkutano huo unaohudhuriwa na viongozi wa nchi zaidi ya 70 unalenga kuimarisha
ushirikiano wa Afrika na nchi za Kiarabu na unapitia makubaliano ya mkutano wa
Sirte, Libya uliofanyika mwaka 2011.
Mkutano
huu unafanyika kukiwa na mabadiliko kadhaa ya kiasiasa, kiuchumi na kimkakati
baina ya nchi za kanda hizi mbili huku taswira ya kukua kwa ushikiano huu zikionekana
bayana kuwa muhimu zaidi sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Hii inatokana na
nchi za kanda hizi mbili, kukabiliwa na changamoto nyingi zinazofanana na
zinazohitaji majibu ya pamoja baina ya nchi za kanda hizi mbili. Baadhi ya
changamoto hizo ni pamoja na; mtikisiko wa uchumi, hali ya ulinzi na usalama,
majanga yanayoikabili dunia, usalama wa chakula na ugaidi.
“Changamoto
hizi hatuwezi kuzikabili wenyewe kama Tanzania ama kama Afrika. Tunahitaji
wenzetu wa ukanda huu wa nchi za Kiarabu kushirikiana nasi. Katika umoja wetu
tutafanikiwa kirahisi kuliko kama tutazikabili changamoto hizi tukiwa
tumejitenga,” alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais.
Tanzania
licha ya kuwa na wananchi wake katika nchi mbalimbali za dunia, tawimu zinaonesha
kuwa, idadi kubwa ya wananchi hao wapo katika nchi za Kiarabu hali inayoashiria
umuhimu wa kukuza mahusiano baina ya Tanzania pekee dhidi ya ukanda wa nchi za
Kiarabu. Katika siku za hivi karibuni kupitia Diplomasia ya Uchumi, Tanzania
imefungua njia kwa wawekezaji wa nchi za Kuwait, Oman na UAE na sasa taswira ya
mahusiano ya Tanzania na nchi hizi ni ya kuvutia ambapo inatoa fursa za
kunufaika kiuchumi kwa Tanzania kutoka katika ukanda huu kuliko kwa wadau wa
maendeleo wa kanda zingine ambazo Tanzania imekuwa ikishirikiana nazo.
Akizungumza
wakati wa kutoa taarifa ya kikao hiki kwa Makamu wa Rais, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia yupo katika msafara wa Mheshimiwa
Makamu wa Rais, Bernard Membe alisema, kazi kubwa ya mahusiano baina ya
Tanzania na nchi za ukanda huu imejengwa na Rais Jakaya Kikwete na sasa milango
imefunguliwa kwa Watanzania kuchangamkia fursa za maendeleo hasa katika suala
zima la masoko ya bidhaa za kilimo, ufiugaji na utalii.
Katika
Hotuba yake kwenye mkutano huu, Mheshimiwa Makamu wa Rais licha ya kutoa
shukrani na salamu za Tanzania kwa Amiri wa Kuwait, Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber
Al-Sabah na wananchi wa Kuwait na kwa viongozi wote wan chi za kanda hizi
mbili, Mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua kuwa Tanzania inatambua mahusiano
ya kitamaduni, kihistoria na kijiografia yaliyopo baina ya kanda hizi mbili na
kwamba zaidi ya theluthi mbili ya watu wa ukanda wa nchi za Kiarabu wanaishi
Afrika hali inayochagiza umuhimu wa uhusiano wa kanda hizi.
Pia Mheshimiwa
Makamu wa Rais alifafanua kuwa, Mkutanouliofanyika Libya mwaka 2011,
haukuonesha mafanikio ya wazi hasa katika miradi ya Maendeleo na akauomba
mkutano huu wa Kuwait, kuhakikisha kanda hizi zinaongeza spidi ya kufanikisha
malengo ya kimaendeleo, ili wananchi wa kanda hizi wazidi kunufaika kutokana na
mahusiano haya.
Katika
msafara huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais pia ameambatana na Waziri wa Kilimo na
Chakula, Enginia Christopher Chiza, Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati wa
SMZ, Ramadhan Shaaban, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu, Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha, Servacius Likwelile na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na
Biashara, Uledi Mussa. Pia katika msafara huo wapo wabunge Hamad Rashid na
Khalifa Khalifa.
Imetolewa na: Boniphace Makene
Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais
No comments:
Post a Comment