Tuesday, August 14, 2012

WANAHABRI MARA WAPIGWA MSASA KUANDIKA HABARI ZA AFYA

MUSOMA

MUUNGANO wa vilabu vya waandishi wa habari nchini UTPC, umenza kutoa mafunzo maalum kuandika habari za afya kwa waandishi wa habari katika mikoa yote nchini.

Hatua hiyo inalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuandika habari za afya  zilizofanyiwa utafiti wa kina kwa lengo la kuboresha sekta afya na kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii.



Mkurugenzi wa UTPC Bw Aboubakar kassan, ameyasema mjini Musoma wakati wa mafunzo ya kwanza ya siku nne kuanza kutolewa nchini kwa waandishi wa habari mkoani Mara ikiwa ni sehemu ya utatuzi wa matatizo na kuibua changamoto zinazokabili utoaji wa huduma ya afya nchini.

Amesema kwa muda mrefu jamii imekuwa ikikabiliwa na sintofahamu juu ya kujikinga na maambukizi ya magonjwa hususan Ukimwi kutokana na waandishi nchini kutoandika habari ambazo zimefanyiwa utafiti wa kina  ambao haotoi majibu ya namna ya kujikinga na maambukizi mapya.

Kwa sababu hiyo ametoa wito kwa wanahabari mkoani Mara kutumia vema nafasi ya mafunzo hayo kwa lengo la kuibua changamoto zinazokabili sekta ya afya hasa maeneo ya vijijini ili kuwezesha wananchi kutumia mbinu bora za kujikinga na maradhi.

Kwa mujibu wa mwezeshaji wa mafunzo hayo DK Ahmed Twaha,amesema takwimu za kiafya hususan katika maeneo ya vijijini zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanaofika katika vituo vya afya ni wanawake na watoto hivyo wanahabari wanapaswa kuibua mbinu kadhaa ya kunusuru kundi hilo kwa kuripoti njia bora za kujikinga na maambukizi ya maradhi kama vile Ukimwi na Malaria.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,

BUNDA

Makarani 15 ambao wameshiriki katika mafunzo ya namna ya kujaza madodoso yatakayotumika wakati wa zoezi la Sensa ya watu na makazi wilayani Bunda  mkoani Mara,wameondolewa kushiriki mafunzo hayo baada ya kubainika kutojua kusoma wala kuandika.

 Mratibu wa Sensa katika wilaya ya Bunda Bw Donatus Wegina,amesema  kuwa watu hao licha ya kupitishwa na kamati ya sensa ya wilaya kuwa miongoni mwa makarani watakaoshiriki zoezi hilo waliridhishwa na barua zao za maombi hivyo baada ya kubainika kuwa hawajui kusoma na kuandika vema wameondolewa.

 Amesema kabla ya kuchukua uamuzi wa kuwaondoa watu hao,wamekuwa wakishiriki mafunzo hayo ambapo baada ya wakufunzi wao kupitia kazi ya mshiriki mmoja mmoja ili kujua kama wanajaza madodoso kwa kufuata maelekezo ndipo wakawabaini watu hao kujaza tofauti tena katika mwandiko usiiosomeka kirahisi hali iliyoashiria kuwa hawajui kusoma.

Akifungua mafunzo hayo katika chuo cha Ualimu Bunda cha mjini humo,mkuu wa wilaya Bunda Bw Joshua Mirumbe, amesisitiza kuwa pamoja na mafunzo hayo lakini pia kutakuwepo na mchujo wa mara kwa mara miongoni mwa washiriki ili kubaini kama kuna watu ambao hawafuati maelekeoz katika ujazaji wa madodoso na kuwaondoa wasije wakajaza isivyo.

Jumla ya makarani 548 wakiwemo walimu 266,watumishi wa kada mbalimbali 176 na watu wa kawaida 106 wanashiriki katika mafunzo hayo yanayofanyikia katika vituo vya chuo cha Ualimu Bunda na Kibara ili kuwajengea uwezo juu ya kufanya kazi hiyo vizuri siku ya sensa Agosti 26 mwaka huu.          
,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,,,
ABIRIA-TARIME

ABIRIA  waliokuwa wakisafiri kwenda maeneo mbalimbali Wilayani Tarime na Musoma Mkoani Mara,wameshidwa kusafiri na kisha kuendelea kusota kituo cha mabasi mjini Tarime baada ya wamiliki wa magari kugoma  kusafirisha abiria kufuatia SUMATRA kushusha viwango vya nauli.

Kufuatia agizo hilo la SUMATRA polisi wilayani Tarime wamefanya zoezi la kukagua tiketi kwa abiria wote ambao walikuwa wakisafiri kuona kama igazo hilo limetekelezwa.

Baadhi ya wamiliki wa magari katika wilaya ya Tarime wamesema kuwa Viwango vipya vilivyopangwa na Sumatra Kutoka Wilayani Tarime hadi Musoma ni 2900  mwendo wa km 87 ambapo kwa nauli ya zamani ilikuwa sh 4,000, magari yatokayo Tarime kwenda Shirati ni 1,700 bei ya zamani 5,000 km 57,magari yatokayo Tarime kwenda Nyamongo 1,700 km 37 bei ya zamani 5,000,magari yatokayo Tarime kwenda Sirari  700 km18 bei ya zamani ilikuwa 1,500,Tarime hadi Mugumu 5,800 bei ya zamani 7,000.
 
Baadhi ya wamiliki hao wa magari wamesema kuwa viwango vya nauli  vilivyopangwa na SUMATRA  ni vya chini  kutokana  umbali,gharama za mafuta pia havikuzingatia ubovu wa miundombinu ya barabara katika maeneo hayo.


Kwa sababu hiyo wameitaka SUMATRA kurekebisha viwango hivyo na kuwa mgomo huo ni endelevu hadi pale Serikali itakaposikiliza vilio vyao  nakufanya mabadiliko ya bei hiyo mpya ya nauli kwa wasafiri.

Afisa Mfawidhi Mamlaka ya usafirishaji Sumatra Mkoa wa Mara Bw Maico Lojasi,amesema kuwa viwango vilivyopamgwa vimefuata taratibu zote za usafirishaji na kiuchumi na kwamba wamiliki wa magari wamekuwa wakijipangia nauli zao wenyewe jambo ambalo linawaumiza wananchi.

,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,MWISHO,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,

TARIME

SERIKALI imeipatia wilaya ya Tarime mkoani Mara vocha za pembejeo za ruzuku zeenye thamani ya shilingi bilioni 1.296 kwaajili ya ya msimu wa kilimo ambao umeishia june mwaka huu.

Afisa kilimo wa wilaya ya Tarime Bw Bw Selvanus Gwiboha,amesema vocha hizo zimetosheleza wakulima 18,000 wakati mahitaji yalikuwa ni wakulima 42,000 kwa wilaya ya Tarime.

Amesema pembejeo hizo ambazo zilisambazwa kwa wakulima hao ni pamoja na mbolea ya kupandia aina ya DAP,kukuzia aina ya UREA na Mahindi Chotara huku vijiji 89 vikinufaika na vocha hizo za pembejeo hizo za ruzuku.

Afisa kilimo huyo ameongeza kuwa wilaya ya Tarime ina eneo linalofaa kwa kilimo ni zaidi hekta 790,630 ambapo eneo linalolimwa ni hekta 69,155 sawa na asilimia 76.30 eneo linalofaa kwa kilimo.

,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,, 
MGOMO-MUSOMA

MAASKOFU wa Kanisa la Anglikana katika Dayosisi ya Mara na Tarime  mkoani Mara,wameishauri Serikali kuacha kutumia Mahakama na vyombo vyake vingine vya dola kama  kinga  katika kumaliza migomo ya walimu,bali watumie njia ya mazungumzo katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu.

Wamesema kuwa hatua hiyo italiepusha taifa na hatari ya kushuka kwa kiwango cha elimu kwa vile watumizi hao wanaweza kurudi kazini na kufanya kazi kwa kinyongo na chuki kwaajili ya kuwakomoa wanafunzi.

Kauli hiyo imetolewa mjini Musoma na maaskofu hao Mhasham Hilkiah Omindo wa Dayosisi ya Mara na Dk Raphael Akiri wa Dayosisi ya Tarime,wakati wakizungumza na wazazi pamoja na wanafunzi wa shule  ya ACT Mara,inayomilikiwa na kanisa hilo ikiwa ni sehemu ya kuwaaga wanafunzi wa darasa la saba.
Wameongeza kuwa madhehebu ya dini yamekuwa yakipata mafanikio katika sekta ya elimu kutokana na kukabiliana na changamoto hizo kwa walimu kabla ya kuleta athari kwa jamii.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo,Bi Apaisaria Kiwori,ameonya tabia ya baadhi ya vijana ya kujiingiza katika matendo maovu yakiwemo ya matumizi ya madawa ya kulevya jambo ambalo amesema limechangia kwa kiasi kikubwa kudidimiza maadili ya vijana wengi nchini.
 ,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,


Tarime.

WAMILIKI wa magari yanayofanya safari zake ndani ya Wilaya ya Tarime hadi Musoma wametakiwa kustisha mgomo na kisha kurejesha magari yao stendi  ili kusafirisha Abiria vinginevyo watakao endelea na mgomo wamedaiwa kufutiwa Leseni zao za gari.

Ni baada ya mgomo  unaoendelea  wa wamiliki wa magari Tarime ambapo leo ni siku ya pili  magari Tarime kutosafirisha abiria maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya hadi Musoma  baada ya SUMATRA Mara  kushusha na kuweka viwango vipya vya nauli kwa magari yanayofanya safari zake Tarime- Musoma,Nyamongo,Sirari,Mugumu na Shirati,ambapo Viwango vipya vya nauli ni 2900 kutoka Tarime-Musoma,Tarime hadi Nyamongo 1700,shirati 1700,Sirari 700 na Mugumu 5,800.

Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya usafirishaji SUMATRA  Mkoa wa Mara Maico Rojas alisema kuwa endapo wamiliki wa magari wataendelea na msimamo wao kuzuia magari watafutiwa leseni.

“viwango tulivyoweka  vimefuata taratibu  zote na za kiuchumi tumefanya uchunguzi tukagundua wamiliki wa magari wamekuwa wakijipangia nauli  zaidi ya mara mbili  ya viwango vya Serikali,kuna magari  madogo yanayofahamika kama michomoko hayatakiwi kufanya kazi  ya kubeba abiria isipokuwa  kwa magari makubwa aina ya Costa na Haice ndiyo yanatakiwa kubeba  kwahiyo tunafanya taratibu za kuyastisha tumefanya mabadiliko kutokana na malalamiko ya Madiwani Tarime kudai vipunguzwe viwango vya nauli watakao kiuka tunawafutia leseni. “ alisema Rojas.

Rojas aliwataka wamiliki wa magari wenye nia ya kusafirisha abiria kuendelea na kazi na kwamba wale wote watakaobughuziwa na kuzuiliwa na wamiliki wenzao  wanapaswa kutoa taarifa SUMATRA au Polisi ili wawajibishwe.

Rojasi alisema kuwa kitendo cha magari kusimama na kutofanya shughuli ni kuwakwamisha wasafi mahali waendako na kwamba endapo wanaona  bado gharama za mafuta ziko juu wanatakiwa kutoa malalamiko yao katika mamlaka inayohusika ili  hatua zichukuliwe.

Pia mmoja wa  wapiga debe stendi  James Juma alisema kuwa mgomo huo wa magari umewaathiri kwani fedha wanazozipata za kumudu familia zao zinatokana na upigaji debe  wa magari ya abiria.

Hata hivyo wamiliki wa magari  walisema kuwa bado wanaendelea na mgomo hadi pale serikali itakapofanya marekebisho ya viwango vya nauli kwa madai kuwa hawawezi kushusha bei kwakuwa gharama za mafuta bado ziko juu ambapo kwa upande wa disel  kwa lita moja ni 2300 huku petrol ikiuzwa 2500.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,

No comments:

Post a Comment