VIGOGO WANNE KUFIKISHWA MAHAKANI MARA
VIGOGO wanne
katika halmashauri ya Musoma vijijini mkoani Mara huenda wakawa ni miongoni mwa
watu watakafikishwa mahakamani endapo itathibitishwa kuwa wamehusika katika
ubadhirifu wa vocha za ruzuku za pembejeo zenye thamani ya milioni 370.
Vigogo hao ambao
wanatajwa kuwa ni wajumbe wa kamati za ugawaji wa vocha hizo pembejea ni mbunge
wa jimbo la Musoma vijijini Nimrod Mkono,aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Musoma
Geofrey Ngatuni,mwenyekiti wa halmashauri Magina Magesa na aliyekuwa mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri hiyo Karaine Ole Kunei ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa
halmashauri ya Ngorongoro.
Hata hivyo
mwenyekiti wa halmashauri ya Musoma vijijini Magina Magesa,aliliambia Nipashe
jumapili kuwa katibu wa vikao vya ugawaji wa pembeje hizo ambaye ni mkurugenzi
mtendaji,hajawahi kumpa mwaliko yeye na mbunge wa jimbo kama wajumbe halali ili
washiriki katika vikao hivyo badala yake wamekuwa wakiwaandikiwa hudhuru katika
mahudhurio ya vikao hivyo.
“Ni kweli mimi
na mbunge(Nimrod Mkono) kwa nyadhifa zetu ni wajumbe lakini cha kushangaza
hatujawahi kupewa taarifa za vikao hivyo hata siku moja lakini katika
mahudhurio wametuandikia tumeomba hudhuru wakati hatujawahi kuitwa wala hatujui
vikao hivyo…hapa anaejua suala hili ni katibu lakini mimi na mbunge
hatumo”alisema Magina.
Tuhuma za
ubadhirifu huo ziliibuliwa katika baraza la madiwani lilofanyija juzi mjini
hapa baada ya madiwani kukataa kupokea taarifa za upokeaji na ugawaji wa vocha
hizo za pembejeo za kilimo baada ya kubaini kuwa hakuna pembejeo ambazo
zimewahi kufikishwa kwa wakulima wa halmashauri hiyo katika msimu wa kilimo wa
mwaka 2011/2012.
Uamuzi huyo umefikiwa
katika kikao hicho cha kawaida cha baraza hilo chini mwenyekiti wake
Magina Magesa,ambapo kwa pamoja madiwani hao baada ya kukataa
taarifa hiyo wameunda tume ya watu sita ili kuchunguza tuhuma hizo.
Wakizungumza
kabla ya kuundwa kwa tume hiyo,baadhi ya madiwani hao bila kujali itikadi za
vyama vyao,wamedai kuwa hakuna hata kijiji kimoja cha halmashauri hiyo
kilichowahi kupokea pembejeo hizo za kilimo kama taarifa hiyo ilivyonyesha huku
ikitaja kuwa ununuzi wa pembejeo hizo umeigharimu serikali kiasi hicho cha
fedha.
“Mimi nilipata
taarifa za kuletwa vocha za ruzuku kutoka kwa mkuu wa mkoa eti halmashauri yetu
ililetewa vocha za milioni 370 lakini ukweli ni kwamba hakuna vocha iliywahi
kuletwa katika kata yangu…naungana na wenzangu tuunde tume kuchunguza tuhuma
hizi za wizi ili ikibainika wahusika wafikishwe mahakamani mara moja”alisema
diwani wa kata ya Tegeruka Alpha Mordekai.
Naye diwani wa
kata ya Mugango Wandwi Kunju,alisema upotevu wa pembejeo hizo ni miongoni mwa
tuhuma nyingi za ubadhifu wa fedha za serikali katika halmashauri hiyo jambo
lilokwamisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo mingine ikitekelezwa
chini ya kiwango hivyo kutaka baada ya tume hiyo kutoa majibu yake watuhumiwa
wafikishwe katika vyombo vya sheria kwaajili ya kuwatendea haki wananchi.
Kwa upande wake
akizungumza katika kikao hicho,mwenyekiti wa halmashauri hiyo Magesa,alisema
kitendo ambacho kimefanywa na idara ya kilimo katika kitengo cha vocha za
ruzuku za pembejeo,licha ya kuwa ni cha hujuma kubwa kwa wakulima,maendeleo ya
halmashauri hiyo pia kitafanya wananchi kukichukia chama cha mapinduzi na
serikali yake endapo hatua za kisheria hazitachukuliwa dhidi ya wahusika baada
tume hiyo kuwasilisha taarifa yake.
“Kwa mazingira
haya kweli watanzania tutafika hivi hapa ndo kusema CCM inawaletea neema
wananchi..lazima tuchukiwe iwe ccm,serikali na halmashauri yenyewe huu ni wizi
wa kutisha kama kweli kila diwani hajawahi kupokea pembejeo hata mimi ni mjumbe
sijawahi kuitwa katika kikao cha kugawa sasa tunakwenda wapi!kumbe ndio maana
mkuu wa mkoa alisema hawezi kuleta chakula cha msaada kwetu kwa vile alijua
tumeiba vocha za pembejea,kwa kweli lazima hatua zichukuliwe ili kuinusuru
serikali ya chama chetu”alisema Magina.
Hivi karibuni
mkuu wa mkoa wa Mara John Tupa,alibaini baadhi ya halmashauri katika mkoa wa
Mara kutumia vibaya vocha za pembejeo za ruzuku zingine zikiuzwa nje ya nchi
huku wakitumia wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari kusaini katika vitabu
maalum vya kupokelea vocha hizo kwa kuwafanya ni wakulima ambao walistahili
mgao huo.
Wakati huo huo
mgogoro mkubwa umelikumba baraza la Madiwani katika halmashauri ya Musoma
vijijini mkoani Mara hadi kufikia baadhi ya madiwani kutaka kupigana baada ya
madiwani wa tarafa ya Nyanja kupinga mgawanyo wa halmashauri hiyo ili kuwa
halmashauri mbili.
Mgogoro huo
ulikuja juzi baada kutokea tena hivi karibuni katika kamati ya fedha na mipango
jambo lilosababisha kuvunjika kwa kikao hicho na kupeleka hoja hiyo katika kikao
cha chama cha mapindizi ccm kabla kurudishwa juzi katika baraza hilo.
Hali hiyo
imetokea katika baraza la kawaida madiwani kufuatia Serikari kutaka
kuanza mchakato wa kugawa halmashauri hiyo ili moja ya halmashauri hiyo iwe ya
Butiama baada ya kupatikana kwa wilaya mpya ya Butiama.
Wakizungumza
katika kikao hicho kabla ya madiwani wa kata kumi na saba kati ya 34 kutoka wa
tarafa ya Nyanja bila ya kujali itikadi zao za vyama vya siasa kutoka nje ya
ukumbi,walisema kitendo cha kugawa halmashari hiyo huku ikiwa chini ya utawala
wa wilaya ya Butiama hakitawatendea haki wananchi.
“Hutuwezi
kukubali kuwa chini ya mkuu wa wilaya ya Butiama kwani kufanya hivyo ni
kutowatendea haki wananchi…mwananchi hawezi kutoka Busekera hadi Butiama zaidi
ya kilometa 200 kumtafuta mkuu wa wilaya wakati mkuu wa wilaya ya Musoma
anaweza kumuona kwa kutembea kilometa 50 tu jambo hili hatukabali hata
kidogo”alisema diwani wa Busekera katika kikao hicho Mambo Rebule akiwa
miongoni mwa madiwani 17 wa tarafa ya Nyanja baadhi ya kata za tarafa ya
Makongoro walipinga hoja hiyo na kutoka nje ya ukumbi
Aidha waliongeza
kuwa Jografia ya tarafa ya Nyanja itawafanya wananchi kushindwa kupata huduma
mbalimbali za kwa viongozi wa wilaya ya Butiama kutokana na umbali huo uliopo
huku wakisisitiza kuwa jambo hilo linapaswa kuangaliwa upya ikiwa ni pamoja na
kuendelea kuwa chini ya mkuu wa wilaya ya Musoma.
Hata hivyo baada
ya madiwani hao kutoka nje ya ukumbi,baadhi ya madiwani wa tarafa za Makongoro
na Kiagata wote wa chama cha mapinduzi,walipendeza kugawa halmashari
mbili kwa kuwa na kata ya kumi na saba kila moja huku halmashauri ya Nyanja
ikipendekezwa kujengwa eneo la Kwikonero kata ya Suguti,mapendekezo ambayo sasa
yatafikishwa katika kikao cha ushauri cha mkoa RCC.
No comments:
Post a Comment