Friday, August 10, 2012


ALIYEKUWA MHANDISI WA BUNDA NA SASA LUDEWA AFIKISHWA MAHAKAMNI NA TAKUKURU

MUSOMA

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru mkoani Mara imemfikisha mahakamani aliyekuwa mhandisi wa Halmashauri ya wilaya ya Bunda ambaye kwasasa amehamishiwa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa.

Taarifa iliyotolewa  kwa vyombo vya habari mkoani Mara na Naibu mkuu wa Takukuru mkoa wa Mara Bi Yustana Chagaka ilisema kuwa Taasisi hiyo imemfikisha Mahakamani  Bw Christopher Msafiri Nyandiga kwa kosa la kumdanganya mwajiri wake kinyume na kifungu cha 22 cha sheria ya Kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Alisema Bw Christopher Nyandiga kwa udanganyifu huo ameisababishia Serikali  hasara ya shilingi milioni 24 kinyume na kifungu cha 10 ibara ya 1 pamoja na vifungu vya 57 na 60 ibara ya 1 na 2 vya sheria ya Uhujumu Uchumi namba 200 iliyorekebishwa mwaka 2002.

Aidha Bi Chagaka alisema kuwa baada ya uchunguzi uliofanywa na Takukuru ilibainika kuwa kampuni inayomilikiwa na Mshitakiwa iitwayo MBULLY ENTERPRISES AND CIVIL WORKS ilipewa zabuni na halamshauri ya wilaya ya Bunda  ya kuleta Windmill aina ya POLDAW  ya mita 5.8  kwa gharama ya shilingi milioni 24,kusimika shilingi milioni 2 na kuifanyia majaribio shilingi milioni moja na hivyo kufanya jumla ya shilingi milioni 27 kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji  Mazao katika kijiji cha Kasuguti.

Alisema mbali na hatua hiyo Takukuru pia ilibaini kuwa Mnamo Desemba 2007 Mtuhumiwa kwa niaba ya Kampuni hiyo aliwasilisha hati ya Malipo namba 0152 kwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Bunda zenye maelezo ya uongo kuwa alikuwa amenunua Windmill moja aina ya POLDAW  ya mita 8.2 yenye thamani ya shilingi milioni 24 huku akijua si kweli .

Naibu mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Mara aliongeza kuwa  kifaa hicho hakikuwa kipya  bali kilikuwa chakavu na hivyo kuisababishia Serikali Hasara kubwa.

Aidha Bi Yustina Chagaka ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa Taarifa za vitendo vyote vya rushwa.   

No comments:

Post a Comment