DC BUNDA AMUWEKA AFISA AFYA RUMANDE
Na Shomari Binda
Bunda.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda Joshua Mirumbe amechukua maamuzi ya
kumuweka rumande Afisa Afya wa Mji mdogo wa Kibara James Manaji kwa kile
alichokieleza kushindwa kusimamia shughuli za Afya katika Mji huo na
kupelekea kuonekana usiofaa kwa makazi ya Binadamu.
Akizungumza na BINDA NEWS Mkuu huyo wa Wilaya alisema Afisa huyo
ameshindwa kutelekeza majukumu yake ya kazi kwa kushindwa kusimamia
shughuli zake na kupelekea kuonekana Mji mchafu huku akiendelea kuchukua
mshahara wa Serikali pasipo kufanya kazi zilizopo mbele yake.
Alisema makazi ya Wananchi wengi katika Mji huo zinaishi bila ya
kuwa na vyoo hivyo kujisaidia ovyo na kuhatarisha Afya na hivyo huenda
kupelekea kuibua kwa magonjwa na mlipuko ambayo yataatarisha maisha ya
Binadamu.
Mirumbe alisema Afisa huyo ameshindwa kusimamia
majukumu yake ipasavyo katika masuala ya Afya kwa kusema suala la choo
ni muhimu katika makazi na tayari yalishatolewa maagizo muda mrefu kwa
Maafisa wote wa Afya kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo kwa ajili ya
kujiepusha na magonjwa ya mlipuko.
"Ni kweli nimemuweka
ndani Afisa Afya wa Mji mdogo wa Kibara kwa kushindwa kusimamia majukumu
yake na suala hili ni nyeti kwa sababu hakuna jambo muhimu kama
kuzingatia taratibu za Afya hususani kuwa na choo katika makazi kwa
sababu tulishatoa maelekezo.
"Na hili si kwa kibara
tu,nimeshatoa maelekezo katika maafisa watendaji wote wa vijiji
kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo na kuhakikisha mazingira ya usafi
yanasimamiwa vizuri ili Wilaya ya Bunda ionekane ipo katika mazingira ya
usafi kwa wakati wote,"alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Alisema suala la uwajibikaji kwa watumishi wa idara zote lazima
lizingatiwe na kudai kuwa ataendelea kufanya ufatiliaji bila kikomo ili
kila mmoja aweze kutimiza wajibu wake wa kazi na kukomesha tabia ya
kukaa ofisini na kupiga gumzo huku kazi zikiendelea kusimama.
DC Joshua Mirumbe alichukua maamuzi ya kumuweka ndani Afisa huyo wa
Afya akiwa katika Mji huo wa Kibara wakati akikagua shughuli za
maandalizi yakiwemo ya usafi kwa ajili ya kupokea mwenge wa Uhuru ambao
unatarajiwa kuwasili Mjini Bunda agosti 18 huku miradi mbalimbali ya
maendeleo ikitarajiwa kuzinduliwa.
Kwa upande wake Afisa
huyo wa Afya wa Kibara James Manaji akizungumza na BINDA NEWS baada ya
kutoka ndani alikokaa kwa muda wa zaidi ya masaa 24 kabla ya kuamuliwa
kutoka, alisema alishangazwa na maamuzi ya Mkuu huyo wa Wilaya kumuweka
ndani bila ya kufanya Takwimu juu ya uhamasisishaji wa ujenzi wa vyoo.
Alisema kazi ya uhamasishaji wa ujenzi wa vyoo inaendelea kufanyika
vizuri katika vijiji vyote vinee vya Mji huo na hatua iliyochukuliwa na
Mkuu huyo wa Wilaya haikuwa sahihi kwa kuwa hakufanya utafiti wowote
juu ya jamabo hilo tangu ulipoanza utekelezaji wa kazi hiyo.
Alidai kuwa DC huyo amekuwa akichukua maamuzi mengine ambayo sio haki
tangu alipoteuliwa kusimamia Wilaya hiyo kwa mujibu wa dhana ya utawala
bora na kudai kuwa katika siku za vivi karibuni amekuwa akichukua
maamuzi kama hayo bila kufanya utafiti na kuvunja haki za msingi za
Binadamu.
No comments:
Post a Comment