Friday, June 1, 2012

MMOJA AUAWA KWA UJAMBAZI DODOMA
 
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi
 
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limefanikiwa kupata taarifa za mtandao wa majambazi waliokuwa wakivamia na kuwapora vifaa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Johns wanaoishi nje ya chuo hicho mjini Dodoma.
 
Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma SACP Zerote Stiven, amesema kuwa kubainika kwa mtandao huo kunatokana na kukurupushwa na kushambuliwa vibaya kwa mmoja wa majambazi hayo aliyejulikana kw ajina la Amor Makanya au Mhiri.
 
Amesema Polisi alipofika eneo la tukio na kumhoji mtuhumiwa huyo, alitoa maelezo yaliyofanikisha kukamatwa kwa baadhi ya vifaa vya wanafunzi hao ambavyo viliibwa katika matukio tofauti na kukutwa katika nyumba ya kulala wageni walimokuwa wakiishi watuhumiwa hao huku wakiendeleza wimbi la wizi kwa wananchi mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa chuo hicho.
 
Amesema katika upekuzi katika vyumba vya watuhumiwa walikuta laptop kadhaa ambazo zilitambuliwa kuwa ni miongoni mwa mali zilizoibwa kutoka kwa wanafunzi wa chuo hicho.
 
Amesema pamoja na mali hizo, Polisi pia walibaini kuwepo kwa tiketi mbalimbali za mabasi ambazo zilitumika kwa safari za ndani na nje ya nchi na hivyo kuongeza shaka kuwa huenda mtandao huo una uhusiano na mitandao mingine ya kihalifu kutoka katika nchi nyingine jirani.
 
Hata hivyo Kamanda Zerote alisema mtuhumiwa huyo alifariki dunia akiwa katika hospital ya Mkoa Dodoma alikopelekwa kwa matibabu kutokana na kipigo cha wananchi.
 
Kamanda Zeropte amesema kuwa kwa siku za hivi karibuni yamekuwepo matukio kadhaa ya kuvamiwa kwa wanafunzi wa chuo hicho waliokuwa wakiishi nyumba za binafsi katika mitaa ya Kikuyu Kaskazini na Kusini mjini humo ambapo kuanzia Mei 26, mwaka huu matukio ya kuvamiwa kwa watuhumiwa hao yalishika kasi.
 
Amesema kuwa Makachero wake walikuwa wakifuatilia nyendo za watuhumiwa hao na ndipo mmoja wao aliposhambuliwa na wananchi usiku wa jana alipokuwa katika maeneo ya Kituo kikuu cha mabasi mjini Dodoma.
 
Vitu vingine vilivyopatikana katika nyumba hiyo ya kulala wageni ya Ukio ni pamoja na kadi za ATM za Mabenki ya Barclays, Kenya National Bank.
 
Amesema walipokagua kitabu cha Wageni katika nyumba hiyo makachero wa Polisi walipata majina ya watu wengine wawili ambao ni Sihoja Lutongisha ma Boaz Adhero ambao wamekimbia na Polisi inawataka wajisalimishe wenyewe kabla ya kutiwa nguvuni.
 

No comments:

Post a Comment