Saturday, June 2, 2012

AFA KWA KUCHOMWA NA KITU CHENYE NCHA KALI,MWINGINE AJINYONGA.

Dinna Maningo wa Blog ya Mwana wa Afrika.

MKAZI mmoja wa Kitongoji cha Nyahongo Kijiji cha Bitiryo kata ya Kyang’ombe Wilayani Rorya Mkoani Mara ameuwawa kikatili   kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu za kichwani na shingoni na kisha mwili wake kutupwa ndani ya korongo la mto Kira.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amemtaja aliyeuwawa kuwa ni Wambura Kichere (34) na kwamba tukio hilo limetokea mnamo Mei 31 majira ya usiku saa isiyofahamika katika kijiji cha Bitiryo.

Kamugisha alisema kuwa marehemu huyo alikuwa ni mfanya biashara wa mkaa na dagaa na mpaka mauti yanamkuta alikuwa anatoka kwenye biashara zake.

Alisema kuwa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kuwa juhudi za kuwasaka waliohusika na mauwaji hayo zinaendelea.

Wakati huo huo,
Mwili wa mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Bhoke Nyangwe (20) mkazi wa kijiji cha Mangucha kata ya Gorong’a Wilayani Tarime amekutwa akiwa amefariki dunia kwa kujinyonga katika msitu wa asili wa wazee wa kimila  wa kijiji cha Masanga.

Kamugisha alisema tukio hilo limetokea mei 31 saa  9 alasiri huko katika kijiji cha Masanga nakwamba  mwili wa  marehemu umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa mazishi.

Alisema kuwa upelelezi unaendelea ikiwa ni pamoja na kubaini chanzo cha tukio hilo.

No comments:

Post a Comment