KIONGOZI WA UAMSHO ZANZIBARA AKUTANA
NA WAANDHISHI WA HABARI
Na Mohammed Mhina, Zanzibar
SIKU
moja tu baada ya Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein, kuzungumza
na Waandishi wa Habari Ikulu mjini Zanzibar kuhusiana na Vurugu
zilizotokea wiki iliyopita, leo Kiongozi wa kundi la Uamsho Sheikhe
Farid Hadi, amezungumza na Waandishi wa Habari na kusema kuwa
wataendelea na harakati zao ya kupinga Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar mpaka kieleweke.
Sheikhe
Farid ambaye amelaani vikali vitendo vya uharibifu wa mali ukiwemo wa
uchomwaji moto magari na baadhi ya makanisa mjini Zanzibar, amesema
pamoja na wao kulisaidia Jeshi la Polisi katika kukusanya taarifa za
kuwabaini wale wote waliohusika na uharibifu huo, lakini pia
wataendeleza harakati za kudai kura ya maoni ya kupinga Muungano wa
Jamhuri ya Tanzania.
Ingawa
alikataa wafuasi wake kushiriki katika vurugu, lakini amesema leo
wanakesha msikitini kuwaombea heri vija wote waliokamatwa kufuatia
vurugu hizo ili waachiliwe bila ya masharti.
Sheikhe
Farid pia amewalaumu baadhi ya vijana wakiwemo wa chama kimoja cha
siasa kuwa wao ni miongoni mwa wanzilishi wa vurugu hizo.
Amesema
kwa hatua hiyo anajenga imani kuwa miongoni mwa watu waliochoma
makanisa siku ya tukio hilo, walikuwa ni mmoja miongoni mwa vijana hao
na wanakamilisha taarifa zao ili kuwapatia Polisi kwa hatua zao.
Amesema
mbali ya kuwa Serikali imepiga marufuku mikutano na maandamano, lakini
Jumuiya yao ya Uamsho itafanya Mhadhara mkubwa Jumapili Juni 3, mwaka
huu kwenye Viwanja vya Lumbumba mjini Zanzibar mhadhara ambao utafuatiwa
na maandamamo yatakayofanyika Juni 26, mwaka huu.
Wakati
wa mkutano huo, Sheikhe Farid pia amevilaumu baadhi ya Vyombo vya
Habari hapa nchini na kusema wameandika habari zenye chumvi nyingi na
kuupotosha umma kwa kuongeza hofu miongoni mwa wananchi wa ndani na nje
ya Zanzibar.
Hata
hivyo Shehe huyo ameshindwa kufafanua baadhi ya hoja alizoulizwa na
waandishi wa habari kwa mfano kuzibwa kwa barabara kwa mawe na magogo ya
minazi ama kuchomwa matairi na makanisa kuwa inauhusiano gani na madai
ya kuwepo kwa muungano.
Mwisho
POLISI KIGOMA WAOKOA WATATU
WANAOTUHUMIWA KWA UCHUWI
Na Pardon Mbwate na Felister Chubwa, wa Polisi Kigoma
Jeshi
la Polisi mkoani Kigoma limefanikiwa kuwaokoa watu watatu waliokuwa
wamezingirwa na kundi la wananchi wakitaka kuwaua kwa tuhuma za
kujihusisha na vitendo vya ushirikina.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma SSP Joseph Konyo, aliwataja watu hao
waliokolewa kuwa ni Evania Sephanga(50), mkazi wa wilaya ya Kibondo,
Bruno January(46), mkazi wa kijiji cha Nyamhoza na mtoto mmoja mwenye
umri wa miaka kumi na mkazi wa kijiji cha Nyamhoza Kigoma mjini ambaye
jina lake linahifadhiwa.
Kamanda
Konyo amesema kuwa wiki iliyopita majira ya saa tisa mchana, watu hao
walizingirwa na kundi hilo kwa madai kuwa walimroga na kumuua msichana
mmoja aitwaye Faines Zawadi(20) mkazi wa kijiji hicho cha Nyamhoza
ambaye siku moja kabla ya kifo chake alionekana kama mtu
aliyechanganyikiwa na kuwa kama kichaa.
Alisema
katika tukio hilo, bibi kizee mmoja ambaye alikuwa mshirika wa kundi la
waliodaiwa kuwa wachawi, alifanikiwa kutoroka katika mazingira ya
kutatanisha alipojifanya kuwa anakwenda kujisaidia.
Kamanda
Konyo amemtaja bibi huyo aliyefanikiwa kutoroka kuwa ni Bibi Editha
Dosiyo mkazi wa kijiji hicho ambaye baadaye alipatikana na kuhojiwa
kabla ya kukabidhiwa kwa Idara ya ustawi wa jamii baada ya kuonekana
kuwa maisha yake yangekuwa hatarini.
Amesema
baada ya Polisi kupata taarifa za tukio hilo, walikimbia na kwenda
kuwaokoa kutoka katika mikono ya kundi la wananchi lakini wakiwa
wameshaadhibu ingawa ilikuwa haijawa kwa kiasi kikubwa.
Habari
zinasema kuwa, baadhi ya wananchi walipata taarifa kutoka kwa mtoto
aliyeokolewa akisema kuwa baadhi ya watoto waliofariki kijijini hapo,
akiwataja (majina tunayahifadhi) alikuwa akiwaona nyumbani kwao nyakati
za usiku wakiosha vyombo na baadaye kupewa chakula.
Siku
ya tukio hilo, baadhi ya wananchi walisema kuwa kabla ya bibi huyo
kutoweka alimnong’oneza jambo mjukuu wake ili amfanyie mareheme ikiwa ni
pamoja na kumruka mara saba kisha bibi huyo alitoweka akijifanya
anakwenda kujisaidia.
Walisema
mara baada ya bibi huyo kutoweka, mtoto huyo wa kiume ambaye ni
miongoni mwa waliozingirwa wakitaka kuuawa, aliamza kutekeleza maagizo
ya bibi huyo na alipomaliza kitendo cha kumruka kwa mara ya saba,
msichana yuyo ambaye alikuwa ni marehemu alizinduka na kuomba uji.
Wamesema
msichana huyo ambaye alikuwa mfu, alipewa uji na kunywa kisha
akapelekwa hospitalini ambako hadi sasa hali yake inasemekana kuwa
inaendelea vizuri.
Hata
hivyo Kamanda Konyo ametoa wito kwa wananchi kuacha kuchukua sheria
mkononi na badala yake watoe taarifa Polisi kwa kila jambo wanaloliona
kuwa linaweza kuleta uvunjifu wa amani ili hatua za haraka zichukuliwe
dhidi ya wahusika.
Mwezi
uliopita watu wawili mke na mume, waliuawa na kundi la watu wenye
hasira kisha miili yao kuchomwa kwa moto mkoani Kigoma baada wa
kutuhumiwa kuwa walikuwa ni wachawi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment