Na Waitara Meng’anyi, Tarime
MWENYEKITI wa Jumuiya ya kikrito Tanzania (CCT) Wilayani Tarime Mchungaji Joseph Mahugija amewataka viongozi wa serikali na wanasiasa kuithamini na kuitambua CCT kutokana na shughuli inazozifanya katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Wito huo umekuja siku chache baada ya maasa tarafa kuwagomesha wazee wa mila kwa kuwambia wadai posho ya shilingi 30,000/- zaidi ya pesa iliyokuwa imeimeandaliwa na mfadhili wao ambaye ni CCT Tanzania.
“Mfadhili wetu aliwandalia wazee wa mila kutoka koo 13 za Kikurya Chakula, usafiri na shilingi 10,000/- lika mmoja. Lakini baada ya kupata chakula cha mchana tu maafisa tarafa waliokuwa wamealikwa waliwashawishi wazee wagome kwa kudai kiasi kikubwa zaidi cha shilingi 30,000/-” aliliambia jibu la maisha ofisini kwake.
Mahugija alisema kuwa pamoja na kanisa kupewa nafasi ya kuihudumia jamii kiroho pia ina nafasi ya kuihudumia jamii kimwili na hilo ndilo linaloisuka CCT kuitaka jamii iachane na vitendo vya udhalilishaji wa watoto wa kike.
Alisema kuwa katika Mwaka 2012 CCT imejiwekea mikakati ili kufanikisha malengo yake. Alisema kuwa kila jumapili ya mwisho ya mwezi washirika wa makanisa yanayounda jumuiya hiyo watakuwa wakikutana kuanzia saa 8 alasiri katika kanisa litakalokuwa limechaguliwa na uongozi Wilayani hapa kwa ajili ya ibada zao.
Aliongeza kuwa katika mwezi wa kwanza washirika wanaounda CCT watakutana katika kanisa la Anglikani na mzunguko huo utaendelea kwa makanisa yote saba yanayoiunda katika wilaya ya Tarime.
Aliyataja makanisa hayo kuwa ni Anglican, AICT, Menonite, Methodist, KKKT, Jeshi la wokovu na Babtist.
“Watoto wa Sunday school watakuwa wakikutana kila jumamosi ya tatu ya mwezi katika siku hiyo watoto watafikisha ujumbe wao kwa jamii kwa njia ya nyimbo, ngonjera, mashairi, maigizo kuhusiana na mada husika katika siku hiyo” alisema Mahugija ambaye ni mchungaji wa kanisa la AICT mjini hapa.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa lengo lao ni kutaka kuwajengea watoto ujasiri wa kusema wazi kero wanazokabiliana nazo katika maisha yao hasa suala la ukeketaji kwa watoto wa kike ambalo linaonekana kitia mizizi zaidi katika Makoa wa Mara hasa Wilaya Tarime.
“Tuna lengo la kuwajengea watoto ujasiri wa kukataa mila zisizofaa na kuwa na uwezo wa kuwashawishi wazazi wao kuachana na mila hizi hatarishi” alisema Mchungaji huyo.
Aidha CCT imekusudia kuendesha semina na wazee wa mila wa koo 13 za wakurya ili kuwaelemisha kuhusu athari zinazotokana na vitendo wanavyoviendekeza vya ukeketaji kwa kudai kuwa wanalazimishwa na miungu yao.
“Njia nzuri ya kutatua migogoro ni kukaa pamoja na kujadiliana ili kufikia mwafaka, na wazee wetu hawa tusipo kaa nao hatuweza kuwaelemisha ili waelewe na waondokane na kile wanachokiamini wao kuwa ni sahihi na huu ni mgogoro mkubwa katika jamii ya wakurya” alieleza mahugija.
Na kuongeza kuwa “tunataka watambue mila nzuri na kuachana na mila potofu kwa kuwafundisha na kuwataka wao wenyewe kuchagua njia wanayoitaka kwa kuisema wazi ili tuwasaidie waondokane na hali waliyonayo sasa” alisema.
Mahugija anasema kuwa mwaka jana CCT iliwaita wazee katika kikao cha pamoja ili kujadiliana kuhusu ukeketaji lakini walishindana baada ya maafisa Tarafa kuingilia kati kuwataka walipwe kiasi kikubwa cha pesa mwisho wake semina ilivunjika.
“Viongozi wa siasa wamepelekea uongozi wa CCT kutofikia malengo yake. Lakini hata hivyo tuna mpango wa kufanya vikao sita kupitia kamati ya usuluhishi na maridhiano kwa kufanyia pale palipo na migogoro ya kikoo ili kuitatua pasipo kuonea upande wowote” alisema mwenyekiti wa CCT Tarime.
Mchungaji anasema kuwa kanisa kupitia CCT limegundua wanafahamu madhara ya ukeketaji ni swala la ukatili wa kijinsia lakini hawajaamua kuacha kwa kuwa ni sehemu ya kujipatia kipato.
“ Tumegundua kuwa wazee wa mila wazee wa mila wanalazimishwa na mizimu yao kuruhusu ukeketaji kuendelea. Wasipo fanya hivyo wanadai kuwa kuna miungu yao inawasumbuwa na kuwasababisha kuendelea kufanya hivyo” anasema.
Na kuongeza kuwa elimu ya kiroho ndiyo itakayobadili mtazamo wa ndani na wa nje wa jamii hii ya Kikurya na siyo kitu kingine. Tumeafikiana kufanya mkutano mkubwa utakaofanyika hapa Tarime katika ya mwezi wa sita na mwezi wa saba mwaka huuu.
Mkutano huo utakuwa ni wa kuwavuta watu katika imani ya kikristo na ufahamu juu ya Mungu wa kweli. Kutokana na mkutano huo tunaamini kuwa ushuhuda wa watu juu ya kuachana na mila hizi potofu wataondokana nazo.
Hata hivyo Mchungaji Mahugija alisema kuwa kazi kubwa wameachiwa wachungaji, mapatri, wainjilisti badala ya watu wote kuungana na kutimiza agizo la Mungu.
“ Wachungaji tunafanya sehemu yetu lakini biblia inasema kila aliyempokea kristo ana nafasi ya kumshuhudia na kulihubiri neno kwa wengine ili waachane na mazoea ya kidunia na kumpokea” Alisema Mahugija.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment