Sunday, August 22, 2010

MHANDO AVURUGA UCHAGUZI BUNDA

Mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM kwa wagombea wake wa nafasi za ubunge na udiwani kwa jimbo la Bunda uliokuwa umepangwa kufanyika kesho(Jumapili) umeahirishwa hadi hapo utakapopangwa tena .

Uzinduzi huo uliokuwa umepangwa kufanyikia kwenye eneo la Stendi ya Zamani mjini hapa kuanzia saa tatu asubuhi umeahirishwa kupisha ujio wa mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili hapa nchini Rose Muhando wilayani hapa.

Habari hii ni kwa msaada wa mwandishi kutoka bunda Christopher Maregesi

Muhando pamoja na kundi lake anatarajiwa kuwasili mjini hapa kesho kwa ajili ya kutumbuiza kwenye matamasha mawili ya kuchangisha fedha za ununuzi wa vyombo vya muziki kwa kwaya ya kanisa la KKKT la mjini hapa yatakayofanyika kwa nyakati tofauti katika uwanja wa Sabasaba na katika ukumbi wa chuo cha Ualimu cha Bunda kuanzia majira ya saa saba mchana.

Akiongea na gazeti hili leo katibu wa CCM wilayani humo Charles Mwangwale amesema chama hicho kimeamua kuahirisha mkutano wake huo ili kutoa fursa kwa wakazi wa jimbo hilo na wananchi kwa ujumla kuhudhuria tamasha la mwanamuziki huyo ambalo ni la kwanza kufanyika wilayani humo.

Kulingana na Mwangwale mkutano huo unaotarajiwa kuhutubiwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho wa wilaya na mkoa wakiongozwa na mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM Stephen Wasira sasa utapangiwa siku nyingine katika wiki ijayo kabla ya ule wa kuzindua kampeni hizo kwa jimbo la Mwibara uliopangwa kufanyika Agosti27 mwaka huu.

Mwangwale ametoa wito kwa wapenzi,wanachama na mashabiki wa chama hicho kuwa watulivu katika kipindi chote cha kampeni za uchaguzi bila kushiriki vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi yetu akiwaonya kuwa uchaguzi hautengui sheria zanchi hivyo atakayeenda kinyume  atakumbana na mkono wa dola.

No comments:

Post a Comment