Friday, June 1, 2012

HALMASHAURI YA WILAYA YA TARIME YATAKIWA KUONGEZA VYANZO VYA MAPATO.

 Na: Dinna Maningo, Tarime.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, imetakiwa kuongeza vyanzo vyake vya mapato ili iweze kujitosheleza yenyewe katika sehemu
kubwa ya matumizi siyo kutegemea ruzuku toka serikalini.

Akiwasilisha taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu taarifa ya fedha za halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 2011 Mkaguzi Mkazi Msaidizi Mkoa wa
Mara, Deogratius Waijaha alisema kuwa asilimia 91.4 ya halmshauri inategemea ruzuku kuu, hivyo lazima ianzishe na kubuni mipango ya kuifanya ijitegemee na sio kutegemea ruzuku kutoka Serikali kuu.

Waijaha alisema kuwa mapato ya ndani ambayo ni Sh. Bilioni 1,503,489,981 ni madogo sana ukilinganisha na ruzuku inayopewa halmashauri kutoka Serikali kuu ya kiasi cha Sh. Bilioni 20, 960,601,198.

Kwa upande wa matumizi ya kawaida alisema kuwa halmashauri ilitumia kiasi ch Sh. 17,604,608,018 kwa matumizi ya kawaida wakati ambapo mapato yake ya kawaida  yalikuwa Sh. Bilioni 18,238,072,617 ikionyesha
kwamba kulikuwa na baki (Balance) ya Sh. 633, 464,599.

Mkaguzi huyo alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2010/2011 halmashauri ilikusanya Jumla ya Sh. 1,503,489,981 kutoka katika vyanzo vyake ukilinganisha na bajeti yake ya Sh. 1,263,405,000 na kusababisha makusanyo zaidi ya Sh. 240,084,981 yakiwa sawa na asilimia 19.

Maeneo ya faini na tozo yalibajetiwa kukusanya kiasi cha Sh.583,405,00 lakini kiasi kilichokusanya  kilikuwa Sh. 549,769, 083 ikiwa na upungufu wa Sh. 33,635,916 sawa na 5.8 ambapo kodi ya ndani ilibajetiwa kiasi cha Sh. 680,000,000 lakini kiasi kilichokusanywa kilikuwa na Sh. 868,036,449  ikiwa ni ongezeko zaidi ya Sh. 188,036,449 ikiwa ni sawa na asilimia 27.7


Pia alisema katika manunuzi yenye jumla ya Sh. 32,050,000 yaliyokusanywa kupitia programu ya maendeleo ya kilimo (ASDP) yalikiuka kanuni Na. 49 ya manunuzi ya umma ya mwaka 2005 kwa kununua vifaa husika katika kiasi kidogo kidogo kupitia hati mbalimbali za malipo badala ya kufuata taratibu za Zabuni(Tender) kama ilivyokuwa ikihitajika na kanuni husika.

Hata hivyo Mkaguzi Waijaha alisema kuwa halmashauri imepata hati inayoridhisha ambapo aliipongeza kwa kusimamia vyema rasilimali na fedha za halmashauri na kwamba hali ya fedha ya halmashauri hadi Juni 30 2011na matokeo ya utendaji na mapato halisi kwa mwaka inawiana na viwango vya kimataifa vya uandaaji wa hesabu za fedha kwa sekta ya Umma.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,MWISHO,,,,,,,,,,
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,

No comments:

Post a Comment