Thursday, May 31, 2012

            MUWASA WANASAMBAZA MAJI MACHAFU MUSOMA

WAKAZI wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara wako katika hatari kubwa ya kukumbwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo Kichokicho na homa ya Matumbo kufuatia Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka MUWASA mjini Musoma kusambaza maji machafu kutoka ziwa Victoria.

Maji hayo yenye uchafu wa kutisha yanasambazwa na Muwasa kwa zaidi ya wiki moja sasa lakini licha ya Mamlaka hiyo kujua tatizo hilo imeshindwa kuchukua hatua kwaajili ya kunusuru maisha ya wananchi.

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Musoma hasa katika kata za Mwisenge,Makoko,Nyasho,Nyamatare na Mwigobero,wakizungumza mjini Musoma,wamesema licha ya kulalamikia suala hilo lakini uongozi wa Mamlaka umekuwa ukidai hauna fedha za kutosha za kusafisha maji kutoka ziwa Victoria kabla ya kuwafikia watumiaji wake.

Mkurugenzi mtendaji wa MUWASA mhandisi Gines Kaduri,akizungumzia suala hilo mbali na kukiri kupata malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu uchafu wa maji hayo lakini amesema tatizo hilo limesababishwa na uchafuzi wa ziwa Victoria jambo ambalo limesababisha kuongeza gharama kuwa za ununuzi wa dawa za kusafishia maji hayo.

Ameongeza kuwa Sistimu ya kusafishia maji katika Manispaa ya Musoma inatumia dawa badala ya mtambo hivyo amesema jibu la tatizo hilo ni kukamilika kwa mradi mkubwa wa Maji unajengwa katika mji ya Musoma na Bukoba huku akitoa wito kwa wadaiwa hasa taasisi za Serikali kulipa shilingi zaidi ya milioni 300 zinazodaiwa na mamlaka hiyo kwaajili kuwezesha kupata fedha za kusafishia Maji.

No comments:

Post a Comment