Friday, June 13, 2014

Timu ya soka ya Kenya kwenda Brazil

Rais Kenyatta akiwa na timu ya taifa Harambee Stars katika Ikulu mjini Nairobi
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameizawadi kwa kuifadhili timu ya taifa ya soka Harambe Stars ziara ya kwenda Brazil kutazama michuano ya kombe la dunia
Hafla ya kuikabidhi rasmi ufadhili huo timu hiyo, ilifanyika katika ikulu ya Rais Ijumaa ambapo wachezaji kumi na moja wa timu hiyo walikabidhiwa vyeti vya usafiri kwenda Brazil.
Mmoja wa wachezaji hao alifurahi sana na kusema kuwa hatua ya Rais Kenyatta kwao imetimiza ndoto yao. Rais atagharamia tiketi za timu hiyo kutazama michuano, malazi na usafiri ingawa haijulikani ni mechi zipi watakazotazama.

Kitendo cha Rais bila shaka ni jambo la kutaka kuwatia motisha wachezaji wa timu ya taifa ambao hivi karibuni waliicharaza Djibouti mabao mawili kwa moja katika duru ya kwanza ya michuano ya kuwania kombe la taifa bingwa Afrika baadaye mwakani.

Hatua ya Rais Kenyatta imewashangaza watu wengi sana nchini Kenya kwa kuwa timu ya taifa ya Kenya haikuwahi kufuzu kushiriki michuano hiyo, sasa wengi wanahoji hatua yake itasaidia nini?
Soka ya Kenya imekuwa ikikumbwa na changamoto si haba, usimamizi duni na wachezaji kukosa motisha ya kufanya vyema kwa ajili ya usimamizi huo mbaya.

Kenyatta na mkewe mama wa kwanza wa taifa Margaret Kenyatta wamewafadhili vijana hao kwa kima cha dola elfu arobaini. Akitoa ufadhili huo Kenyatta amesema lengo lake hasa ni kuwapa matumaini na motisha ya kuweza kuinua mchezo wa soka nchini Kenya.

Pia ni kama ishara ya kuthamini wachezaji hao ambao hivi karibuni walishinda kombe la Cecafa.
Kenyatta mwenyewe hatakwenda na kikosi hicho bali amewaasa vijana hao kuwa mabalozi wema wa Kenya nchini Brazil.

Ufadhili huu unakuja miezi sita baada ya Kenyatta kukubali kumlipa mshahara wa kocha wa timu hiyo kwa miakja miotano ijayo.

Kenya haijawahi kufuzu kwa michuano ya kombe la dunia lakini ziara hii kwa vijana wa Harambee Stars itawafungua macho huku wakiwa na azma ya kufuzu kwa michuano ya taifa bingwa Afrika mwaka 2015 baada ya kufuzu kwa duru ya pili na kujiandaa kuchuana na Lesotho tarehe 18 Julai.

No comments:

Post a Comment