Makachero wa Jeshi la Polisi
Zanzibar, wamefanikiwa kuzikamata silaha mbili na risasi 40 za Kivita zinazosadikiwa
kutumika katika matukio mbalimbali ya kihalifu likiwemo la mauaji ya Askari
Polisi lililotokea Machi 2, mwaka huko kwenye Hoteli ya Kitalii ya Pongwe Bay mkoa
wa Kusini Unguja Zanzibar.
Taarifa ya Afisa habari Mkuu wa
Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, imemkariri Mkurugenzi wa
Upelelezi Zanzibar SACP Yusufu Ilembo, akisema kuwa pamoja na kukamatwa kwa
silaha hizo pia Makachero hao wamewatia nguvuni majambazi watatu kati ya wanne
waliohusika katika tukio hilo la mauaji ya Polisi.
Mapema akizungumza na Waandishi
wa Habari mjini Zanzibar SACP Yusufu Ilembo, alisema silaha hizo zilikamatwa
nyumbani kwa mmoja wa watuhumiwa anayeishi eneo la Mkokotoni katika mkoa wa
Kaskazini Unguja zikiwa zimefungwa na vipande vya plastiki na vitambaa na
kuviringishwa katika waya mpya wa kupigilia madirisha.
Bila ya kuwataja majina yao kwa sababu za kiupelelezi, DCI
Ilembo ameainisha wazi kuwa baadhi ya watuhumiwa hao ni wenyeji wa Pangani
mkoani Tanga na wengine ni wenyeji wa Kisiwa cha Pemba Zanzibar.
Amesema katika mahojiano na makachero
wa Polisi, Majambazi hayo pia yalikiri kuhusika na matukio mbalimbali katika
mikoa ya Viisiwani na Mikoa ya Tanzania Bara matukio ambayo yangali yakichunguzwa
katika Vituo mbalimbali vya Polisi.
Watuhumiwa hao pia walipatikana
na vitu mbalimbali zikiwemo fedha taslimu shilingi 490,000 za Kitanzania, dolla
75 za Kimarekani, Euro na fedha kadhaa za Kichina pamoja na vitu mbalimbali
zikiwemo simu za mkononi.
Hata hivyo, SACP Ilembo amekiri
wazi kuwa kukamatwa kwa silaha hizo pamoja na watuhumiwa, kumetokana na taarifa
za siri za Raia wema zilizotolewa Polisi na kupelekea kufanyiwa kazi na kuleta
mafanikio hayo.
Amewaomba wananchi katika maeneo
mbalimbali kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za siri
zitakazowafichua watuhumiwa wakiwemo waliofanya na wanaotarajia kufanya makosa
ili waweze kufuatiliwa na kukamtwa na kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.
No comments:
Post a Comment