Friday, December 6, 2013

Waandishi wa habari waliofanikisha kukamatwa kwa Afisa Usalama feki wapongezwa Mkoani MaraBaadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mara wametoa pongezi kwa Waandishi wa habari waliofanikisha kukamatwa mtu aliyekuwa akijitambulisha katika idara mbalimbali za Serikali kuwa ni Afisa usalama kutoka Makao Makuu.

Wananchi hao walisema kuwa kitendo cha Mtu huyo kuwasiliana na Mkuu wa mkoa wa Mara na kuagizwa kwa baadhi ya Maafisa waandamizi wa vyombo vya usalama kuambatana nae kwa kile alichokuwa akidai kuwepo kwa mtandao wa watu wanaosafirisha risasi bila kumshtukia ni cha hatari  katika suala zima la usalama

“Hili tukio ni la kushtua sana maana mtu huyu amedanganya Mkuu wa mkoa na baadhi ya wakuu wa vyombo vya usalama bila kumshtukia na mpaka wanampatia sehemu ya kulala na chakula bila kutumia mbinu zao kumgundua ni hatari sana” alisme bw John Magafu mkazi wa Nyamatare.
                   Bw Liso Chacha - Afisa usalama feki

Katika hatua nyingine Bw Samson Chacha Mkazi wa Bweri Manispaa ya Musoma Mkoani Mara alisema kuwa kitendo hicho kimewatia shaka katika  suala la usalama na hivyo kuvitaka vyombo vya usalama kuongeza umakini.

Alisema wakati mwingine  baadhi ya idara za Serikali zinaona waandishi kama adui na kushindwa kuwapa ushirikiano jambo ambalo halipaswi kufumbiwa macho kwani kitendo kilichoonyeshwa na baadhi ya waandishi kumshtukia Afisa huyo feki ni cha kishujaa na kuonyesha wapo mstari wa mbele katika kuilinda nchi yao.

‘Mimi nawapongeza sana hawa waandishi maana wameonyesha kitendo cha kishujaa sana maana haiwezekani siku karibia tatu mtu huyo anacheza na akili za watu wenye dhamana ya ulinzi katika Mkoa mpaka waandishi ndiyo wamshtukie” alisema Bw Samson

Julai 17 Bw Liso Chacha alifika katika ofisi za ITV mkoani Mara na kuwakuta waandishi wa habari wa Channel Ten (Augustine Mgendi) na ITV (George Marato) ambapo alidai kuwepo kwa mtandao wa watu wanaovusha risasi kutoka kikosi cha 27 KJ Makoko na hivyo kuhitaji msaada wa waandishi hao katika kufanikisha lengo lake la kuwakamata watu hao.

Katika kujitambulisha kwake Bw Liso alisema kuwa ni Afisa usalama kutoka Makao Makuu na hivyo yupo mkoani Mara kwa Kazi Maalum  jambo ambalo lilitiliwa shaka na Waandishi hao pale walipomuuliza Makao makuu ya Usalama wa Taifa nchini yapo sehemu swali ambalo alionekana kushindwa kulijibu.

Kufuatia hatua hiyo Bw Liso alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Mara kutokana na taarifa zilizotolewa Polisi na waandishi hao ambapo taarifa hizo ndizo zilizowashtua viongozi mbalimbali ambao tayari walikuwa wamemuamini Bw Liso kama Afisa Usalama kutoka Makao Makuu.

Baada ya Ushahidi kutolewa na mashahidi saba akiwemo Afisa utumishi kutoka idara ya usalama wa Taifa,Desemba 4  hukumu ilitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Musoma Bw Richard Maganga, ambapo alisema kuwa Mahakama imeridhishwa na Maelezo ya Mashitaka wakiwemo mashahidi saba kutoka idara mbalimbali ambazo ni  Jeshi la Polisi,Mkuu wa utumishi idara ya usalama wa Taifa ,Waandishi wa habari na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na hivyo kumtia hatiani mtuhumiwa huyo kwa kujifanya Mtumishi wa idara ya Usalama wa Taifa na hivyo kwenda jela Miaka mitatu

No comments:

Post a Comment