Tuesday, November 19, 2013

MAKAMU WA RAIS DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA TATU WA AFRO – ARAB NCHINI KUWAITMakamu wa Rais wa Jmhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika mkutano wa mashirikiano baina ya nchi za Afrika na zile za Kiarabu, mkutano wa siku mbili unaofanyika katika nchini Kuwait. Mkutano huo unaohudhuriwa na viongozi wa nchi zaidi ya 70 unalenga kuimarisha ushirikiano wa Afrika na nchi za Kiarabu na unapitia makubaliano ya mkutano wa Sirte, Libya uliofanyika mwaka 2011. 
 
Mkutano huu unafanyika kukiwa na mabadiliko kadhaa ya kiasiasa, kiuchumi na kimkakati baina ya nchi za kanda hizi mbili huku taswira ya kukua kwa ushikiano huu zikionekana bayana kuwa muhimu zaidi sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Hii inatokana na nchi za kanda hizi mbili, kukabiliwa na changamoto nyingi zinazofanana na zinazohitaji majibu ya pamoja baina ya nchi za kanda hizi mbili. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na; mtikisiko wa uchumi, hali ya ulinzi na usalama, majanga yanayoikabili dunia, usalama wa chakula na ugaidi.
 
“Changamoto hizi hatuwezi kuzikabili wenyewe kama Tanzania ama kama Afrika. Tunahitaji wenzetu wa ukanda huu wa nchi za Kiarabu kushirikiana nasi. Katika umoja wetu tutafanikiwa kirahisi kuliko kama tutazikabili changamoto hizi tukiwa tumejitenga,” alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais.
 
Tanzania licha ya kuwa na wananchi wake katika nchi mbalimbali za dunia, tawimu zinaonesha kuwa, idadi kubwa ya wananchi hao wapo katika nchi za Kiarabu hali inayoashiria umuhimu wa kukuza mahusiano baina ya Tanzania pekee dhidi ya ukanda wa nchi za Kiarabu. Katika siku za hivi karibuni kupitia Diplomasia ya Uchumi, Tanzania imefungua njia kwa wawekezaji wa nchi za Kuwait, Oman na UAE na sasa taswira ya mahusiano ya Tanzania na nchi hizi ni ya kuvutia ambapo inatoa fursa za kunufaika kiuchumi kwa Tanzania kutoka katika ukanda huu kuliko kwa wadau wa maendeleo wa kanda zingine ambazo Tanzania imekuwa ikishirikiana nazo.
 
Akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya kikao hiki kwa Makamu wa Rais, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia yupo katika msafara wa Mheshimiwa Makamu wa Rais, Bernard Membe alisema, kazi kubwa ya mahusiano baina ya Tanzania na nchi za ukanda huu imejengwa na Rais Jakaya Kikwete na sasa milango imefunguliwa kwa Watanzania kuchangamkia fursa za maendeleo hasa katika suala zima la masoko ya bidhaa za kilimo, ufiugaji na utalii.
 
Katika Hotuba yake kwenye mkutano huu, Mheshimiwa Makamu wa Rais licha ya kutoa shukrani na salamu za Tanzania kwa Amiri wa Kuwait, Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah na wananchi wa Kuwait na kwa viongozi wote wan chi za kanda hizi mbili, Mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua kuwa Tanzania inatambua mahusiano ya kitamaduni, kihistoria na kijiografia yaliyopo baina ya kanda hizi mbili na kwamba zaidi ya theluthi mbili ya watu wa ukanda wa nchi za Kiarabu wanaishi Afrika hali inayochagiza umuhimu wa uhusiano wa kanda hizi. 
 
Pia Mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua kuwa, Mkutanouliofanyika Libya mwaka 2011, haukuonesha mafanikio ya wazi hasa katika miradi ya Maendeleo na akauomba mkutano huu wa Kuwait, kuhakikisha kanda hizi zinaongeza spidi ya kufanikisha malengo ya kimaendeleo, ili wananchi wa kanda hizi wazidi kunufaika kutokana na mahusiano haya.
 
Katika msafara huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais pia ameambatana na Waziri wa Kilimo na Chakula, Enginia Christopher Chiza, Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati wa SMZ, Ramadhan Shaaban, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Servacius Likwelile na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Uledi Mussa. Pia katika msafara huo wapo wabunge Hamad Rashid na Khalifa Khalifa.
Imetolewa na: Boniphace Makene
Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais

No comments:

Post a Comment