Tuesday, September 24, 2013

Tanzania ikomeshe ujangili’

                 na Lucy Ngowi -Tanzania Daima
UCHUMI wa Tanzania kwa kiasi kikubwa unategemea utalii wa wanyamapori, hivyo juhudi zinahitajika kukomesha ujangili.
Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexander Songolwa, alisema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Tembo kitaifa alipokuwa akimwakilisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Alisema juhudi za haraka zinahitajika kuhakikisha ujangili unakoma.
“Nchi yetu kwa kiasi kikubwa uchumi wake unategemea utalii, madini yakichimbwa wanaondoka nayo tunabaki na mashimo, tembo wakitunzwa vizuri wakazaliana wanabaki. Uchumi wetu umebebwa na wanyamapori, juhudi za makusudi zinahitajika kuokoa wanyama hao,” alisema.
Alisema ujangili unaoendelea hivi sasa nchini unasababishwa na wachache wenye uroho, hivyo Watanzania waikatae hali hii kwa kuipinga vikali.
Kwa mujibu wa Songolwa, kuna nchi zilizokuwa na tembo barani Afrika lakini hivi sasa hawana, hivyo Tanzania ikicheza muda si mrefu watatoweka.
Alizitaja nchi hizo kuwa ni Gambia, Swaziland, Burundi na Mauritania. Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na tembo wengi, inayoongoza ni Botswana.

No comments:

Post a Comment