Tuesday, July 2, 2013

WAFUGAJI WAIPA SERIKALI ANGALIZO KUNUSURU VURUGU

WAFUGAJI walioko kando  ya mapori ya akiba ya Ikorongo na
Grumeti wilaya za Serengeti na Bunda wameitaka  serikali kuwachukuliahatua askari wa mapori hayo wanaoshirikiana na Kampuni ya SingitaGrumeti Reserves wanaohusishwa na utesaji wananchi na mauaji ya mifugo wanapowakamata.

Mbele ya viongozi wa serikali ,madiwani na Kampuni ya Singita Grumeti Reserves kwenye ukumbi wa Mandela Issenye wakati wa Kongamano lililoandaliwa na shirika la Maendeleo ya Wafugaji Jamii yaWataturu(Shimwajawa)wafugaji walisema hali ilipofikia inahatarisha uhifadhi kwa kuwa hakuna ushirikiano pande hizo mbili.

Gidai Murasi(75) mfugaji kutoka Hunyari wilayani Bunda kwa hasira alinukuu maneno ya Mwalimu Nyerere kuwa “ili tuendelee tunahitaji ardhi,siasa safi,watu na uongozi bora…tatizo ni uongozi bora…kama inafikia wahifadhi wanaua ng’ombe wetu ili tuwe masikini….kuna mapato gani ya uhifadhi yanaweza kutuhudumia sisi kwa umaskini
wanaotusababishia?”alihoji.

Alisema  wafugaji hao  ni kama hawako Tanzania ,maana kwa umri wake hajaona taifa linalowafanya wananchi wake kuwa maskini…”mimi sijasoma…maisha yangu yote ni ng’ombe,natunza na kusomesha watoto kwa mifugo…hivi kwa nini mnatengeneza majambazi…nchi hii itakuja kuwa navita mbaya sana”alisema.

Murasi alisema serikali inatambua tatizo lao ni malisho hasa baada ya
kuchukua maeneo yao na kuwa hifadhi,wakati wa kiangazi hali huwa mbaya zaidi,lakini kama kungekuwa na uhusiano wangeruhusiwa kuingia hatua chache na kunywesha mifugo kwa kuwa mto walioutegemea nao ulichukuliwa na hawakuchimbiwa malambo.

Esther Balebe mkazi wa Issenye alisema mahusiano mabaya yaliyopo kwa wahifadhi na wafugaji yanachangia kukithiri kwa ujangili,kwa kuwa hata akina mama wakienda kuokota kuni  wanadhalilishwa wanapigwa na kutendewa mambo yasiyofaa.

Joash Tangera alisema udhaifu wa serikali utakuja kuibua matatizo
makubwa kati ya pande hizo,kwa kuwa hiyo ni vita ya ndani ,lakini iko siku itakuja kuwa kubwa,wafugaji hawapendi kuingiza mifugo hifadhini lakini tatizo kubwa ni malisho,baada ya eneo lao kuchukuliwa na kuwa kwa mahusiano wangeruhusiwa kuchungia mita chache wakati wa kiangazi.

Walihoji sababu za serikali kuwafidia wafugaji wa Monduli baada ya
ng’ombe wao kufa kwa ukame,wakati nao wana matatizo kama hayo,wengine wanauawa na pia wanyama wanaua watu,mifugo na kula mazao na hakuna fidia iliyowahi tolewa.

Gijeshi Gambarara mkazi wa Iharara alisema ng’ombe wake watatu
walifukuzwa kwa helkopita yaSingita Grumeti Reserves  na kushuka
karibu upepo ukawapelekea kuzama mtoni na kufa,huku shamba lake la ekari 10 likiwa limeliwa na wanyama pori,lakini hajawahi pata
msaada,na kuwa uwekezaji huo haufai kwa jamii.

Wafugaji walisema mpango wa mwekezaji ni kuua mifugo yao ,hata kwenye mipango yake hakuna mkakati wa kusaidia wafugaji.

Baadhi walisema serikali isisubiri matatizo kama ya Mtwara ndio
ichukue hatua bali wakae chini watafute ufumbuzi wa pande hizo,kwa kuwa madhara yake ni makubwa ikiwemo ongezeko la ujangili wa tembo kwa kuwa jamii haioni faida ya kutoa ushirikiano kwa sekta inayowatia umaskini.

Mwenyekiti wa Shimwajawa Gohebu Gorobani na katibu wake Mnada Mayonga walisema lengo la kukutanisha wahifadhi,wafugaji na serikali ni kutafuta muafaka kwa maslahi ya taifa kwa kuwa kuna kila dalili za uvunjifu wa amani.

Kaimu Katibu Tawala wilaya ya Serengeti ambaye ni afisa tarafa ya
Grumeti Paulo Shanyangi alisema njia hiyo inalenga kuleta muafaka, serikali itachukua hatua za haraka ili kuleta mahusiano,akiitaka kampuni ya Singita Grumeti kusaidia wananchi upande wa malambo ya maji.

Kwa upande wa Kampuni ya Singita Grumeti waliomba suala hilo
lisichukuliwe kwa jazba madhara yake ni makubwa kwa kuwa watakaoumia ni vijana wao ,kwa kuwa mwekezaji hakuja na watu wake,bali watumie njia ya kuzungumza kwa kuwataja wahusika hatua zichukuliwe.

Hivi karibuni askari hao wametuhumiwa kuua ng’ombe 51 na wengine 100 kupotea mali ya Kiteku Meshinya mkazi wa Mariwanda wilayani Bunda,baada ya kuwakamata na kisha kuwafukuza kwa magari na kuzama mto Rubana.

Mwanzoni mwa mwaka huu ng’ombe zaidi ya 40 mali ya Kijiji mkazi wa Motukeri waliuawa kwa mtindo huo,na mwaka 2008 ng’ombe 65 wa Gorobani Marosina walizamishwa mtoni,huku ikidaiwa kijana mmoja naye alikufa maji baada ya kumkimbiza na kutumbukia mtoni.

Hata hivyo uongozi wa Senapa,ofisi ya mkuu wa wilaya na mkurugenzi halmashauri ya Bunda hawakuhudhuria kongamano hilo licha ya kuwa na taarifa.
Mwisho.
 WAFUGAJI WAKATI WA KONGAMANO LILILOWAKUTANISHA NA WAHIFADHI NA VIONGOZI WA SERIKALI CHINI YA SHIRIKA LA SHIMWAJAWA ISSENYE WILAYANI SERENGETI
 MMOJA WA WAFUGAJI KUTOKA MARIWANDA WILAYANI BUNDA AKIELEZA MIKASA IWAKUTAYO WAFUGAJI
HATA AKINA MAMA WAFUGAJI HAWAKUSITA KUSEMA WANAVYOTENDEWA NA WAHIFADHI WAWAKAMATAPO HIFADHINI WAKIWA NA MIFUGO AMA WANASENYA KUNI

No comments:

Post a Comment