Monday, June 10, 2013

Taifa Stars yawasili leo ikitokea Morocco, Poulsen asema Refa aliuharibu mchezo wetu.


IMG_5878
 Wachezaji wa Taifa Stars wakiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere Jumatatu alfajiri wakitokea Morocco.
IMG_5874
IMG_5825
-Asema adhabu ya kadi nyekundu haikuwa na ulazima
-Asema wangecheza 11 ushindi ulikuwa wazi
 
Kocha wa Timu Taifa stars  Kim Poulsen amesema refa wa mechi ya Taifa Stars na Morocco iliyopigwa Marrakech Jumamosi kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la  Dunia Brazil mwakani aliuwa mchezo kwa kutoa kadi nyekundu kwa mchezaji Aggrey Morris.
 
Akitoa maoni ya mchezo huo, Poulsen alisema alisikitishwa na jinsi refa huyo alitoa adhabu kali ambayo haiendani na kanuni za FIFA.
 
Aggrey Morris alioneshwa kadi nyekundu baada ya kugongana na Abderazak Hemed Allah ambaye aliifungia Morocco bao la kwanza katika dakika ya 37.
 
“Hakuwa na sababu ya kumuonesha Morris kadi nyekundu kwani tayari alishawapa Morocco penalti, alisema Poulsen huku akiongeza, “FIFA imeshawaonya marefa mara kadhaa dhidi ya kuua mchezo kwa namna hii ya kutoa adhabu kali kupita kiasi.”
 
Poulsen alisifu wachezaji wake na kusema licha ya kucheza pungufu walipambana uwanjani na kufanikiwa kupata bao kupitia kwa Amri Kyemba. Morocco walishinda kwa 2-1.
 
“Kama tungecheza kumi na moja hadi mwisho nina uhakika tungeshinda mechi hii lakini refa aliiua mechi na huwezi kufanya hivi katika mechi ngumu kama hii,” alisema Poulsen.
Kocha huyo alisema kupata goli la ugenini unapochez na timu ngumu kama Morocco ni jambo la kujivunia hasa mnapokuwa pungufu uwanjani.
 
Alisisitiza kuwa sasa wanaelekeza nguvu zote katika mechi shidi ya Ivory Coast Jumapili ijayo. “Mambo ya Morocco yamekwisha sasa tunafikiria namna ya kushinda mechi ya Jumapili.
 
Tanzania iko katika kundi C inayoongozwa na Ivory Coast yenye pointi 10, Tanzania 6, Morocco 5 na Gambia 1.
 
Taifa Stars imerejea Jumatatu alfajiri kutokea Marrakech Morocco na itaendelea na kambi ya wiki moja ili kujiandaa na mechi dhidi ya Ivory Coast.
 
Nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja alisema wachezaji walicheza kwa ari kubwa na walifurahishwa na jinsi watanzania walijitokeza kwa wingi.
 
“Tulipata faraja kubwa sana kuwaona watanzania wengi uwanjani…mambo ya Morocco yameisha sasa tuangalie Ivory Coast,” alisema.
 
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe ambaye bia yake inadhamini Taifa Stars, alisema wacezaji walijitahidi hasa ikizingatiwa walicheza pungufu na hata wakafanikiwa kufunga bao moja.
 
“Katika hali kawaida, wachezaji wengine wangekata tamaa lakini bao hili moja linaonesha kuwa wachezaji walikuwa na ari ya kupata ushindi,” alisema Bw Kavishe.
 
Alisema wao kama wadhamini wana imani kubwa na Taifa Stars na kwamba wanaamini hii ni safari ya mafanikio ambayo ilianza mwaka mmoja uliopita tangu Bia ya Kilimanjaro Premium Lager ianze udhamini huo.

No comments:

Post a Comment