Na Grace Michael
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya unaendelea kutekeleza mpango wake wa kuhakikisha utaalam wa madaktari bingwa wachache waliopo hapa nchini unatumika kitaifa na unawanufaisha Watanzania wote.
Kutokana
na hali hiyo, timu ya madakati bingwa saba na watalaam wengine wawili
itaanza kazi rasmi katika Mkoa wa Katavi siku ya Jumatatu katika
Hospitali ya Mpanda na timu hiyo itahudumia wananchi na wanachama wa
Mfuko kwa muda wa siku saba.
Mbali
na kutoa huduma katika Mkoa mpya wa Katavi, timu hiyo pia ianatarajiwa
kutoa huduma katika Mkoa wa Rukwa mapema Julai na itadumu kwa muda wa
siku saba lengo ni kutoa huduma hizo za kitaalam kwa wananchi hao ambao
kwa muda mrefu wamekosa fursa hiyo.
Akizungumza
na timu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba alisema kuwa lengo
la Mfuko kugharamia mpango huo ni kuhakikisha utaalam wa madaktari
bingwa ambao ni wachache hapa nchini unatumika kitaifa.
“Kwanza
niwashukuru sana madaktari kwa kukubali kushirikiana na sisi, inatupa
nguvu ya kuendelea na mpango huu lengo kubwa ni kuwahudumia wananchi
wote bila ya ubaguzi…wananchi na wanachama watatakaokuwa na mahitaji ya
kuonana nanyi Nawaomba sana muwahudumie kwa kadri ya utaalamu wenu ili
kila mwananchi anufaike na uwepo wenu kwa muda mtakaokuwa huko,” alisema
Bw. Humba.
Alisisitiza
kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mbali na mpango huo utaendelea na
mikakati mingine ya kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika uboreshaji
wa huduma za afya lakini pia kuwasaidia wananchi kutambua afya zao
mapema kupitia mpango wa elimu kwa umma utakaokwenda sambamba na upimaji
wa afya bure kwa wananchi.
Timu
ya Madaktari hiyo ni pamoja na Dr. Billy Aonga (bingwa wa Mifupa), Dr.
Albert Ulimali (bingwa wa Usingizi), Hillary Tesha (Mtalaam wa Mazoezi
tiba) na July Nkwama (Mhudumu wa Chumba cha upasuaji) wote kutoa Taasisi
ya Mifupa (MOI).
Wengine ni Dr Delila Kimambo (Bingwa wa magonjwa ya
kawaida na moyo), Dr. Edna Majaliwa (bingwa wa watoto) wote kutoka
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Timu
hiyo pia itajumuisha na Daktari bingwawa upasuaji kutoka Hospitali ya
Rufaa Mbeya na Daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na kawaida
kutoka hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Rukwa.
Kutoka
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Mwenyekiti wa Bodi Balozi Ally Mchumo,
Mjumbe wa Bodi, Bi Lyidia Choma na Mkurugenzi Mkuu.
No comments:
Post a Comment