Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mariwanda wilayani Bunda Samson Kisung’uda
Juni 22,2013.
Mara-ASKARI wa mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti kwa kushirikiana na Kampuni ya Singita Game
Reserve ,wanatuhumiwa kusababisha vifo vya ng’ombe 51na 100 kupotea wa mkazi mmoja wa
Kijiji cha Mariwanda wilayani Bunda.
Tukio hilo linadaiwa kutokea
aprili 22,majira ya saa 10.30 jioni mwaka huu katika eneo la Mto Rubana eneo la
Mariwanda limethibitishwa na polisi na ofisi ya mifugo wilaya ya Bunda na uongozi
wa kijiji hicho.
Kiteku Meshinya Kisereta mwenye mifugo
akiongea na Mwandishi wa blog hii katika ofisi ya Wasaidizi wa Kisheria na Haki
za Binadamu wilayani Serengeti (WASHEHABISE)alisema,chanzo cha vifo hivyo ni
askari hao waliowakamata kwa kuingia hifadhini kuwasagwa na kuwazamisha mtoni
ili wavuke na kufa 51,na wengine 100 hawajaonekana.
“Mizoga iliyoopolewa majini 51 na
kuthibitishwa na polisi na ofisi ya mifugo…wengine 100 haijulikani
walikopotelea..,siku hiyo nilitaarifiwa kupitia simu namba 0682 760012,0756 019672
na 0786 757603,kuwa ng’ombe wangu wamekamatwa na askari wa Grumeti nikalipe
faini…wakati najiandaa kwenda nikataarifiwa na mchungaji wangu kuwa
wamezamishwa mto Robana”alisema.
Alisema alilazimika kujulisha
uongozi wa kijiji ,mkuu wa wilaya ya Bunda akamtuma Oc Cid ambapo walifika na
kukuta ng’ombe 46 wamekufa maji,na aprili 24 walipata mizoga 5 na kufanya idadi
ya 51,lakini wengine 100 haikujulikana wako wapi na hakuwahi kuwapata.
“Si mara ya kwanza ng’ombe wangu
kukamatwa kutokana na shida ya maji wanajikuta wamevuka…askari hupiga simu ama
wanasema tuma fedha ya faini kwa Mpesa…ukilipa wanaachiwa ingawa hawatoi
stakabadhi….hata siku hiyo walinipigia niende na fedha,ajabu wakaamua
kuwasukumia mtoni baada ya kuchelewa,”alisema kwa masikitiko.
Aliwataja askari waliohusika na
tukio hilo kuwa ni Peter Gorobani na Juma Mwiyuga askari wa Kampuni ya Singita
Grumeti Reserves,ambao walikuwa chini ya uongozi wa Anthony Mamboleo wa Pori la Ikorongo ambaye
yuko chini ya Mkurugenzi wa wanyamapori.
Serikali ya Kijiji
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji
cha Mariwanda Samson Kisung’uda alisema tukio hilo ni mwendelezo wa Manyanyaso
wanayopata wananchi dhidi ya mwekezaji na wizara,”wananchi wamefikia hatua
mbaya maana hawa mwaka juzi walifukuza kijana aliyekuwa anachunga ng’ombe
akazama mtoni akafa,hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika”alisema.
Alisema mambo kama ya Mtwara
huenda yakajitokeza kwa kuwa wananchi wanahasira na kampuni ya Singita Grumeti
Reserves kutokana na vijana wake wanavyowatendea unyama wananchi,”sisi viongozi
tunapata shida sana…siku hiyo ilikuwa wanaungana na vijiji vya jilani kwenda
kuteketeza magari yao….tulitumia ushawishi kuwatuliza …kukaa kimya bila
watakuja shangaa”alibainisha.
Kutokana na ukubwa wa tatizo
waliwasiliana na Mbunge wa jimbo hilo Steven Wasira ambaye ni Waziri ofisi ya
Rais Uhusiano na kuagiza kuandika barua kwenda kwa waziri wa Maliasili na
Utalii ili aweze kuchukua hatua.
Barua hiyo ya mei 10,2013 imefafanua
ilivyotokea na kunakilishwa kwa viongozi mbalimbali ,akiwemo mkuu wa mkoa wa
Mara ,mbunge.Rpc,Dc na Ocd Bunda kwa Taarifa,hata hivyo hawajapata majibu
kutoka wizara licha ya Mbunge wao kuwahakikishia kuwa alimkabidhi waziri mwenye
dhamana.
Watuhumiwa.
Anthony Mamboleo askari wa pori
la Ikorongo alipoulizwa kwa njia ya simu,alikiri kuwepo kwa tukio hilo,lakini
hakutaka kulizungumzia”naomba umtafute kaimu meneja wa Ikorongo akupe taarifa
zaidi”alisema na kukata simu.
Juma Mwiyuga(askari wa Singita
Grumeti game reserves(VGS)alisema yeye alishatoa maelezo polisi ilivyotokea
,”kwanza nilikuwa post sikuwepo…lakini nilishatoa maelezo polisi…haya mambo
mimi sipendi kuyazungumzia zaidi”alijibu.
Peter Gorobani alipoulizwa
alisema hilo suala hawezi kulisemea mpaka afuatwe ofisini kwake atasema mambo
mengi,alipoulizwa ofisi yake ilipo ili blog imtafute akasema”sasa unataka kuja
ofisini….aaah,kwaheri”akakata simu.
Kaimu Meneja Ikorongo.
Upendo Kimaro kaimu Meneja mapori
ya akiba ya Ikorongo na Grumeti alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikiri kuwepo
lakini akasema kuna anayeshughulikia”sisi tunafanya kazi chini ya Kanda tunatoa
taarifa Kikosi cha Kuzuia Ujangili (KDU)wanasema suala hilo liko Mahakamani
tafuta katibu Mkuu ama Mkurugenzi wa wanyama pori watalisemea maana
tunawashitaki sisi”alisema.
Hata hivyo suala hilo
halijafikishwa mahakamani kama alivyodai meneja huyo ,alipotakiwa kueleza
jalada lipi liko mahakamani kwa kuwa jalada la polisi BND/INQ/22/2013
lililofunguliwa na Meshinya dhidi yao halijafikishwa mahakamani,alisema”basi litakuwa
polisi…maana nasi tuliwashitaki”alisema bila kutaja mashitaka hayo.
Mkurugenzi akana hana
taarifa.
Mkurugenzi wa Wanyamapori
Tanzania Alexander Songorwa alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu malalamiko ya
mfugaji huyo alisema hana taarifa,”wewe ni Mwandishi wa pili ,juzi nimeulizwa
kwa kweli sina taarifa nafuatilia nitajulisha kama kuna maandishi yoyote
yameletwa na mtu wetu wa huko”alisema.
Hata hivyo alijibu kwa ujumbe
mfupi wa simu(sms)kuwa hakuna taarifa iliyowahi wasilishwa kwake na maafisa
wake kama walivyodai.
Ofisa Mifugo akiri.
Masuke Ogwa ofisa mifugo wilaya
ya Bunda kupitia simu ya Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Bunda
Simon Mayeye alikiri kushuhudia mizoga ya ng’ombe na kuwa walikufa
maji,”mazingira yaliyopelekea wafe ni kazi ya polisi…lakini kwa ujumla
nilishuhudia ng’ombe kama 51 au 52 wamekufa na ripoti ipo nitaikabidhi polisi
“alisema
Singita.
Afisa mahusiano wa Kampuni ya
Singita Grumet Game Reserves Shaabani Madanga alisema analifahamu suala hilo,na
mlalamikaji amelifikisha kwa Waziri,”hata hivyo kwa huko linashughulikiwa na
Ikorongo Game Reserves”alisema.
Wanaharakati.
Mwenyekiti mtendaji wa shirika la
Wasaidizi wa Kisheria na Haki za Binadamu wilaya ya Serengeti Samweli Mewama
alisema ,uwekezaji unaowatia umaskini wananchi huibua hasira na chuki na kuomba
serikali kuchukua hatua ili mfugaji atendewe haki.
Mtandao wa wafugaji ,warina asali
na waokota matunda(Ping’os)walisema wanafuatilia tukio hilo ili kuhakikisha
mwananchi huyo anatendewa haki,kwa mazungumzo ama mahakamani.
Waziri
Juhudi za kumpata Waziri wa
Maliasili na Utalii Khamisi Kaghasheki hazikuzaa matunda baada ya simu yake
kuita bila kupokewa,na hata alipotumiwa maswali kutaka kujua hatua gani
imechukuliwa,licha ya kupokelewa lakini hakujibu.
Matukio Mengine.
Blog hii imebaini oktoba 8,2008 askari wa Ikorongo na
Kampuni ya Singita Grumeti Reserve aliswaga ng’ombe kwa kutumia magari na
kusababisha ng’ombe 65 mali ya Gorobani Marosina mkazi wa Issenye
wenye thamani ya sh,24,600,000 kuzama Mto Robana na kufa na kuthibitishwa na
Paulo Munkhoma Augustine afisa mifugo na taarifa yake yenye
kumb.Na.Vy/a.20/1/30 kwenda kwa Dc ikionyesha tathimini aliyotakiwa kulipwa .
Hata hivyo licha ya Tathimini
kuonyesha alivyostahili kulipwa kwa kuzingatia bei ya mnada wa mwezi huo
,mfugaji huyo alitishwa na uongozi wa wilaya kushitakiwa na kulipwa sh.mil.7.
Mwanzoni mwa Mwaka huu kampuni
hiyo kwa staili hiyo ya kuswaga kwa kutumia magari walizamisha ng’ombe zaidi ya
40 mali ya mkazi wa Motukeri aliyejulikana kwa jina la Kijiji,naye alitishiwa
na hakulipwa fidia .
Mwisho,ufuatiliaji unaendelea.
No comments:
Post a Comment