Monday, May 6, 2013

MBWANA SAMATTA, YONDANI, KAPOMBE, BOCCO, NANI KUWA MCHEZAJI BORA WA TANZANIA - TCHETCHE, OKWI, NIYONZIMA NA KIIZA NANI KUWA MCHEZAJI BORA WA KIGENI?

KLABU ya Azam imeingiza wachezaji wawili katika kinyang’anyiro cha tuzo ya Mwanasoka Bora kwenye Tuzo za Wanamichezo Bora za Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) 2012/2013.

Uongozi wa TASWA kupitia kwa katibu wake mkuu Amri Muhando aliwataja wanandinga hao wa Azam ambao wameingia katika tuzo hizo ambazo zitafanyika baadaye mwaka huu kuwa ni Khamis Mcha pamoja na John Bocco (Adebayo).

Hata hivyo, katika vita hiyo ya kumtafuta mwanasoka bora wa Tanzania wachezaji hao watachuana vikali na Kevin Yondani (Yanga), Shomary Kapombe (Simba) anayeshikilia tuzo hiyo, Mbwana Samatta pamoja Thomas Ulimwengu wote kutoka TP Mazembe ya DRC.

Azam pia imeingia mchezaji mmoja katika kipengele cha tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kigeni anayecheza Tanzania, ambaye ni Kipre Tchetche kutoka Ivory Coast atakayechuana na Mganda Emmanuel Okwi aliyekuwa Simba na sasa anakipiga katika klabu Etoile du Sahel ya Tunisia.

Wachezaji wengine katika kipengele hicho ni, Haruna Niyonzima na Hamisi Kiiza (Yanga).

Upande wa wanasoka wa kike, Fatuma Mustafa atachuana na Asha Rashid, Mwanahamisi Omary, Sofia Mwasikili anayeshikilia tuzo huyo pamoja na Esther Chabruma.

Katika hatua nyingine Muhando alisema aliongeza kuwa kwa upande wa mchezo wa ngumi za kulipwa Francis Miyeyusho anachuana vikali na Ramadhan Shauri, Thomas Mashali, Said Mbelwa na Francis Cheka.

No comments:

Post a Comment