Yanga SC; Mabingwa 2012/2013 |
Na Prince Akbar, Tanga
YANGA bingwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2012/2013. Habari ndiyo hiyo. Yanga ya Dar es Salaam imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu jioni hii, kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo wa ligi hiyo baina ya wenyeji Coastal Union na Azam FC ya Dar es Salaam, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo.
Matokeo hayo yanamaanisha, Azam FC waliokuwa washindani wakuu wa Yanga SC yenye pointi 56, hawawezi tena kufikisha pointi hizo ambazo wanazo mabingwa hao wapya, kwani hata wakishinda mechi zao nyingine mbili zilizobaki, watamaliza na pointi 54.
Mchezaji aliyepeleka shangwe na vigelegele Jangwani leo ni Danny Lyanga, ambaye aliifungia Coastal bao la kusawazisha dakika ya 72.
Lyanga ambaye ilibaki kidogo asajiliwe Yanga msimu huu kutoka Toto Africans, kama si kuzidiwa kete na Coastal, alifunga bao hilo katika mpira wake wa kwanza kuugusa tangu aingie kuchukua nafasi ya Suleiman Kassim ‘Selembe’ dakika ya 71.
Alifunga bao hilo, baada ya kupokea pasi nzuri ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Pius Kisambale, ambaye ni mdogo wa kiungo wa Wana Jangwani hao, Athumani Iddi ‘Chuji’.
Azam ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika mchezo wa leo, lililofungwa na beki Aggrey Morris kwa penalti dakika ya 60, baada ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Gaudence Mwaikimba kuchezewa rafu kwenye eneo la hatari na beki Yussuf Chuma- na refa Andrew Shamba wa Pwani akaamuru pigo hilo.
Baada ya bao hilo, Coastal walionekana kufanya jitihada za wazi kusawazisha na ndipo Lyanga aliyetokea benchi akawapa ubingwa Yanga.
Matokeo haya yanakuwa sawa na Coastal kulipa fadhila kwa Yanga, kwani hata wao, ubingwa wao pekee wa Ligi Kuu waliochukua mwaka 1988 ulitokana na ‘msaada’ wa wana Jangwani huo.
Msimu huo, mshindani wa Coastal katika mbio za ubingwa alikuwa Simba SC ambaye ili kutwaa taji hilo, alihitaji kushinda mechi ya mwisho dhidi ya African Sports mjini Tanga huku akiomba Wagosi wa Kaya walale mbele ya Yanga Uwanja wa Taifa.
Lakini Yanga wakacheza ‘kichovu’ na Athumani China akaenda kupiga penalti ‘kiviivu’ akakosa, Coastal ikishinda 2-0 na kusherehekea taji pekee la ubingwa wa Ligi Kuu, licha ya Simba pia kushinda 3-0 dhidi ya Sports Tanga.
Hili linakuwa taji la 24 kwa Yanga, tangu watwae kwa mara ya kwanza mwaka 1968.
Aidha, huu unakuwa msimu wa pili mfululizo, Azam wanaukosakosa ubingwa wa Ligi Kuu, baada ya msimu uliopita pia kuzidiwa kete na Simba SC.
Kikosi cha Coastal Union leo kilikuwa; Shaaban Kado, Hamad Khamis, Othman Tamim, Philip Mugenzi, Yussuf Chuma, Abdi Banda, Joseph Mahundi, Razack Khalfan, Pius Kisambale/Mohamed Soud dk85, Suleiman Kassim ‘Selembe’/Danny Lyanga dk71 na Twaha Shekuwe.
Azam FC; Mwadini Ally, Himid Mao, Erasto Nyoni, David Mwantika, Aggrey Morris, Jabir Aziz/Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’ dk75, Brian Umony/Seif Abdallah Karihe dk68, Ibrahim Mwaipopo, Gaudence Mwaikimba/Abdi Kassim ‘Babbi’ dk82, Humphrey Mieno na John Bocco ‘Adebayor’.
ORODHA MABINGWA WA JUMLA LIGI KUU:
1965 : Sunderland (Dar es Salaam)
1966 : Sunderland (Dar es Salaam)
1967 : Cosmopolitans (Dar es Salaam)
1968 : Yanga
1969 : Yanga
1970 : Yanga
1971 : Yanga
1972 : Yanga
1973 : Simba
1974 : Yanga
1975 : Mseto SC (Morogoro)
1976 : Simba
1977 : Simba
1978 : Simba
1979 : Simba
1980 : Simba
1981 : Yanga
1982 : Pan African
1983 : Yanga
1984 : Simba
1985 : Yanga
1986 : Tukuyu Stars (Mbeya)
1987 : Yanga
1988 : Coastal Union (Dar es Salaam)
1989 : Yanga
1990 : Simba
1991 : Yanga
1992 : Yanga
1993 : Yanga
1994 : Simba
1995 : Simba
1996 : Yanga
1997 : Yanga
1998 : Yanga
1999 : Mtibwa Sugar (Morogoro)
2000 : Mtibwa Sugar (Morogoro)
2001 : Simba
2002 : Yanga
2003 : Simba
2004 : Simba
2005 : Yanga
2006 : Yanga
2007 : Simba (Ligi Ndogo)
2008 : Yanga
2009: Yanga
2010: Simba SC
2011: Yanga SC
2012: Simba SC
2013: Yanga SC
No comments:
Post a Comment